Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018

Hon. Kiteto Zawadi Koshuma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018

MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kutoa mchango wangu katika kujadili Taarifa ya Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, naomba kupongeza juhudi za Serikali za awamu zote kwa kuhakikisha kuwa nchi yetu inakuwa ni nchi ya uchumi wa viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya sababu iliyopelekea nchi yetu kubinafsisha viwanda ni kuleta tija. Kama nchi, tuliamini ya kwamba kubinafsisha viwanda kutaleta tija, kuongeza uzalishaji, pia kuongeza ajira, kuweka teknolojia mpya, kuongeza ubora na thamani ya bidhaa ambazo zinazalishwa katika viwanda hivyo tulivyovibinafsisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaendelea kuamini kwamba viongozi waliopita walikuwa na nia njema ya kubinafsisha viwanda vyetu. Ila nia hiyo njema iliharibiwa na baadhi ya Watendaji na Wawekezaji ambao walikuwa na dhamira ya kupotosha dhamira kubwa ya kubinafsisha viwanda ambavyo vilikuwa vimebinafsishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulibinafsisha viwanda yapata 156, lakini leo hii viwanda vinavyofanya kazi na hata taarifa ya Kamati inaonyesha ni viwanda 16 tu peke yake katika viwanda 156. Suala hili siyo suala la kulifumbia macho, lakini kwa sababu tumeshateleza, hatuna budi kuendelea kuishauri Serikali ili kuona ni kwa namna gani wanaweza wakarudisha nia ya madhumuni ambayo yalikuwa ni mema ya ubinafsishaji wa viwanda hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali katika maeneo mawili; eneo la kwanza, kuhakikisha ya kwamba inapitia mikataba yote ambayo ilihusika katika ubinafsishaji wa viwanda. Wakati zoezi zima la ubinafsishaji wa viwanda linafanyika, kulikuwa kuna mikataba ambayo ilikuwa ni ya ovyo, mikataba ambayo iliifanya Serikali kutokuwa na nguvu ya kuweza kuwanyang’anya viwanda wale ambao walivitumia vibaya na kuweza kuvirudisha kwa wale ambao sasa wana uwezo wa kuvifanya viwanda hivi kuwa na tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, naishauri Serikali, kama itampendeza Mheshimiwa Spika kuunda Kamati Maalum ya Kibunge ili waweze kufuatilia mikataba ambayo Serikali iliingia na ili kuweza kuipa Serikali nguvu ya kuweza kuvitwaa viwanda ambavyo havifanyi kazi kama vile unavyoona kwamba katika viwanda 156 ni viwanda 16 peke yake ambavyo vinafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, naishauri Serikali kuangalia namna ya kuviondoa katika orodha ya viwanda, viwanda vile ambavyo havifanyi kazi. Hii ni kwa sababu ukiangalia kwenye taarifa yetu ya Kamati; na Kamati imesisitiza kwamba vile viwanda ambavyo havifanyi kazi vizuri viondolewe basi kwenye orodha ili kuepuka mgongano wa mawazo wa kusema kwamba tuna viwanda vingi na vinafanya kazi, tukiendelea kuamini kwamba vinafanya kazi wakati havifanyi kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ili kuondoa hiyo notion ya kuwafanya Watanzania waamini kwamba tunavyo viwanda vikubwa na vingi ambavyo vinafanya kazi, ni vyema tukaondoa vile viwanda ambavyo havifanyi kazi katika orodha ya viwanda ambavyo vimebinafsishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba kuangalia katika suala zima la upelekaji wa fedha. Katika taarifa ya Kamati tumeona upelekaji wa fedha katika Wizara ya Viwanda na Biashara wamepelekewa fedha kwa asilimia 18 hadi kufikia Desemba, 2018. Katika hiyo asilimia 18, ni 6% peke yake ambayo ilikuwa imeenda kwenye miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini nia njema ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli ambayo anatangaza kila mara kwamba anataka kuona uchumi wa viwanda katika nchi yetu ya Tanzania. Ninaamini Mheshimiwa Rais anayo nia njema kabisa, lakini je, nia njema aliyonayo Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, itafikiwa vipi kama tu hata upelekaji wa fedha katika Wizara ni kwa asilimia ndogo namna hii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kuangalia kwamba kama tunataka kweli kwenda katika uchumi wa viwanda, tuhakikishe tunatenga fedha za kutosha lakini zile fedha tunazozitenga tuhakikishe zinaenda kama ilivyoidhinishwa na Bunge ili kuweza kusaidia kuleta tija katika suala hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika Wizara ya Mazingira, ninaamini kwamba ni Wizara nyeti, ina mambo mengi sana ya kuyaangalia. Kwa mfano, katika hiki kipindi cha hivi karibuni, maeneo mengi sana yanaonekana kwenda kuwa na jangwa na kuna uharibifu mkubwa sana wa mazingira, lakini Wizara hii imekuwa ikitengewa fedha ndogo; na hizo fedha kiasi kidogo ambacho kinatengwa pia kinaenda kidogo. Kwa maana hiyo, Wizara hii tunaizorotesha na kuifanya ishindwe kufanya kazi yake ya kuweza kuyatunza mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa siku ya leo baada ya kuyasema hayo, ninaomba Serikali iweze kupitia maoni ambayo yametolewa na Kamati ya Viwanda na Biashara, lakini pia niendelee kupongeza juhudi ambazo zinafanywa na Serikali ya Awamu ya Tano ili kuhakikisha kwamba tunafikia katika uchumi wa viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)