Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Eng. Gerson Hosea Lwenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. ENG. GERSON H. LWENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia machache kwenye mwongozo wa mpango wa mwaka 2019/2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimwia Waziri, Naibu Waziri pamoja na wataalam kwa kutuletea mapendekezo ya mpango. Tunapata nafasi ya kuchangia kwa sababu kuna kitu kilicholetwa. Kwa hiyo, nawapongeza, mmeleta maeneo mengi ambayo manafikiria kwamba tukiyatekeleza haya yatakwenda kujibu haja ya wakulima na wafanyabiashara wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango mzuri ni ule ambao hautaleta manung’uniko kwa wananchi. Tunasema kwamba uchumi unakua na pia wananchi wetu wameweza kuzalisha chakula cha kutosha ndiyo maana nchi inakuwa na amani, kama kuna njaa nchi haiwezi kuwa na amani. Pamoja na kuwa na hali hiyo ni vizuri tuangalie hawa wakulima ambao wametufikisha katika hali ya kuwa na utulivu, maana wanalima, hasa wakulima wa mahindi, wamelima miaka miwili mfululizo lakini hakuna anayewasemea wapi watauza mahindi yale na ndio maana kuna hii ziada. Kwa hiyo, mpango huu tunaoutengeneza ni lazima uende kujibu kwamba sasa mazao yao yatanunuliwa kama tunavyozungumzia mazao mengine ya biashara, hilo lilikuwa la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mapendekezo ambayo nafikiria ni kwamba ili mpango huu uweze kutekelezwa ni lazima tuone ni namna gani tutaongeza ukusanyaji wa mapato. Katika mapendekezo yaliyoletwa ni kwamba mwakani tunatarajia tukusanye shilingi bilioni 23, kwa maana ya TRA pamoja na Halmashauri zetu, sasa hii mradi ambayo tumeshaweka mikataba ni lazima tuhakikishe kwamba mikataba ambayo imeshasainiwa tunaitafutia fedha zake tuweze kutekeleza. Sehemu kubwa ya fedha hizi, kama alivyosema, zinatokana na mapato ya ndani. Kama hatuna mikakati mizuri ya kupata fedha hizi tutakuwa tunaingia mikataba halafu tunashindwa kulipa mkandarasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi mingi tumeingia mkataba kwa mfano miradi ya umeme kupeleka vijiji 555, ni jambo zuri lakini haiendi kwa kasi kwa sababu wakandarasi wale hawalipwi ama hawalipwi kwa wakati. Tumeingia miradi mingi kwenye upande wa maji wakandarasi wengi kwenye miradi mingi hawalipwi certificate zao. Kama tunakuwa na mpango mzuri lakini hatuwezi kuwa tunawalipa wakandarasi mwisho wake inakuwa kwamba hatujibu haja ya wale wananchi kwamba wanapata maji na huduma nyingine ambazo zinatarajiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nafikiri kwamba katika miradi ya kipaumbele ambayo ameielezea kwenye ukurasa wa 34, iko kama 14 lakini nafikiri tuibadilishe. Mawazo yaliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge ni mengi, tuwe na namna ya kuweza kubadilisha vipaumbele vilivyowekwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nafikiri kipaumbele cha kwanza ambacho wananchi wetu wanategemea sana ni ile miradi ambayo tuliwahamasisha wananchi wachangie nguvu zao kujenga zahanati, madarasa na maabara, ni miaka saba Serikali haijapeleka fedha. Nadhani hiki ndiyo kiwe kipaumbele cha kwanza ili wananchi hawa waone kweli tunatengeneza mpango ambao wananchi wanaukubali pamoja na kulipa madai ya kazi ambazo zimeshafanyika hasa za wakandarasi na yale madeni ya ndani, hiki kingekuwa kipaumbele cha kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipaumbele cha pili, katika miradi ile 14 nafikiri mradi wa kwanza ungekuwa wa kujenga Liganga na Mchuchuma, kingekuwa ndiyo kipaumbele chetu katika fedha tutakazokuwa tumezipata. Tumeuzungumza mradi zaidi ya miaka mitano lakini hatuoni hatua zinazoelezeka kwa wananchi kwamba Serikali inafanya nini. Tunazungumza miaka yote, hivi kuna tatizo gani mradi wa Liganga na Mchuchuma hauwezi kutekelezwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema tunataka Tanzania ya Viwanda, hatuwezi kuwa na viwanda bila kuwa na chuma chetu. Kwa hiyo, nafikiri mradi huu uchukue nafasi ya kwanza katika ile miradi mingine ya kielelezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, miradi ile ambayo tayari Serikali imeshaweka mkataba, tunaipongeza sana Serikali kwa ujenzi wa Reli ya Kati kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma tayari mikataba imesainiwa, fedha zake zile lazima tuzitenge. Isifike mahali wale wakandarasi wanasimama kwa sababu hawalipwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu Mradi wa Stigler’s Gorge, mkataba umeshawekwa fedha yake iwepo katika mpango huu. Pia na miradi ya REA nayo ni muhimu fedha zake ziwepo tuwe na uhakika. Ile mikataba ambayo imeshasainiwa fedha ziwepo. Viwanda vinavyohusiana na kilimo vipewe kipaumbele cha kwanza kwa sababu hizo ndizo shughuli ambazo wananchi wengi wanajihusisha na kutakuwa na mzunguko wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeamua Dodoma kuwa Makao Makuu, sasa Dodoma iwekewe kipaumbele katika miradi ya kuondoa msongamano. Imetajwa Dar es Salaam na Mwanza lakini tuanze na Dodoma maana tusipotengeneza sasa hizo Flyover na barabara za mchepuko tutakuja kuwa na tatizo hapo baadaye. Kwa hiyo, nilifikiri hilo jambo liwekwe kwenye vipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu namna ya kupata fedha, ndiyo TRA inajitahidi lakini peke yake haitaweza kukusanya mapato tunayohitaji kuweza kutekeleza miradi hii. Kodi za nyumba (property tax) mmeamua TRA wakusanye lakini kwa ukiritimba wao hawataweza kukusanya kodi hii. Nafikiri Halmashauri zetu za Wilaya zikusanye hii property tax. Mheshimiwa Rais, alisema kila nyumba Sh.10,000, ni kitu rahisi kwa wale wa Tawala za Mikoa kukusanya fedha hizi kuliko TRA. TRA wanakwenda kufanya valuations kiasi kwamba mtu hawezi kulipa kodi zile. Kama alivyosema Mheshimiwa Rais nyumba za kawaida shilingi 10,000 na ghorofa shilingi 50,000, tukikusanya fedha hizi tuna mahali pa kuanzia. Kwa hiyo, nafikiri kwamba Halmashauri wakusanye kwa niaba ya TRA ili tuweze kuongeza mapato na kuweza kutekeleza mipango hii tuliyojiwekea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Mheshimiwa Dkt. Mpango, pamoja na kwamba umeleta mpango mzuri lakini mawazo ya Waheshimiwa Wabunge uyaweke na utakapoleta majumuisho tuone ni jambo lipi ulilolipokea. Maana haya yanayoongelewa miaka yote huwa yanaongelewa lakini tujue ni lipi umelipokea na tuone maboresho ya mpango huu ili uweze kutekelezwa na kukidhi haja ya Watanzania wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi, ahsante sana.