Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Saul Henry Amon

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rungwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. SAUL H. AMON: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi adimu ndani ya Bunge hili kuchangia. Kwanza kabla ya yote, naunga mkono hoja nisije nikasahau. Pili, naomba ku-declare interest kwenye uchangiaji wangu kwa sababu nitachangia kuhusu biashara nami ni mfanyabiashara, kwa hiyo na-declare interest mapema kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza, nataka kutoa pongezi kwa Serikali yangu ya Tanzania hasa kwa Mheshimiwa Rais kwa ununuzi wa ndege. Pamoja na kwamba kuna watu wanaopinga, lakini nawashangaa kweli kweli kwamba nchi inaweza kuwa bila ndege! Hata nchi ndogo zina ndege, sisi tusiwe na ndege; kwa kweli nampongeza sana na hili wanipelekee hiyo taarifa kwamba nampongeza kutoka ndani ya moyo wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, kuna wenzangu wamechangia kuhusu property tax. Nataka nimkumbushe tu Mheshimwa Waziri wa Fedha kwamba wakumbuke hili alilochangia mchangiaji mwingine simtaji jina, lakini Mheshimiwa Rais alilizungumza, akawaambia nyie wakusanya kodi mnafanya kodi zisikusanywe kwa sababu mnaweka kodi zisizobebeka. Hili amezungumza mchangiaji mwenzangu amesema kwa sisi viongozi; kiongozi akizungumza yanakuwa ni maamuzi sahihi na kama lina matatizo au ukakasi, namwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, basi lije hapa lizungumzwe ili hizo kodi za property tax ziweze kupunguzwa.

Mheshimiwa Spika, nakumbuka aliongea Mheshimiwa Rais, sio mtu mwingine; akaongea bei mpaka akaongea akaweka mfano, nyumba ya ghorofa changisheni Sh.100,000/= sijui Sh.50,000/= lakini wanawaambia watu kodi ambazo haziwezi kubebeka. Ndiyo kweli aliyokuwa anazungumza mchangiaji mwingine aliyepita, wanaleta makadirio ya ajabu. Anakwambia ulipie kodi shilingi milioni 30 wakati hilo jengo wewe hupati hata shilingi milioni 30 kwa mwaka. Wanawatwisha watu mizigo ambayo haiwezi kubebeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, aliyeongea ni Mheshimiwa Rais na watu wote walisikia. Tunachotakiwa ni kumuunga mkono Mheshimiwa Rais na naamini kwamba kodi hii ikiwa ni ya kiasi ya watu kutaka kwenda kulipa wenyewe italipika, lakini kwa haya mamilioni yanayotajwa kwa kweli sidhani kama watu wengi, kama alivyozungumza mchangiaji mwingine, mzee kastaafu, unamwambia akalipie Sh.200,000/=, ndivyo walivyoenda kukagua na kutoa tathmini ya hiyo nyumba yake. Kwa kweli ni ghali sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, kuna haya matatizo na vikwazo katika biashara tunazozifanya na ndiyo maana nime- declare interest. Kuna hizi taasisi za umma zinaingiliana mno na zinaenda zote kwa pamoja; lakini nitazungumza mojawapo ambayo ni hii ya uingizaji wa mizigo. Unakuta, TFDA, kwa mfano, tunaweza kuiondoa TRA. Sasa hivi katika watu wanaofanya kazi nzuri kupita maelezo, ni TRA lakini vikwazo vinavyowekwa na hizo Idara nyingine za Serikali ndizo zinazofanya uchangiaji wa uchumi kukua upungue. Kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitazungumza katika eneo langu la vipodozi. Nchi nyingi kwenye vipodozi wanaoshughulikia ni watu wanaoshughulika na afya. Hapa kwetu naamini kwamba TFDA ndiyo wanaoshughulika na mambo ya dawa, vyakula pamoja na vipodozi. Unakuta TFDA wamekupa certificate, hawana matatizo. Wamekupa, wanakwambia kabla hujaingiza mzigo wako, lete tuukague, tuupime, tunakupa certificate.

Mheshimiwa Spika, unapewa certificate na TFDA, unayo. Unaenda kuleta mizigo, TBS wanakwambia huu mzigo haufai. Hapo wanakinzana mno na ndiyo maana wamesababisha watu wengi wapite porini. Siyo watu wote wana nguvu za kuweza kupita moja kwa moja. Naomba hilo liangaliwe na hapa siwezi kulizungumza sana kwa sababu nilikuwa nimekuja na hayo mawili. Pongezi kwa Mheshimiwa Rais kuhusiana na property tax na hiyo ya mambo ya kupingana kwa Idara za Serikali. Kwa kweli zinapingana sana kiasi kwamba wale wadogo wadogo ambao wamekuja kabisa na kwamba wamelipia wana karatasi za DFTA, lakini huyu anakataa. Kwa hiyo, unakuta wanakinzana.

Mheshimiwa Spika, TRA wako very efficient, unakwenda unafika siku tatu. Maana tulikuwa tunachukua wiki tatu au nne, lakini sasa hivi TRA siku mbili au tatu wamemaliza kazi yao. Unaanza kupiga kwata huku TFDA, wamemaliza; unaanza na TBS. TBS umemaliza nao wanakwambia kuna vipimo. Jamani, Kampuni iliyotengeneza hiyo mizigo ni ya Kimataifa, nitatoa tu mfano labda Procter and Gamble, watengenezaji wakubwa ambao wako katika kila nchi na vipimo vinajulikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mtu anakwambia lazima tupime tu hii chupa kama kweli ni mills 50, naye umlipe. Tupime hii chupa ni mills 100 naye umlipe. Ni kweli kabisa na siyo kwamba nazungumza kwa kuambiwa, ni vitu ambavyo navisikiliza. Kwa hiyo, wangekaa pamoja ili wahakikishe kwamba tunafanya shughuli za uzalishaji na kukusanya kodi iwe rahisi. Itakuwaje rahisi? Ni kwa kuchukua hizi mamlaka kwamba wewe ndio utashughulika na hili, wewe ndio utashughulika na hili, kuliko kila mmoja huyu kikwanzo, huyu hapana.

Mheshimiwa Spika, nitampa Mheshimiwa Waziri mifano mingi lakini hapa muda sina, kwa hiyo, muda nitautafuta mwenyewe nimpelekee mifano nimwambie kwamba na hawa wanamkwamisha kukusanya mapato na ndiyo sababu ya watu kupita porini, siyo kwamba watu hawapiti porini na vitu havingii.

Mheshimiwa Spika, nchi hii ni kubwa, mipaka yake ni mikubwa. Wewe mwenyewe ukiangalia kutoka Mombasa uje ufike Mtwara, utoke Mtwara umalize yote Malawi; utoke Malawi uende Zambia; yaani mpaka ni mkubwa sana. Nakumbuka tukirudi huko nyuma, kulikuwa na uongozi uliwahi kulegeza, walikuwa wanakusanya mapato makubwa sana. Vikwazo havileti mapato, wala kodi kubwa haileti mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la tatu, naomba kumalizia, nalo hili Mheshimiwa Waziri wa Fedha nakushukuru kwa sababu kwanza namfahamu ni rafiki yangu kwa muda mrefu, mkaliangalie. Vipodozi siyo kweli kwamba ni anasa, vipodozi siyo sigara wala siyo pombe. Kama siyo sigara wala pombe na kila aliyepo hapa ndani hakuna ambaye hakupakaa kipodozi. Wanapoweka tax kubwa namna ile mpaka na excise duty utafikiri unauza sigara au pombe kali, hawamtendei haki huyu mlaji wa mwisho. Mimi nitaleta, lakini atakayeumia ni huyu aliyemo humu. Sasa wanaponiwekea hiyo kodi kubwa, siamini hata kwamba Mheshimiwa Dkt. Mpango anataka watu wanuke vikwapa humu ndani, haiwezekani. Kwa hiyo, vipodozi, nataka nimwambie kabisa siyo kitu cha anasa. Nenda nchi yoyote; nenda Amerika, nenda Ulaya vipodozi vinaingizwa kwa sababu wanajua faida yake, hakuna asiyepakaa. Kwa hiyo, waangalie hilo na waliangalie vizuri sana. Hayo mambo matatu; Idara zinazokinzana wakae pamoja...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana.