Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Stephen Hillary Ngonyani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Korogwe Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nami naomba kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa fursa hii ya kutoa maoni yangu mbele ya Bunge lako Tukufu na kwa sababu muda ni mdogo naomba niende moja kwa moja kwenye mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango, kwa kitu hiki kizuri alichotuletea cha mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2019/2020. Ndugu zangu, mkiusoma vizuri mpango wa mwaka jana na mwaka juzi na huu, mpango huu uko tofauti kabisa. Mpango huu umekuwa rahisi kuuelewa, umetumia lugha ambayo hata sisi watu ambao siyo wa uchumi tumeweza kuelewa kwa undani sana. Nampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa kazi nzuri hiyo aliyoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe tu katika eneo la ujenzi wa barabara akifananisha na mpango wa mwaka jana alikuwa umeorodhesha baadhi ya barabara na kwa kweli ukiangalia hata katika utekelezaji wenzetu wa ujenzi walikuwa wanafuata kile kilichoandikwa katika mpango. Kwa hiyo, naomba mpango huu utakapokamilika nimwombe Mheshimiwa Waziri aoneshe vilevile na orodha ya barabara zitakazohusika ili zitoe mwongozo kwa Wizara husika ili kwa mfano kubwa zaidi barabara ambazo bado hazijakamilika hadi sasa tungeomba sana zikamilishwe, zitengewe bajeti iingie katika mpango ili kukamilishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hizo ni pamoja na Barabara ya Likuyufusi hadi Mkenda ambayo inaunganisha Tanzania na Msumbiji kupitia Jimbo la Peramiho. Vilevile barabara nyingine ni barabara ya Lumecha – Kitanda – Londo – Kilosa kwa Mpepo – Lupilo – Ifakara hadi Mikumi. Barabara hii iko sehemu kama robo hivi imetekelezwa hadi sasa na niombe sana tuendelee kutenga fedha ili barabara hii ikamilike, hasa kipande kile kinachoanza Lupilo – Kilosa kwa Mpepo hado Lumecha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingine ambayo inatuunganisha sisi na Wilaya ya Mavago ya Msumbiji ambayo inaanzia Mtwara Pachani – Ligera – Lusewa – Magazini – Lingusenguse hadi Nalasi. Nimwombe sana Mheshimiwa Dkt. Mpango barabara hii aliitengea fedha mwaka jana kwa ajili ya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri hizi barabara zote ziingie katika Mpango ili Wizara inayohusika iweze kuingiza barabara hizo katika utekelezaji wake.

T A A R I F A . . .

MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa sababu haelewi kwamba nilikuwa natoa hiyo kama mifano na tunaongelea barabara za Tanzania nzima. Katika barabara ndani ya mpango nimesema barabara zile ambazo zinatakiwa ziendelee zisiondolewe katika mipango yetu ya mwaka huu. Kwa hiyo, siongelei barabara moja hii nilikuwa natoa mfano tu, nadhani hatuelewani kwa sababu tuko katika levels tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika upande wa ujenzi wa reli niipongeze sana Serikali kwa kuendelea na ujenzi wa reli ya kisasa ya kutoka Dar es Salaam – Morogoro hadi Mwanza na sasa tupo – kwa maana ya kupatikana kwa wakandarasi mpaka Dodoma. Naomba sana kazi hiyo iendelee kufanyika ili mtandao wote wa reli wa kuanzia Dar es Salaam hadi Mwanza; Isaka hadi Rusumo; Tabora hadi Kigoma; Uvinza hadi Msongati na Kaliua hadi Karema zote zikamilike ziingie katika mpango. Vilevile reli ya kutoka Tanga hadi Musoma na reli ya kutoka Mtwara kupitia Tunduru – Namtumbo hadi Mbambabay nayo iingie katika mpango ili tuhakikishe kwamba kazi kubwa hii ambayo Mheshimiwa Rais ameianza ikamilike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli kutoka kwenye sakafu ya moyo wangu napenda sana Serikali hii ya Awamu ya Tano isiondoke kabisa kabla kazi hii ya kukamilisha mtandao huu wa reli haijakamilika. Kwa hiyo, naomba sana hata kama itachukua miaka 30 ni vyema tu tukakubali kwa sababu tunafahamu kitu kinachofanyika ni kwa manufaa ya Watanzania wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuongelea masuala ya kilimo, hususani mazao makuu. Tukiangalia katika mazao makuu yanayotajwa, mengi sana yamewekwa kwenye mpango lakini kuna mazao kama mawili hayakuwekwa ndani ya mpango, yanatajwa kama mazao ambayo ndiyo tunapata hela za kigeni kwa wingi ikiwa ni pamoja na tumbaku, lakini kwenye mpango zaidi ya kutaja kwamba kama ni chanzo chetu cha fedha lakini hakuna kitu chochote ambacho tunakielezea au tunafanya nini kuliendeleza zao hili la tumbaku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri katika kazi zinazotakiwa kufanyika katika zao hili la tumbaku ni kitu ambacho hata fedha hazihitajiki. Kinachotakiwa, moja ni kufungua masoko tu na soko kubwa ni soko la Misri ambapo ndiyo mlango wa kuingilia nchi za Ghuba na nchi zote za Kiarabu. Ningeomba sana wenzetu wa Foreign Affairs, Wizara inayohusika na masuala ya biashara pamoja na Wizara ya Fedha ikishirikiana na Wizara ya Kilimo zitufungulie soko hili la Egypt ili hata sisi tunaopata fursa ya kulima tumbaku pamoja na wenzetu wa upande wa magharibi na kaskazini tuweze kupata kiasi kikubwa zaidi cha mgao wa tumbaku hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kwa sasa nikitoa mfano tu; katika Wilaya ya Namtumbo kwa mfano uwezo wa kulima ni zaidi ya tani 4000 lakini sasa hivi tunaazimia kulipa chini ya tani 1000 kwa sababu ya ukosefu wa soko na hiyo ni kwa sababu hatujaingia katika soko kubwa la nchi za kiarabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba sana, nimeongea mara nyingi na Mawaziri husika, watusaidie tuingize katika mipango yetu ili tunaposema mazao haya matano na sasa ni mazao sita, yanayotuletea kipato kikubwa cha fedha za kigeni tutekeleze vile vikwazo vidogovidogo vinavyozuia mazao haya yasituingizie fedha za kutosha zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa maji nimefurahi sana mpango umeelezea vizuri kwamba sasa tunakwenda kushughulikia vile vikwazo vinavyozuia upatikanaji wa maji usitimilike kwa haraka. Kikwazo kimoja kikubwa ni uhakika wa upatikanaji wa fedha. Naamini Mheshimiwa Dkt. Mpango safari hii katika mpango huu ambao tunakamilisha sasa hivi ametuletea mapendekezo, aje na mapendekezo au Serikali ikubali kutenga ile Sh.50/= ya nyongeza ili hatimaye iwe Sh.100/= iingie katika Mfuko wa Maji ili tuhakikishe…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Hongera sana kwa kazi kubwa wanayoifanya.