Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Goodluck Asaph Mlinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ulanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nataka nimpe taarifa kaka yangu Mheshimiwa Silinde amesema kwamba Serikali inatumia kichaka cha uhakiki kama kujificha. Kwa faida ya Bunge, mimi professional yangu ni Mtawala. Elimu ya juu nilisoma Utawala na ya juu zaidi nikasoma Sheria za Upatanishi na Usuluhishi. Kwa hiyo, migogoro hapa ni kaburi lake.

Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia uhakiki wa Watumishi Serikalini, hata wale wanaoenda kuhakikiwa wanajiandaa jinsi ya kukwepa ule uhakiki. Kwa hiyo, mnaweza ukazungumza uhakiki kwamba Serikali haimalizi uhakiki, mkumbuke hata wale wanaoenda kuhakikiwa na wale waliowaingiza wale watumishi hewa, kwa sababu wanajua wakigundulika na wenyewe watakuwa matatani, kwa hiyo wanajiandaa jinsi gani ya kukwepa huo uhakiki. Kwa hiyo, wasiituhukumu Serikali tu wakasema uhakiki hauishi. Sisi watawala tunaelewa uhakiki maana yake ni nini na changamoto zake ni zipi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo langu la pili ambalo nilikuwa natamani sana kulizungumza leo kwa kupata nafasi hii, nchi yetu mwanzo ilikuwa nchi ya wakulima, wafanyakazi na wafanyabiashara. Kuna kundi lingine limeongezeka kubwa sana. Sasa hivi nchi yetu ni ya wakulima, wafanyakazi, wafanyabiashara na wacheza kamari. Bahati nzuri imezungumzwa, sasa hivi wanafunzi wote wa Vyuo Vikuu wakipata mikopo wanajazana kwenye vituo vya kucheza kamari.

Mheshimiwa Spika, pia wazee wetu wakipata pension wanaenda kucheza kamari; wake zetu, zamani sisi enzi zetu wakati tunaoa, unaambiwa ili uwe na maisha mazuri, ukipata kahela kako mpelekee mkeo akatunze. Ukimpelekea mke, ukija kuchunguza simu zake, unakuta meseji za Biko na Tatu Mzuka. Madereva wa Bodaboda wote, yaani vijana wote tunavyozungumza sasa hivi, wote wanacheza kamari. Hili ni janga la Taifa. Gaming Board watafute namna gani ya kuliratibu.

Mheshimiwa Spika, madhara ya kamari ni makubwa kuliko biashara nyingine. Rafiki yangu Mheshimwia Musukuma hapa alikuja na zao lake mbadala kwa ajili ya kutuletea uchumi tukalikataa, tukasema lina madhara, lakini ninavyokwambia kamari madhara yake ni makubwa kuliko bangi au kuliko hata viroba. Kwa hiyo, tutafute utaratibu wa kuendesha kamari, lakini siyo kama sasa hivi inavyoenda.

Mheshimiwa Spika, labda tu kwa watu ambao hawajui madhara ya kamari; kwanza, imevunja nguvu kazi za nchi yetu. Zamani ilikuwa ukienda vijijini unawakuta vijana wanacheza pool table. Sasa hivi pool table haipo, vijana wote kwenye betting maana kamari zenyewe ziko nyingi, zimeongezeka, mara kuna Tatu Mzuka, Biko, sijui Mkeka Bet, sijui nini bet, yaani ziko nyingi kweli kweli na zinaongezeka kwa kasi, umeona.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nguvu kazi ya vijana imepotea. Vijana wote wanaamini watakuwa matajiri, kwa sababu matangazo yale ambayo tumeyaruhusu kiholela sasa hivi inawafanya vijana wengi wawe na tama. Mtu anasema nitapata kesho, nitapata kesho. Kwa hiyo, akipata kihela kidogo, kwenye kamari.

Mheshimiwa Spika, madhara mengine ni addictive. Mtu yeyote anayecheza kamari hawezi kuacha. Nao walivyokuwa wataalam, anakupa Sh.5,000/= leo umeshinda. Ukishinda Sh.5,000/= hiyo huwezi kuacha, hata ucheze shilingi milioni 20 hutaacha. Kwa hiyo, inasababisha hiyo addictive, wenyewe wanaita uteja.

Mheshimiwa Spika, lingine madeni. Watu sasa hivi wanaenda kukopa kwenye Vicoba ili wacheze kamari. Kwa hiyo, inasababisha Taifa la watu kuwa na madeni. Ndiyo maana hata ukienda kwenye Vicoba mikopo hailipiki, watu wanakopa kwa ajili ya kwenda kuchezea kamari. Hivyo, malengo ya Taifa letu yanapotea kwa sababu wengi wanaweka malengo kwa kutegemea kamari.

Kwa hiyo, ndiyo hivyo. Ninachoomba Gaming Board watafute utaratibu wa kuendesha haya mazoezi ya kamari, lakini siyo kwa mfumo huu. Watafute mfumo mwingine. Wametoa matangazo; kuna tangazo wamelitoa zuri, lakini hilo tangazo linapita kwa watu kiasi gani? Maana yake wanasema, usitumie fedha yenye malengo mengine kuchezea kamari. Hebu niwaulize, leo hii Tanzania nani ambaye ana pesa ambayo haina malengo imekaa tu? Kila pesa tunayoipata ina shughuli , ada za shule, nini na vitu vingine, lakini watu wanaishia kwenye kamari.

Mheshimiwa Spika, kuna mwanafunzi mmoja alijinyonga juzi juzi hapa kwa sababu alitumia pesa ya ada kwenye kamari na akaliwa. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri wakati ana wind-up atuambie ni namna gani Gaming Board watatafuta utaratibu wa kuendesha kamari bila kusababisha matatizo ambayo yanatokea sasa hivi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili, wakati Serikali yetu ya Awamu ya Tano inaingia madarakani, tulikubaliana Serikali nzima tubane matumizi yasiyo na tija ili hiyo pesa tuipeleke sehemu nyingine ya maendeleo. Kweli tulifuta safari za nje kama Bunge, sasa hivi hatuendi nje. Taasisi za Serikali zilitoa fedha zao kutoka kwenye mabenki ya biashara wakapeleka Benki Kuu. Pia pakatolewa maelekezo kuwa tutumie huduma zinazozalishwa na taasisi za Serikali. Hata matibabu ya nje yalizuiliwa. Mpaka mtu aende kutibiwa nje inatakiwa utaratibu mrefu na ionekane kuna haja ya muhimu kabisa huyu mtu kwenda kutibiwa nje.

Mheshimiwa Spika, hivi ninavyoongea, Benki Kuu ya Tanzania ndiyo taasisi inayotumia fedha nyingi katika matibabu bila msingi wowote. BoT Mfanyakazi akiwa na mafua anaenda kutibiwa Uingereza au India. Wanatumia fedha nyingi na wamesahau kuwa hizi fedha ni za walipa kodi.

Mheshimiwa Spika, Taasisi zetu za Serikali zimewekewa utaratibu maalum kwa ajili ya kupatiwa matibabu. Tunaitumia NHIF, hata Bunge tulikuwa tunatumia Private Company sasa hivi tumeingia NHIF, BoT wanatumia Private Insurance gharama ya matibabu ambayo wangeitumia NHIF shilingi bilioni moja wanatumia shilingi bilioni 12 kwa mwaka. Angalia ufisadi wa hali ya juu uliopo. Shilingi bilioni moja kwa shilingi bilioni 12 kwa sababu watu wana maslahi binafsi.

Mheshimiwa Spika, wewe ni shahidi, wanasema wao hawawezi kwenda NHIF kwa sababu haina matibabu nje ya nchi. Sasa naomba niulize, wao wanasema taasisi yao ni nyeti, Usalama wa Taifa wako NHIF, Bunge tuko NHIF, PCCB wako NHIF. Mke wa Rais aliugua, alilazwa Muhimbili, lakini BoT hawakubali. Wanasema wao taasisi yao ni nyeti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge tulikubali hadi matezi dume tulipimwa kwenye Dispensary ya Bunge hapa hatukuona tatizo, lakini wao mtu akiugua kidogo wanataka kwenda nje.

Mheshimiwa Spika, naomba ulisimamie hili. Kuna ufisadi mkubwa katika mchakato huu wa BoT kwenda kupata matibabu kwa kutumia Private Insurance.

Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache, siungi mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri mpaka atakapokuja na majibu ya haya niliyoyatoa. Ahsante.