Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wizara hii ya Sheria na Katiba ninayo machache sana. La kwanza imenipa faraja sana hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuonesha kwamba fedha za ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Sikonge zipo na akataja na kiwango kabisa. Mimi namuomba Mheshimiwa Waziri asimamie kwa sababu fedha hizo ni za mwaka huu wa fedha wa2015/2016 ili zifike haraka, ili kusudi hiyo Mahakama ianze kujengwa haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi binafsi nimejitolea kuruhusu ofisi ya zamani ya Mbunge iwe wazi kwa ajili ya matumizi ya Mahakama ya Wilaya ya dharura. Niliiachia hiyo ofisi tangu mwezi wa 11 mwaka jana, lakini mpaka sasa hivi Hakimu wa Wilaya hajahamia! Wakati anafanya majumuisho Mheshimiwa Waziri naomba aniambie kwamba Hakimu wa Wilaya atahamia lini? Labda wiki hii au wiki ijayo? Ili kusudi wananchi wasiendelee kutaabika! Wanatumia fedha nyingi kwenda Tabora kwa ajili ya kuhudhuria kesi zao au kesi za ndugu zao na hakuna sababu kwa nini waendelee kupata shida namna hiyo wakati ambapo Mbunge wao nimejitolea ofisi iliyokuwa ya zamani ya Mbunge, itumike kwa ajili ya Hakimu wa Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile hata polisi wanatumia pesa nyingi sana, gharama kubwa kwenda kupeleka watuhumiwa Tabora wakati ambapo nimeachia ofisi! Ninaomba sana Wizara hii iweke msisitizo wa dharura kabisa ili Mahakama ya Wilaya ya Sikonge ianze kwa dharura hata wiki ijayo, wasisubiri mpaka majengo yakamilike! Najua majengo yatachukua muda mrefu, inawezekana wakianza ujenzi mwezi huu au mwezi ujao wanaweza wakachukua miaka miwili kukamilisha majengo, miaka miwili nadhani haitavumilika kuendelea kusubiri wakati maeneo ya kuanzia kwa dharura yapo, hilo lilikuwa jambo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili napenda kuzungumzia maeneo ambayo sheria zinakinzana. Ninajua sekta zinahusika lakini mratibu mkubwa wa sheria katika nchi yetu ni Wizara hii. Ninaomba sana ichukue uongozi wa kusoma sheria zote, ili kusudi maeneo yote ambayo yanakinzana, unakuta sheria hii inakinzana na sheria nyingine, zifanyiwe harmonization mapema iwezekanavyo ili kuondoa utata wa aina yoyote ambao unaweza ukajitokeza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda kuchangia ni masuala yanayohusiana na Sheria ya Ununuzi. Tuliahidiwa kwamba sheria ile itakuja ili kusudi tuifanyie marekebisho lakini bado mpaka sasa hivi naona haijaletwa! Sikuona vizuri kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri jambo hilo limeripotiwa! Kwa sababu sheria hiyo ni ya msingi sana na imekuwa ni sehemu kubwa ya malalamiko kwa watekelezaji wengi kuhusu kuchelewesha kazi na mambo mengine ninaomba sasa Wizara hii ichukue hatua za makusudi ili kusudi sheria hiyo ifanyiwe marekebisho haraka iwezekanavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna baadhi ya mambo ambayo kwenye sheria ile hayapo, kwa mfano, masuala yanayohusu miradi mikubwa ya miundombinu, turnkey projects. Kwa mfano, ujenzi wa Reli ya Kati, ujenzi wa barabara kuu kama kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma! Hizo ni turnkey projects ambazo unaweza ukakaribisha sekta binafsi zikaingia kwenye investiment.
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya masuala yanayohusu turnkey projects hayamo kwenye hii sheria na yamekuwa yakisababisha utata mkubwa wakati mwingine Wizara zimekuwa zinaambiwa hazijafuata taratibu za manunuzi, lakini unakuta ule utaratibu haujaelezwa vizuri kwenye hiyo sheria
Mheshimiwa Naibu Spika, Kimataifa baadhi ya taratibu za turnkey projects zinapingana na Sheria ya Ununuzi ya kwetu hapa Tanzania! Nilikuwa naomba mambo kama hayo yafanyiwe haraka utaratibu ili kusudi tusiachwe kama kisiwa Tanzania twende pamoja na nchi za wenzetu ambazo zimeingiza taratibu za turnkey projects kwenye sheria zao za manunuzi ili tuweze kufaidika na uwekezaji mkubwa wa sekta binafsi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ambalo napenda kulizungumzia kwenye sekta hii ya sheria ni idadi ya watumishi katika Idara ya Mahakama. Maeneo mengi sana hata Mahakimu tu wa Mahakama za Mwanzo ni shida! Kule kwetu Sikonge tumejitolea Kata tano zianzishwe Mahakama za Mwanzo, lakini wanatuambia sijui kama watapatikana Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo!
Mheshimiwa Naibu Spika, nashangaa tuna Tume ya Utumishi wa Mahakama na amepewa kazi bwana mkubwa mmoja ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa TAMISEMI, yuko pale! Nilikuwa ninadhani labda hawana fedha, lakini sijaona humu kama fedha imeombwa kwa ajili ya watumishi! Naomba sana Serikali ichukue hatua za maksudi kuhakikisha kwamba Watumishi katika Idara ya Mahakama wanapatikana na wanakuwa wa kutosha. Hiyo ni pamoja na Majaji, pamoja na Mahakimu wa Mahakama za Wilaya, Wasajili, ile schedule yote ya utumishi katika Mahakama ikamilike ipasavyo ili kusudi kama kesi kusikilizwa zichukue muda mfupi, kusiwe na muda mrefu wananchi wanasumbuliwa kusubiri kesi zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni hayo tu na mimi naunga mkono, ahsante sana.