Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018

Hon. Eng. James Fransis Mbatia

Sex

Male

Party

NCCR-Mageuzi

Constituent

Vunjo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018

MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi nami nichangie Taarifa ya Kamati mbili zilizoko mbele ya Bunge letu. Nitaanza tu kwa kukumbusha wajibu wetu sisi Wabunge. Wakati wa Taarifa za Kamati Bunge wajibu wake namba moja ni yale majukumu kwa Taifa; tunaacha tofauti zetu nyingine zote; na ndiyo wajibu wa kuisimamia Serikali vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Taarifa ya Kamati ya Miundombinu, mimi ni Mjumbe. Taarifa yetu tunazungumzia kuhusu suala la bandari. Ukiangalia bandari zetu hasa Dar es Salaam na wale wengine wote wanaosimamia, kwenye maoni yetu ya Kamati tumeeleza namna gani ilivyo bora watu wetu kupata elimu au weledi katika Mataifa mbalimbali. Sasa nilikuwa najaribu kuangalia kwetu sisi Tanzania ambao kati ya nchi 38 za Afrika ambazo wana bandari, Tanzania tupo kwenye hali gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, bandari zetu; nasisitiza, bandari zetu tukijilinganisha na bandari nyingine Afrika, Bandari za Egypt katika mambo ya Container Terminal ina uwezo wa container 2,900,000, Durban 2,600,000, Tangier Morocco 2,500,000 na Dar es Salaam 501,000. Kwenye mizigo, Bandari ya South Africa ni tani milioni 72, Mombasa tani milioni 31, Dar es Salaam tani 13,800,000 kwa mwaka. Ukiangalia kwenye region yetu hii, East Africa yote na Central Africa, Mombasa ndiyo wanaongoza. Sasa hapa ni kwa nini tunafikia kwenye hali hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijasema kwa nini tumefikia kwenye hali hii, hebu tuangalie hapa Tanzania uwezo wetu wa forex. Utalii kwa takwimu za Benki Kuu za mwezi Novemba ni bilioni 2.4, asilimia 28; dhahabu, US Dollars bilioni 1.5, asilimia 17.6; bandari, transit goods, bilioni 1.23, asilimia 14.5; mazao yote ya kilimo ni dola milioni 883 ambayo ni asilimia 10.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukiangalia bandari yetu ambalo ndilo lango kuu la uchumi, ambapo tunategemewa na Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia, DRC Congo, Malawi, hata mpaka na Sudan; uwezo wa bandari yetu huwezi ukasema unawekeza, lazima ziende sambamba. Bandari na reli lazima ziendane sambamba, upende usipende. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mkakati wa bandari na iko kwenye Taarifa ya Kamati yetu, huwezi ukaweka vinginevyo kabla hujaangalia mzigo mkubwa wa bandari unapatikana wapi? Kwa hiyo, kipaumbele cha kiuchumi lazima kabisa bila kumung’unya maneno lazima tungewekeza kwenye tawi la Tabora, Kigoma, Uvinza na Msogati. Ambapo sasa ukiunganisha na bandari yetu ya Dar es Salaam ndiyo unaweza ukasema sasa hapa uchumi wako unaenda barabara, badala ya kuanza mambo mengine labda ya kisiasa na mambo ya namna ambayo hayawezekani kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nazungumzia bandari? Sisi ukanda wetu una urefu wa kilometa za bahari 1,424 na strategically tungetumia bandari yetu tu, forex ambayo mwaka jana, kwa takwimu za BoT, dola bilioni 8.5 tungezipata zote kutoka Bandari ya Dar es Salaam. Leo hii Bandari ya Dar es Salaam kama tulivyosema hapa ni asilimia 14 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sijui tunafikiriaje? Lazima tuangalie hata washindani wetu wa Afrika, wakati sisi tunazungumzia mambo ya 20 equivalent units za mambo ya container, ukizungumzia Shanghai peke yake ni zaidi ya milioni 40 wakati sisi ni 501,000. Sasa radical change katika uchumi itakuwaje kama hatuwezi tuka-think globally na tukauza dhahabu in lacal solution? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa najaribu kuangalia bandari za Afrika. Kuanzia South Africa mpaka Na. 13, unaenda South Africa, unaenda Egypt, Nigeria, Morocco, Algeria, Congo, Kenya, Ivory Coast, mpaka Na. 13 wala huioni Tanzania tuko wapi? Sisi tuko hoi bin taaban. Kwenye mizigo kwa mwaka ni tani milioni 13.8.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kuwekeza vizuri katika Bandari ya Dar es Salaam kwenye wharfage badala ya Serikali au Waziri Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa maana ya Hazina kuchukua zaidi ya bilioni 400 wangewaachia bandari wawekeze serious kwenye bandari ili bandari zetu ziweze kuwa na nguvu za kutosha katika kutekeleza wajibu wake. Vile vile tumezungumzia bandari za nchi kavu miaka nenda rudi, miaka nenda rudi, songa, panda hivi and so forth, waende wakajifunze duniani wanafanyaje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumzia bandari nizungumzie kidogo barabara za Jiji la Dar es Salaam, barabara za Jiji la Dar es Salaam ni zaidi ya miaka kumi sasa na iko ukurasa wa 38, tumezungumzia suala la muda unaopotea barabarani, suala la mafuta, suala la msongo wa mawazo (stress) na suala la uchafuzi wa mazingira. Tulipozungumzia Dar es Salaam mpaka nakumbuka taarifa ya Chenge one na mkakati tufanye nini? Tukaja na mawazo na Serikali ikaja na MV Dar es Salaam kwa ajili ya kusafirisha watu kwa njia ya maji, naomba niiulize Serikali leo MV Dar es Salaam ipo wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ingesaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa msongamano katika Jiji la Dar es Salaam na ingesaidia kuzuia uchafuzi wa mazingira na muda wa kufanya kazi ambapo kila siku msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam unagharimu Taifa hili zaidi ya shilingi za Kitanzania bilioni nne kwa utafiti uliofanyika takribani miaka kumi iliyopita tangu mwaka 2009. Sasa Mheshimiwa Januari Makamba na mkakati wake wa mazingira na nini ile MV Dar es Salaam ipo wapi? Ili iweze kufanya kazi kwa mujibu na taratibu zinazosaidia, ni Serikali hiyo hiyo moja. (Makofi)

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila utaratibu)

MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama ipo Dar es Salaam sawa kama ipo wapi basi tuhakikishe kwa sababu gani? Usafiri ulio rahisi kuliko mwingine wowote na unarahisisha ni usafiri wa majini na utasaidia katika mikakati ya namna hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie kuhusu barabara zetu ambazo nimezungumzia za Dar es salaam lazima kuwepo na mkakati madhubuti zile by pass, flyovers kuahakikisha tunaondoa na kuwekeza kwelikweli kwa sababu pale ndiyo lango kuu la uchumi ndiyo uchumi wetu zaidi mapato yetu ndani asilimia karibu takribani 80 tunapata katika Jiji la Dar es Salaam sasa either you like or not lazima tufanye hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la hizi barabara ambazo zinasaidia katika maendeo mbalimbali huwezi katika karne hii tukaanza kuzungumzia kabla hatujaunganisha barabara za Mikoa ya Katavi - Kigoma, Katavi - Tabora, Kigoma - Kagera, Njombe - Makete na Mbeya kwa pamoja ili kuhakikisha nchi nzima miji yote mikuu imeunganishwa kwa barabara za lami na ni sera ya Serikali kuhakikisha kipaumbele kinawekwa kwenye barabara zote kwenye miji yote mikuu kuhakikisha imeunganishwa kwa lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda nizungumzie kidogo kuhusu Kamati ya Viwanda na Biashara, ule ukurasa wa 80 ambao unazungumzia mazingira ya kufanya biashara yaliyo rafiki, tukiri kwamba private sector ni engine ya uchumi wetu, lakini leo hii mazingira ya wafanyabiashara na Kamati imeandika hapa katika ukurasa wa 80 yamekuwa ni magumu kwelikweli na yamekuwa ya hofu. Sasa tutapata wapi fedha kama tunafanya wafanyabiashara ni washindani wa Serikali, badala ya Serikali kuwawezesha wafanyabiashara kujenga mazingira rafiki ya kikodi, kujenga mazingira rafiki ya uwekezaji, kujenga mazingira rafiki na wakitoa kauli watoe kauli, kwa mfano, niulize lile suala la refundable, zile fedha billion 32 kwenye viwanda vya sukari hasa viwanda vya soda, mbona hawajarudishiwa kodi yao? Naomba warudishiwe fedha hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maduka ya fedha za kigeni Mkoa wa Arusha amesema Mheshimiwa Lema hapa yapo kwenye hali mbaya na zile fedha zao mlizochukua Benki Kuu muda umetosha, warudishiwe fedha zao immediately ili wafanyabiashara hawa waweze kuendelea kufanya shughuli zao, kama wana makosa waelezwe hayo makosa na kama wameshafanya ukaguzi wao wazirudishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jiji la Arusha katika uchumi, utalii, tumekubaliana hapa forex kwenye utalii ni zaidi dollar billion 2.4 ambayo ni sawa na asilimia 28 ya fedha zote za forex ni za utalii na Jiji la Arusha ni la utalii. Sasa forex mnafunga, sasa tumlilie nani na watu wafanye nini? Sasa kama tukifanya maamuzi ya namna hii ya kupararazi forex katika Jiji la Arusha ambayo ndiyo radical change, this is very unfortunately. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niombe kwamba wakati wa Kamati za Bajeti kama zinarudia kwa sababu wa muda, sisi Wabunge jukumu letu namba moja ni kuhisimamia Serikali kwa niaba ya wananchi, kwa sababu sisi tumekuja hapa ili kuweza kusimamia kodi za wananchi, sisi tumekuja hapa kwa ajili ya wananchi ambao ni walipakodi, wajibu wetu namba moja ni kuisimamia Serikali, kuishauri Serikali, kuweka kando tofauti ya vyama vyetu vya siasa ili kuona Taifa letu linapewa kipaumbele na wajibu wa Mbunge namba moja ni kwa Taifa lake, Taifa lake, Taifa lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna ubishi leo hii huu ukurasa wa 80, unasema mazingira ya kufanya biashara yamekuwa magumu na ugumu huo kwa kiasi kikubwa unasababishwa na uwekezaji wa Sheria mbaya za kodi na kwa kuwa hali hiyo imepelekea baadhi ya wafanyabiashara kuendelea kufunga biashara zao ambao hali hii haitoi tafsira nzuri kwa ustawi wa Tanzania, lakini pia wawekezaji nchini. Sasa niiombe Serikali na niishauri kwa nia ya dhati kabisa, mkinena maneno myasimamie maneno yenu, mkisema ni mazingira rafiki, kweli yaonekane rafiki, kama ni kodi kwenye biashara kwa mfano kwenye utalii kuna kodi zaidi 50, yatakuwaje mazingira rafiki na mazingira wezeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nihitimishe kwa kusema na kuomba tena chonde chonde, tujaribu kuangalia tusiangalie humu ndani tukapongezana humu Tanzania, tujiangalie Afrika tupo kwenye position gani? Kidunia tuko kwenye position gani, elimu ya teknolojia dunia hii na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia duniani sisi tuko kwenye position gani? Tukiweza ku-think global and have a local solution, naamini tutafanya radical change kuondoa hali hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Makofi)