Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Munde Abdallah Tambwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii ya kuchangia. Kwanza kabisa nianze kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa ambayo anaifanya, wote tunaiona lakini nimpongeze kaka yangu Waziri Mpango, Naibu Waziri na menejimenti nzima ya Wizara ya Fedha kwa kazi kubwa wanayoifanya ya usimamizi mzuri wa bajeti ambayo waliileta hapa Bungeni. Tunaamini bajeti hiyo inasimamiwa vizuri na ndio maana mambo yote yanakwenda kwa sababu ya usimamizi na udhibiti wao mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja kwenye mjadala, nimesikia wanasema kwamba tusipokuwa makini Waziri na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha baada ya utawala huu wanaweza kufungwa. Niwaambie hafungwi mtu hapa, kwa sababu kazi zote zinaonekana zinavyofanyika. Serikali iliyopita tulikuwa hapa Bungeni walikuwa wanasema Serikali hii haidhibiti rasilimali za nchi, Serikali hii ni dhaifu, leo tumepata Serikali inayodhibiti maliasili ya nchi yao, utafikiri maliasili zile ni za kwao wao binafsi, lakini leo hii wanakuja tena kuwaambia watu hawa watafungwa kwa kushindwa kudhibiti rasilimali za nchi yetu. Niseme hiki kitu siyo kweli, tumeona Mheshimiwa Rais amepambana kwenye madini, ameleta sheria tumebadilisha, yote hiyo ni kudhibiti rasilimali za nchi yetu ili Watanzania waweze kunufaika na rasilimali hizo. Tumeona Rais amepambana kwenye rushwa kwenye uwajibikaji, kwenye nidhamu ya watumishi na mambo yanaenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii wanamwambia mtu atafungwa, unabaki unashangaa, atafungwa kwa kutoa bajeti ya afya bilioni 30 mpaka bilioni 260, atafungwa kwa kusimamia ujenzi wa reli ya kisasa kwa kutumia pesa zetu za ndani, atafungwa kwa ujenzi wa barabara, atafungwa kwa kusomesha watoto wetu elimu bure, atafungwa kwa ndege sita zilizonunuliwa kwa mpigo. Nimuombe Waziri wa Fedha na Katibu Mkuu wasikate tamaa, waendelee kuwafanyia kazi Watanzania kama wnavyowafanyia. Tumeona kabisa ndani ya miaka mitatu kazi kubwa iliyofanywa na Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeonekana. Leo kule kwetu sisi Tabora, Mkuu wetu yule wa Mkoa, watu wanaona kama vichekesho lakini anaongea ukweli, anasema Tabora imekuwa kama Toronto, sio utani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukifika saa 12 mitaa yote inawaka taa, mitaa yote ina lami, kule tulipozaliwa sisi Uswahilini kulikuwa hakuna lami toka tumezaliwa mpaka sasa ndio tumekuja kuiona lami. Nasema Serikali inafanya kazi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu hawa hawaeleweki, wasipofanya kazi wanawaita dhaifu, wakifanya kazi wanawaita madikteta, tabia zao sio za kiume wala sio za kike, hawa watu sijui ni wa aina gani, nashindwa kabisa kuwaelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Rais kwenye suala zima la korosho, tulikuja hapa Bungeni tukajadili sana kuhusu korosho, tukapata wanunuzi wanataka kununua kwa shilingi elfu mbili na kidogo. Rais wa wanyonge akakataa, akasema korosho hizo atazinunua yeye mwenyewe, lakini tunashuhudia amepatikana mnunuzi, amezinunua kwa shilingi 4,480, tunampongeza sana Rais amepambania wanyonge wake kwa vitendo. Ajabu leo unakuta mtu analaumu tu, anaona haya mambo ni mepesi, anaona haya mambo ni rahisi, huu ni uthubutu wa hali ya juu aliouonesha Rais. Rais wetu ni jasiri Rais ana maamuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napata tabu sana, hawa watu kila siku wanatuambia hawauoni utawala bora, wanaona udiktekta tu. Mimi nashindwa kuelewa hawa watu wako huru, wanaita vyombo vya habari, wanaongea na vyombo vya habari, wanafanya wanavyovitaka, wanaisema Serikali, wanamsema Rais lakini bado wanasema hakuna utawala bora. Utawala bora kwao ni maandamano tu ndiyo wataona kwamba kuna utawala bora. Yapo wanayoyasema, wanaenda Mahakamani, wanashtaki, hatua zinachukuliwa, maamuzi yanatoka, lakini bado hawaioni Serikali kama ina utawala bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile wamekuwa wakitushawishi tukubali masharti ambayo kama nchi yetu na tamaduni zetu hatuwezi kuyakubali. Mimi niendelee kuipongeza Serikali iendelee kuwa na misimamo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku zote nimekuwa nikimwambia Rais wangu kupitia Bunge hili pamoja na viongozi waendelee kufanya kazi zao kama walivyojipangia, wasiyumbishwe na mtu yeyote, wasimfuate mtu yeyote maana hawa watu wanawayumbisha kwa makusudi ili siku ya mwisho waje wawaambie kwamba wameshindwa kufanya kazi na waweze kusema. Tumeona miaka mitatu mapinduzi yaliyotekea ni makubwa, maendeleo yaliyotokea ndani ya miaka mitatu ni makubwa, mtu yeyote unayemwambia aangalie anaona, nashangaa wanapokuwa kila saa wanalaumu, kila ni watu wa kubeza…

T A A R I F A

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, namheshimu sana aliyetoa hii taarifa lakini hawezi kunilazimisha hicho kipengele chake kwa sababu yeye ni mfanyabiashara, wote tuongelee biashara hapa ndani. Mimi naongelea kupongeza Serikali yangu kwa kazi kubwa inayoifanya, ndicho nachoongelea mimi na hawezi kuni-drive anapotaka yeye. Tena namheshimu ni rafiki yangu, kutwa ananiambia anataka kurudi CCM huyu wewe muache tu. (Makofi)

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kukutana na wadau wa madini, yote hii ni juhudi kubwa za kutaka kuongeza pato la nchi yake, za kutaka kuongeza uchumi wetu ili Watanzania waendelee kunufanika na matunda yao. Mheshimiwa Rais ambaye anahitaji amani kila siku amekutana pia na Viongozi wa Dini ili kuweka amani katika nchi yetu, kusikiliza kero zao na mambo kadha wa kadha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Rais akutane na wadau wa pamba, tumbaku na kahawa. Mazao haya tunayategemea sana kwa ajili ya kuingiza fedha za kigeni kwenye nchi yetu lakini yanategemewa pia kwenye viwanda vyetu vya ndani na yanatoa ajira kwa vijana wetu na sisi wenyewe. Kwa hiyo, niombe pale Mheshimiwa atakapopata nafasi akutane na wadau wa mazao haya makuu ya nchi yetu ili kuleta tija kama alivyoleta tija kwenye madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)