Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018

Hon. January Yusuf Makamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bumbuli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia, taarifa ya Kamati. Nianze kwa kuipongeza Kamati kwa kazi nzuri ambayo imeifanya na kwa taarifa nzuri ambayo imeitoa. Pia nishukuru Mwenyekiti wa Kamati na Wajumbe kwa ushirikiano mzuri ambao wamekuwa wanatuonesha, kwa msaada ushauri na maelekezo mbalimbali, ambayo wamekuwa wanatupatia, kwa hiyo nampongeza sana Mwenyekiti, Mheshimiwa Sadiq Murad pamoja na Kamati yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali tunayapokea Maazimio yote ya Kamati yanayohusu mazingira kama yalivyoandikwa kwenye ripoti ya Kamati, ambayo yapo ukurasa wa 81 na 82 ambayo yanahusu mazingira. Ni maazimio mazuri na hatuna mabadiliko yoyote katika hayo maazimio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nizungumzie mambo mawili matatu tu yaliyojitokeza kwenye taarifa ya Kamati ambayo labda yanahitaji maelezo kidogo. La kwanza lipo kwenye ukurasa wa 57 ambapo Kamati imesema, kuwa kutegemea gesi ya LPG kama nishati mbadala ni kuwaumiza Watanzania kwa kuwa bei ya nishati hii ni kubwa na inaendelea kupanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka hili jambo likae sahihi kwenye kumbukumbu za Bunge na Wabunge kwa ujumla, kwamba ukiangalia takwimu za matumizi ya nishati hapa nchini, nishati ya LPG ni moja ya nishati ambazo bei yake inashuka kila mwaka. Mtungi wa kilo tano, kilo sita mwaka uliopita ulikuwa Sh.21,000, sasa hivi ni Sh.17,000. Mtungi wa lita 15 ulikuwa Sh.55,000, sasa hivi Sh.45,000 na tunaona trend kwamba uwekezaji na usambazaji kwenye LPG unaongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya sekta ambazo hazithaminiwi kwa ukuaji mkubwa lakini zinakuwa kwa kasi ni hii ya nishati ya LPG. Kwa hiyo, nataka tu ieleweke wazi kama sisi kama Serikali tunaunga mkono wawekezaji katika tasnia hii na tunaamini kwamba sisi na wenzetu wa Wizara ya Nishati ambao wanahusika na udhibiti tutachukua hatua za kisera kuhakikisha kwamba tunailea tasnia hii ili ikue na Watanzania wapate nishati hii ya LPG ya gesi ya mitungi kwa bei nafuu na mahali popote walipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani jambo la msingi kujua kwamba, nchi yetu bado kwa sehemu kubwa inategemea rasilimali asili kwa maendeleo yake, kwa shughuli za kilimo, shughuli za ufugaji na nyinginezo. Kwa hiyo, uhifadhi wa mazingira katika haya maeneo una nafasi kubwa zaidi ya kuisaidia nchi yetu. Napenda Bunge lichukue uongozi kama ambavyo Kamati imechukua uongozi katika kuhakikisha kwamba masuala ya mazingira yanatiliwa maanani sana katika mipango yetu ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tunaongea hapa na Naibu Waziri wangu, tunahesabu Wabunge waliochangia hii Kamati ni wangapi wamegusa masuala ya mazingira, ni Wabunge watatu tu. Tunajua kwa sababu ya umuhimu wa masuala ya viwanda na biashara, lakini nataka niseme bila hifadhi ya mazingira hakuna viwanda na biashara. Tunataka tuseme kwamba Tanzania, Waheshimiwa Wabunge, naomba tusikilizane tafadhali! Tanzania ni moja ya nchi tano zinazoongoza duniani kwa kukata misitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila siku inayoenda kwa Mungu kila dakika, kila siku, tunakata misitu kwa kiwango cha kiwanja cha mpira, kila dakika, kila siku; kila dakika inayopita hapa Tanzania, misitu inayofyekwa ni size ya kiwanja cha mpira wa miguu. Hizi takwimu zimeanza kuchukuliwa mwaka 2010. Kwa hiyo, fikiria kwa miaka tisa mfululizo kila dakika unakata size ya kiwanja cha mpira wa miguu, asilimia 61 ya nchi yetu inakaribia kuwa jangwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama kwa uchumi ya land degradation, forest degradation ni takriban shilingi bilioni 2.2 dollar kwa mwaka kwenye uchumi au asilimia ya GDP. Kwa hiyo, hatua hizi zote tunazochukua za kuisukuma mbele nchi yetu kimaendeleo, kama hatutahifadhi mazingira zitakuwa ni za bure, kabisa. Kama hatutachukua hatua madhubuti za kuhifadhi mazingira, kilimo, uvuvi, ufugaji itakuwa ni bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku hizi kuna mbinu mpya ya kupima utajiri wa nchi na utajiri wa watu, inaitwa natural per capita natural resource capital, yaani maliasili hizi za nchi nzima zinathaminiwa na kila Mtanzania anapewa kwa per capita, thamani yake. Kwa miaka 20 iliyopita utajiri wa maliasili wa kila Mtanzania umeshuka kwa asilimia 35. Kwa hiyo hizi physical asset zinaongezeka, lakini natural capital, utajiri wa maliasili wa kila Mtanzania unapungua kwa asilimia 35 katika kipindi cha miaka 20 iliyopita. Kwa hiyo, kwa sababu idadi yetu inazidi kuongezeka kwa kasi, hili jambo ni la muhimu na la kulitazama. Kwa hiyo, ningependa Bunge lako lichukue uongozi kwenye eneo hili la hifadhi ya mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo limezungumzwa hapa ni lile suala la mita 60 na athari zake kwa shughuli za watu na maelekezo ya Mheshimiwa Rais yaliyotoka ya kutazama sheria hizo ili kuweza kuruhusu watu wafanye kazi. Ni dhahiri kabisa kwamba Watanzania wengi wanategemea maeneo chepechepe, mbogamboga nyingi tunazokula mijini michicha, cabbage na nini vinazalishwa kwenye maeneo haya na maeneo haya pia yanatoa; ukienda kule kwa ndugu zangu, kule kwetu kwa Bwana Shangazi tunaita vitivo, ukienda kule kwa ndugu zangu kwa akina Mwamakamba kule unyalukolo wanaita vinyungu na kadhalika. Kwa hiyo tunaelewa kwamba kuna baadhi ya Watanzania wanategemea haya maeneo ya chepechepe kwa ajili ya maisha yao na Serikali za Mitaa zinapata kodi humo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kutokana na maelekezo ya Mheshimiwa Rais, tayari Wizara sita tutakaa na kuangalia namna gani tunaweza kuhakikisha kwamba ruhusa inatolewa huku hifadhi ya mazingira ikizingatiwa. Moja ya nyenzo tulizonazo ni Kifungu cha 57 cha Sheria ya Mazingira, kinasema kwamba:

“Kwa kuzingatia Kifungu cha (2) ndani ya mita sitini hakutafanyika shughuli yoyote ya binadamu ya kudumu au ambayo kwa asili yake inaweza kuharibu mazingira…”

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sheria imepiga marufuku shughuli ndani ya mita sitini. Kifungu hicho hicho cha 57(2) kinasema: Waziri, kwa maana ya Waziri mwenye dhamana ya mazingira, anaweza kuweka miongozo ya kuendesha shughuli za binadamu ndani ya maeneo hayo yaliyoelekezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua hilo nililolisema awali, sheria yenyewe imeweka uwezekano wa Serikali kuruhusu shughuli kufanyika kwa masharti maalum. Kwa hiyo, sisi kama Ofisi ya Makamu wa Rais na kwa mamlaka niliyopewa kama Waziri mwenye dhamana ya Mazingira, tutaweka miongozo ya kuendesha shughuli za kibinadamu katika haya maeneo; miongozi ambayo itazingatia hifadhi ya mazingira, lakini pia upatikanaji wa riziki za watu. Kwa hiyo tutaweka namna ambayo kwa mfano aina ya mazao unayoweza kulima, ukaribu na kwenye kingo, matumizi ya mbolea za kemikali, ruhusa ya kutoingiza udongo kwenye mto na kadhalika. Miongozo hii itakuwa technical na itatumika kuzuia jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hili jambo linawezekana kufanyika, hakuna contradiction hapo kwa sababu sheria yenyewe imetoa ruhusa hiyo na tutaitumia sheria hii kuhakikisha kwamba azma ya Kiongozi wetu inatimia, lakini azma vilevile ya hifadhi ya mazingira inatimia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. (Makofi)