Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Prof. Jumanne Abdallah Maghembe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi nichangie katika mdahalo huu wa mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo na Mwongozo wa Bajeti kwa ajili ya mwaka wa fedha unaokuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niipongeze kwanza Serikali kwa kutuletea mpango mzuri, na ningependa sana niweke msisitizo hapa na kuweza kumu-encourage Dkt. Mpango kwa kazi nzuri anayoifanya kule Wizara ya Fedha. (Makofi)

Mimi nitachangia kitu kimoja tu katika sekta moja ya elimu, na nitachangia juu ya kuboresha utaratibu wa kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Ndugu zangu wote mnajua kwamba tunatoa karibu shilingi bilioni 500 kila mwaka, lakini kwenye vyuo vikuu bado wanabaki wanafunzi wengi hawapewi mikopo, wanafunzi wanalalamika, vijana wanalalamika, wazazi wanalalamika na watu wale ambao wanalea watoto na kuwapitisha katika elimu wanalalamika sana.

Sasa kwa mtaji huu wa shilingi bilioni 500 tukiweka marekebisho kidogo tunaweza kuwapa mikopo wanafunzi wote ambao wanapata elimu ya juu na hapa ndio ninapotaka kutoa mapendekezo.

Pendekezo la kwanza, ni kwamba badala ya mikopo kutolewa na Serikali, Serikali ishirikiane na sekta binafsi ili kuhakikisha kwamba sekta binafsi ndio inatoa mikopo, kwa hiyo mikopo itoke kwenye benki za biashara.

Pili, mikopo itolewe kwa wanafunzi wote ambao wamejiunga na wana sifa za kupata elimu ya juu. Na mikopo hiyo itolewe bila riba kwa watoto wanaokopeshwa na kwa sababu watoto watakopeshwa wote, kiasi cha mikopo kitapanda kitafika mpaka shilingi bilioni 800/bilioni 900 hata trilioni moja. Lakini kwa sababu inatoka kwenye sekta binafsi haiwezi kuwa na pressure kubwa katika bajeti ya Taifa.

Kwa hiyo katika utaratibu huu Serikali itakuwa na wajibu wa kuzilipa benki riba ya mikopo hiyo. Kwa hiyo, kwa estimates ambazo nimeweka hapa kwenye karatasi hapa juu ya bahasha, kama mikopo inakuwa bilioni 500 kama ambayo inatolewa sasa benki ziki-charge riba ya asilimia 10 Serikali italipa shilingi bilioni 50 kila mwaka. Lakini kama benki zita- charge asilimia 20 basi Serikali italipa shilingi bilioni 100 na hii ni badala ya kulipa mikopo shilingi bilioni 500. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, benki zinatoa mkopo kwa wanafunzi ambao watalipa principal wakati wameshapata degree zao, Serikali itakuwa inalipa riba ya mikopo hiyo mpaka mwanafunzi amalize na mwanafunzi anatakiwa apewe time frame ya kulipa na kumaliza na time frame ipo katika mikopo ambayo inatolewa sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napendekeza kwenye kipindi cha sasa mpaka kwenye bajeti itakapotangazwa hapa mwaka kesho Serikali ije na mpango ambao itashirikiana na benki kuhakikisha kwamba watoto wote ambao wanakwenda chuo kikuu kila mmoja anapata mkopo na kila mmoja analipiwa riba na Serikali, watoto watafurahi, wazazi watafurahi, wapiga kura watafurahi na Serikali itapunguziwa kiasi ambacho inatoa na kulipa kama mchango wake kwa mikopo kwa wanafunzi wanaokwenda chuo kikuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ningependa niliseme sasa kwa sababu nina muda kidogo katika kuboresha elimu ya sekondari nchini kwetu maja ya matatizo tuliyonayo shule hazina maabara kwa miaka sita mpaka saba sasa Serikali inawahimiza wananchi wajenge maabara katika shule zile za kata, kwenye Wilaya yangu mimi nina shule 25 na ni shule mbili tu ambazo zimeweza kujenga maabara tatu zinazotakiwa, sasa mwaka huu. Serikali ije na bajeti ya kusaidia wazazi wanaojenga maabara za shule za sekondari hili shule zote ziweze kuwa na maabara kwa sababu tumenunua vifaa, lakini vifaa vyote vimewekwa stoo kwa sababu hakuna hakuna maabara kwenye shule zetu za sekondari na haiwezekani tuwe na wana sayansi ambao wanafundishwa bila maabara, hakuna wanasayansi wanaopatikana bila kupatikana maabara ya kufundishia msingi wa sayansi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, mwaka huu wala tusipeleke huko mbele na hizo pesa ambazo tunaweza ku- save kutokana na kupungua kwa mikopo inayotolewa na serikali tunaweza kuzitumia kujenga maabara zote zikakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho katika Mkoa wa Kilimanjaro na hasa Wilaya za Mwanga na Same kwa miaka
15 hatujapata walimu hata siku moja, walimu wanagawanywa lakini mikoa ile haipati sababu mwanzoni walikuwa wanasema wana walimu wengi kupita maeneo mengine ya Tanzania.

Kwa hiyo, walimu wanastaafu wanaondoka, wanafariki wanazikwa, wanahamishwa wanakwenda mikoa mingine lakini nafasi zao hazijazwi. Kwa miaka 15 katika Wilaya ya Mwanga tunahitaji walimu 1,005. Sasa hivi tuna walimu 601 na upungufu mkubwa kabisa wa walimu 384 sasa kwenye shule zetu za msingi kuwa na walimu wawili, watatu, wanne, ndiyo maximum, watoto wanakaa shule hawafundishwi, nafasi za walimu zipo na nafasi hizo zina mishahara yake maana wale watu waliostaafu wameacha nafasi zile zina mshahara, mtu aliyefariki ameacha nafasi ile ina mshahara, mtu aliyehama amehama amechukua nafasi nyingine Wilaya nyingine pale Mwanga nafasi yake ipo. Nimeiomba Serikali kwenye bajeti iliyopita, nimewapelekea Mawaziri wahusika barua kwa ajili ya kuwakumbusha nataka nikumbushe tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanafunzi wa elimu ya msingi wa Wilaya ya Mwanga hawana walimu hata kidogo tunaiomba Serikali kwenye mpango huu Serikali ituletee walimu 384 ili watoto waendele kufundishwa, na kufurahia elimu ya bure iliyoazishwa na Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii nina unga mkono hoja iliyopo mezani kwetu.