Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Jesca David Kishoa

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kujadili kwenye hotuba hii muhimu ya mpango wa maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapojadili mpango wa maendeleo kimsingi tunajikita kwenye mambo matatu makubwa, jambo la kwanza tunajadili ni namna gani tunakwenda kuongeza mapato; jambo la pili, tunajadili ni namna gani tunakwenda kupunguza gharama ambazo sio muhimu kwa maana ya kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, lakini jambo la tatu tunazungumza namna ya kutekeleza vipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nitakwenda kugusia upande wa ni namna gani tunaweza kuongeza mapato. Nitajikita kwenye eneo ambalo ninaamini kwa sehemu kubwa sana tunapoteza mapato; tunapoteza mapato mengi kwenye eneo la mikataba mibovu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni bahati mbaya sana na ninashindwa kuilewa commitment ya Serikali katika hili. Kwamba, ni kwa nini mnashindwa kufanya review kwenye mikataba mibovu ambayo tunapoteza mapato mengi Serikalini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 5 mwezi Mei mwaka huu alisimama AG humu ndani, kipindi cha Bunge la Bajeti akiwa anajibu hoja yangu ya mikataba mibovu, specifically kwenye Mkataba wa SONGAS. Ali-declare na akakubali kwamba, mkataba wa SONGAS ni mkataba ambao uko very complicated na Hansard ninayo hapa ya siku nzima ya tarehe 5, kwa sababu ya muda siwezi kumnukuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliahidi kwamba, mikataba mibovu ukiwepo mkataba wa SONGAS utakwenda kufanyiwa marekebisho ndani ya miezi miwili kuanzia mwezi wa tano, lakini mpaka hivi ninavyoongea leo huu ni mwezi wa 11 hakuna mrejesho wowote, hakuna chochote ambacho kumefanyika na kila mwezi kuanzia mwezi wa 05 mpaka sasahivi mwezi wa 11
tunapoteza dola milioni tano kila mwezi kutokana na mkataba huu mbovu for 14 years, kwa miaka 14 tumekuwa tukipoteza mapato kutokana na mkataba huu. Hapa ndio ambapo naweka kigugumizi ni kwa nini Serikali inashindwa kurekebisha kufanya review kwenye mikataba hii ambayo inaingiza hasara kubwa kwenye Taifa letu? Nataka wakati tunahitimisha Mheshimiwa AG aje atupe mrejesho wa wamefikia wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo ukienda ukiangalia international standards za contracts kuna kipengele kwenye mikataba ambayo, especially mikataba ya umeme, kuna kipengele kinaitwa despute resolution. Hiki ni kipengele ambacho kama kuna conflict of interest kwenye pande mbili kwenye mkataba basi, wanapata fursa kupitia kipengele hiki kwenda kufungua account ambayo inaitwa ni Escrow Account, wanaweka fedha kule mpaka mgogoro utakapokwisha. Kwa nini kwenye suala la SONGAS kunakuwa kuna kigugumizi cha kuchukua mapato yanayopatikana kupeleka kwenye account ya Escrow mpaka pale tutakapojua mbivu na mbichi ni zipi? That is question number one.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ni kwa nini kwenye Mkataba wa SONGAS Serikali mnashindwa kuchukua kesi na kuipeleka arbitration? Who is behind this kiasi kwamba, mnashindwa? Mbona kesi ngapi mnazipeleka arbitration kwa nini kesi ya SONGAS ambayo taarifa mmepoteza pesa nyingi kuliko hata kwenye kipindi cha IPTL?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni hii tunaingia hasara kubwa sana kama Serikali, sijajua ni kwa nini tunasuasua katika kuchukua hatua? Ninashindwa kuelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo kama Taifa tunapoteza mapato, hapa naomba niwazungumzie TEITI na nichukue fursa hii kuwapongeza sana TEITI (Tanzania Extractive Industry Transparency Initiatives). TEITI wote tunajua ni muunganiko wa makundi matatu, kundi la kwanza ni asasi za kiraia wako watano, kundi la pili ni makampuni wawakilishi kutoka kwenye makampuni ambao wako watano, makampuni ya sekta ya uziduaji, na kundi la tatu ni wawakilishi kutoka Serikalini jumla wako 15 ni makundi muhimu sana. TEITI wametoa ripoti mwezi wa nne mwaka huu ambayo inaonesha kwamba Serikali ya Tanzania inakiri kupokea shilingi bilioni 435 kutoka kwenye makampuni yanayo-deal kwenye sekta ya uziduaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo huo makampuni husika, kwa maana ya makampuni yanayo--deal kwenye oil, gas and mining, yanakiri kwamba yenyewe yamepeleka Serikalini bilioni 465. Sasa na TEITI wanasema kwamba huu utafiti walioufanya uli-deal na makampuni 50 kati ya makampuni 1,287. Unaweza ukajiuliza kama kwenye makampuni 55 peke yake ya sekta hii ya uziduaji wamegundua kuna upotevu wa fedha shilingi bilioni 30 what if wangefanya upekuzi kwenye makampuni 1,287 tungekuwa tumepata hasara kiasi gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, well and good Mheshimiwa Waziri aliā€¦

T A A R I F A . . .

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa sababu amezidi kuishindilia hoja yangu na kuthibitisha kwamba kuna sintofahamu ya shilingi bilioni 30. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amesema kwamba wamepeleka taarifa ili CAG aweze kukagua haya makampuni. Swali dogo sana, wote tunajua kwamba, sheria haimruhusu CAG kufanya ukaguzi kwenye makampuni ambayo Serikali inamiliki less than 50% ya shares kwenye makampuni hayo. Sasa anatuthibitishia kwa kiwango gani kwamba CAG atapata mamlaka ya kwenda kufanya upembuzi na ukaguzi ambao ni wa uhakika na wakati bado hana authority ya kufanya hivyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hii niiseme tu, kipindi kijacho tutunge sheria ambayo itampa uwezo CAG aweze kwenda kupenya mpaka kwenye makampuni ambayo Serikali inamiliki less than 50% ili kuweza kuondoa mapato yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tukishindwa kudhibiti mapato yetu yanavyoendelea kupotea hatuwezi kufanya maendeleo yoyote, miradi yoyote haiwezi kufanyika. Natambua zipo njia nyingi ambazo zinatumiwa na makampuni mbalimbali kukwepa kodi na kupoteza mapato yetu. Na moja ya njia hizo, yapo makampuni ambayo yanatumia njia ya transfer pricing, yapo makampuni ambayo yanatumia njia ya thin capitalisation na yapo makampuni ambayo yanatumia njia ya production cost na eneo hili ndio sisi kama Taifa tunapoteza sana.

Kwa hiyo, nilikuwa ninaiomba Serikali kwa unyeyekevu mkubwa sana wala sina nia ya kumkomoa mtu yeyote hapa, ninachojaribu kukifanya ni kutaka kama Bunge, kama Serikali, kama nchi, tuhakikishe tunalinda mapato yetu na hatupotezi mapato yetu kwa namna yoyote ile. Kwa sababu siku ya mwisho wanaokwenda kuumia ni sisi wenyewe. Tunakaa hapa, tunakaa Bungeni tunakula fedha za wananchi kwa njia ya posho tunajadiliana mambo ambayo utekelezaji wake ni mdogo sana kwa sababu kubwa usimamizi wa mapato bado ni mdogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili ni jambo la msingi ambalo nashauri sana na wala nisitafsiriwe tofauti, ni kwa nia ya kutaka kujenga.