Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Usimamizi wa Matumizi ya Fedha za Umma katika Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2017

Hon. Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Usimamizi wa Matumizi ya Fedha za Umma katika Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2017

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia na mimi mchana huu nikiamini kwamba kazi tunayoifanya hapa ni kazi ya kuisaidia na kuishauri Serikali na kulisaidia Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni Mjumbe ya Kamati ya PAC, pamoja na mambo mengi yaliyozungumzwa lakini pia nasikitika kuamini kwamba na sitaki kuamini kwamba watu wanatamani kusikia mabaya siku zote, lakini wakati unakumbuka kusikia mabaya lazima tukubaliane na hili wala halina ubishi na mazuri yapo na kazi hizi zinafanywa na binadamu. Kama zinafanywa na binadamu hakuna mwanadamu aliye mkamilifu katika nchi hii au dunia hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninachotaka kusema CAG kwa mara ya kwanza amefanya kazi kubwa sana na ninyi ni mashaidi wakati tunaingia hapa tulilalamika sana suala juu ya kumuwezesha CAG kufanya kazi kwenye maeneo makubwa. Kwa mara ya kwanza CAG hajakuwa na malalamiko ya kibajeti kwa mwaka wa fedha ulioisha na kazi kubwa sana aliyoifanya. Yeye mwenyewe amedhibitisha, kati ya mashirika 200 aliyotazamia kukagua amekagua mashirika 188, lakini taasisi za Serikali pamoja na taasisi zingine alipanga kukagua taasisi zaidi ya 241 na zote hizo amezikagua kadri alivyoweza na kwa nguvu zake zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye ukaguzi huu kama nilivyosema haiwezekani watu hawa wote wakawa malaika, lakini makosa ya kibinadamu yanakuwepo. Mimi niwashukuru sana Wajumbe wa Kamati na Mwenyekiti wa Kamati, mmefanya kazi kubwa na kwa utulivu mkubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mimi nijikite tu kwenye hoja kama tatu hivi; cha kwanza cha kwanza ni ration za polisi ni aibu sana na mimi nimuombe kwa sababu Mheshimiwa Kangi yupo hapa ripoti karibu zote tunazozizungumza humu ndani, Mheshimiwa Halima alisema kwamba ripoti moja tu ndiyo ilikuwa ya ukaguzi maalum, tuna ripoti takribani nne ni ukaguzi maalum kwenye taarifa tunayoisoma hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala ration za polisi Mheshimiwa Waziri yupo hapa, maana humu tunaweza tunahangaika, kila mmoja amekariri jambo moja, anataka aseme hilo hilo apotoshe afurahi aendelee mbele. Fedha zaidi ya bilioni 888 zimelipwa kwa watu wasiokuwa maaskari wakati askari wetu wanahangaika awapati ration kwa wakati Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani. Jambo hili limekuwepo muda na hakuna mtu anayechukua hatua hata mmoja. Tukuombe sasa Mheshimiwa Kangi tunataka watu hao wapatikane, wachukuliwe hatua na fedha za umma zilizotakiwa kwenda kwa wahusika zipelekwe, vinginevyo tutabaki hapa tunalaumiana tunapiga kelele alafu atuendi kwenye mambo ya msingi ambayo tunataka yawasaidie Watanzania, ni lazima tuhakikishe mambo haya yanafanyiwa kazi na yanapata ufumbuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nigusie kidogo suala la NSSF. Inawezekana kabisa watu waliokuwa wanafikiria, walifikiria vizuri, lakini wale waliokuja kutenda wametenda kinyume na mipango iliyokuwa imetengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano tumezungumza hapa na sisi tumeangalia upande mmoja tu hapa, tumeangalia upande wa ardhi ambazo zilikuwa zinanunuliwa kwa ajili ya kuhifadhi kwa matumizi ya uwekezaji. Uwekezaji ulikuwa wa aina gani? Mpango wa kuekeza ulikuwa ulikuwa upi? Feasibility study ilifanyika kwa kiwango gani? Yote haya hayakuonekana. Hapa tunazungumza ukienda Mwanza, ukienda Arusha, ukienda Dar es Salaam, ukienda sijui Pwani, kila sehemu ni matatizo matupu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano fedha iliyonuniliwa ardhi peke yake ni zaidi ya bilioni 27. Shilingi bilioni 27 inaponunua ardhi tafsiri yake ni nini, lazima tuwe na mipango madhubuti ambayo tulielekeza kule. Hizi taasisi sio kwamba hazikuwa na watu au zilikuwa hazisimamiwi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nikupe tu mfano mmoja mdogo ukichukua pale wanasema mfano ukienda Dar es Salaam wanasema wamenunua ardhi Dar es Salaam na Pwani kwa zaidi ya shilingi bilioni 14 plots tano, zinatajwa plots tano. Inaweza kuwa ya square mita 4,400, inaweza kuwa square mita 30 ama inaweza kuwa square mita 15.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninachosema hapa ni kwamba hatuwezi kuendelea kubaki tunalalamika. Mimi niishukuru sana Serikali kwa kuamua kuunganisha mifuko hii na kupata mifuko miwili. Sasa ni wajibu wa BOT na SSRA kuhakikisha mifuko hii haiingii tena kwenye mikataba ya hovyo itakayotupeleka taifa na watumishi wetu kukosa michango yao wanapohitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukifanya hivyo tutakuwa tumeisaidia Serikali tutakuwa tumelisaidia Taifa, lakini ardhi yote ambayo inaonekana ipo ipo juu ufanyike uhakiki wa kina sasa itambuliwe na Halmashauri zote zinazohusika zihakikishe hati ardhi hizi zinapatikana, vinginevyo tunapiga tu mark time tu hapa halafu hatuwezi kuisaidia nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Suala lingine ningependa nizungumzie NDC. Ni kweli NDC ni shirika la maendeleo ambalo limetengenezwa maalum kwa ajili ya kusaidia kwa haraka na kwa kazi uwekezaji kwenye sekta ya viwanda na biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa mfumo wa shirika hili lilivyo, kama tutaendelea kuliegemea, nataka nikuahakikishie hakuna hata siku moja linaweza kuwa zao bora kwenye viwanda tunavyovitegemea na haliwezi kumsaidia Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano limezungumzwa hapa TANCOAL na PCEA. TANCOAL tunafahamu ni taasisi au ni kampuni iliyoundwa kutoka Serikalini na hii inayoitwa PCEA ni mwekezaji aliyekuja, sasa cha ajabu kabisa uwezi kukifikiria TANCOAL imechukua asilimia 30 lakini hawa waliokuja kama wawekezaji wamepewa asilimia 70. Mtaji wa mwekezaji ni shilingi milioni 1.75. Moja ya makubaliano ni lazima atoe dola milioni 20 na dola milioni moja 1.47 zinunue vifaa na kuwekeza kwenye magari.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka mmoja baadae, mwaka 2012 mwekezaji kaenda kukodi vyombo na magari vyenye dhamani ya dola milioni 42.7. Tafsiri yake ni nini, mwekezaji huyu awezi kulipa kodi ya Serikali hata senti moja, hawezi kulipa mrabaha wa makubaliano ya Serikali, lakini zaidi ya yote kila mwaka kukicha kukirudi anapata hasara na hata walioingia mkataba Mheshimiwa Kiswaga hapa amesema hivi kweli tuna watu leo wanakaa kwenye ofisi hawezi kufikiria mkataba alioingia asilimia 70 na 30 anazobaki nazo kama Serikali hatujui hata dhamani ya mawe yanayokwenda kuchimba na kwa umri upi?

Mheshimiwa Naibu Spika, watu hawa wapo, wanaishi, wanakula maisha, hakuna hatua, tumekaa, bodi imeuliza maswali ya kutosha lakini imetumia muda muda mchache sana mpaka leo haijaleta hata jibu moja juu ya hii. Tuombe sana Serikali na Mheshimiwa Waziri wa Uwekezaji upo hapa, hili ndilo eneo sasa tunataka tumsaidie Mheshimiwa Rais anayefanya kazi kubwa ya kulinda rasilimali za taifa hili ya kuhakikisha tunafaidika na rasilimali zetu ya kuahakikisha tunapambana na mambo yote yaliyokuwa ya ovyo, kuisaidia Serikali irudi kwenye wakati unaofaa kwa ajili ya umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, sote tunafahamu na mimi nimesema sana, haiwezekani na haitakaiwezekani kila siku tukikaa hatuna suluhu, tunataka tufike sehemu. Leo tunasema Mheshimiwa Kangi kuna magari 777 hayaonekani na ninyi mpo. Tusaidieni haya mambo yashughulikiwe, tuondoe maswali kwa watu, tumwache Mheshimiwa Rais ashungulike na mambo ambayo yanaweza kulisaidia Taifa hili na kuweka maendeleo zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizungumza fedha zote tunazozisema hapa, pale Nyamagana ukija nahitaji Vituo vya Afya vitatu tu ninacho kimoja sasa hivi. Fedha hizi ni nyingi nahitaji barabara za lami kama kilometa 30 hivi. Fedha hizi zingeweza kusogezwa pale zikawasaidia wananchi na maeneo mengine mengi. Ndiyo, ananikumbusha kwa mfano ukiwa unatoka Nyegezi unaenda Majengo barabara ni mbaya kule, ingewezwa kutengenezwa kupitia hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nakushukuru sana na Mungu awabariki sana. (Makofi)