Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Masoud Abdalla Salim

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtambile

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu wataala aliyetujalia uzima na afya njema katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani katika kumi hili la Maghfira ikiwa ndio siku ya 19 na nikimwona rafiki yangu Mheshimiwa Ally Keissy ametulia kweli kweli leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Watanzania tulitegemea makubwa kutoka Wizara ya Fedha. Tulitegemea fedha ambazo Waheshimiwa Wabunge tunazipitisha sisi katika maeneo mbalimbali fedha hizi za maendeleo zitakuwa zikitolewa, lakini imekuwa ni kizungumkuti; haifahamiki, hali ni mbaya, tatizo limekuwa ni kubwa.

Mheshimiwa Spika, fedha za maendeleo katika Wizara mbalimbali hazitolewi kwa wakati hata zikitolewa basi inakuwa ni pungufu sana na inaonekana hadi sasa ni chini ya asilimia 40 ya fedha za maendeleo katika maeneo mbalimbali ya Wizara ambazo tumezipitisha. Hili ni janga kubwa, ni tatizo kubwa, tatizo ambalo wananchi mategemeo yao waliyokuwa na huyo yameondoka. Mheshimiwa Waziri wa Fedha atuambie tatizo hasa ni nini kwake Wizara ya fedha? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia kwenye volume II Treasury mambo ambayo waliyojipangia katika maeneo mbalimbali, ukienda kwenye book four, nimwambie Waziri wa Fedha, kama kuna tatizo la vyanzo vya fedha, hana fedha ripoti ya Spika ambayo imewekwa juzi Jumamosi pale Mezani kuna fedha ambazo zilipatikana kwenye uvuvi wa bahari kuu, hivyo ni vyanzo, kuna mambo tayari yapo kwenye ripoti ya Tume ya Spika aliyoiunda, vyanzo vya kutoka bahari kuu kuna matrilioni ya fedha, hebu aingie atafute fedha tatizo nini, mbona haeleweki, hasomeki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni kuhusu wastaafu, hali ya wastaafu ni mbaya sana, wastaafu wetu kwa kipindi kilichopita walikuwa kwenye kima cha chini kutoka Sh.50,000 hadi Sh.100,000 baadhi yao walio wengi, lakini ahadi yetu kwa wastaafu kwa hivi sasa inaonekana kama Serikali haina dhamira ya dhati kuboresha hawa wastaafu wetu ambao wastaafu walikuwa ni watumishi wetu, walifanya kazi kwa uadilifu kwa muda wa kipindi kirefu lakini hali zao za maisha ni mbaya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye hotuba hii ukiangalia Waziri hana jambo ambalo la kushika zaidi akasema kwamba labda wastaafu hawa wataweza kupata maslahi yaliyo mazuri ukurasa 104 kaeleza mengi, lakini kasema tu kuna moja, mbili, tatu.

Mheshimiwa Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, wastaafu wetu katika kada mbalimbali hali zao ni mbaya sana. Nitoe mfano mmoja, wakati wastaafu kwenye Jeshi la Wananchi kuanzia cheo cha private hadi Brigadier General Jeshini mafao yao yanakuwa ni madogo sana mbali ya hao wengine, hawa walifanya kazi, walikwenda kwenye vita, vita va Kagera, walikwenda Msumbiji na kwingineko, leo wanayafungua mageti kwa watu binafsi inaumiza kweli kweli hasa kuanzia cheo cha private, Brigadier General hata hawa walinzi wetu hatuwathamini hawa walinzi wetu walipigana vita na Kagera, waliokwenda kuokoa Msumbiji hata hilo? Mwaka huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hili nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, mwenzake Waziri aliyepita Mheshimiwa Saada Mkuya aliweza kufanikisha kupandisha hizi pension za wastaafu kwa kila mwezi, hebu naye ajiandae, aandae mazingira mazuri apandishe hizi pension za wastaafu za kila mwezi kwa sababu hali imekuwa ni mbaya sana.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri aangalie vilevile katika suala la wastaafu pale wanapostaafu, kwanza mafao yao wanacheleweshewa sana, lakini yeye amesema kwamba wataandaaa mazingira, mazingira hayapo kwa sababu gani kumekuwa na kudhulumiwa, kumekuwa na kunyonywa kwa wastaafu kwa muda mrefu hata ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali mbalimbali zimekuwa zikisema kwamba mafao ya wastaafu wanapunjwa.

Mheshimiwa Spika, watu wamefanya kazi kwa uadilifu, wamechoka hata mafao yao, ripoti za CAG zipo kibao, nyingi sana ripoti mbalimbali kwamba mafao ya wastaafu wanapunjwa tangu mwaka 2013, angalieni ripoti za CAG, jinsi wastaafu wanavyonyonywa na kupunjwa. Kumbe wazee wetu maskini kwa sababu ya Serikali wanawadhulumu na kuwapunja tatizo nini? Mwaka huu.

Mheshimiwa Spika, naomba niseme pale ambapo mstaafu anafariki. Anapofariki mstaafu wanafamilia wanafungua mirathi, lakini niseme tu kwamba inakuwa na milolongo mikubwa sana kuzipata zile haki. Familia inapofungua ile mirathi wakifika pale mahakamani ndani ya muda mfupi sana Hazina wanaambiwa kwamba hicho kitu faili lake halionekani. Baada ya mwezi mmoja kufa faili lake halionekani na hayo yapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mzee Bobali, baba yake mdogo Mheshimiwa Bobali hapa, muda mrefu tangu amestaafu huu ni mwaka wa kumi na hajapata mafao yake, ni tatizo kweli wanaofariki na wao mafaili yao wanaambiwa hayapo. Kwa kweli wastaafu wametupwa, wanaonewa hili ni jambo kubwa sana na jambo ambalo kwamba halikubaliki.

Mheshimiwa Spika, nadhani kwamba hakuna kitu kinachoumiza kwamba watu hao walitumika katika hali nzuri sana wakati wakiwa na nguvu lakini wameachwa Mheshimiwa Waziri atuambie tatizo ni nini alilonalo na ahadi ya Serikali kwa wastaafu, kuna kipi kikubwa zaidi ambacho wanawapelekea mpaka leo wanakuwa maskini sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niache hilo, pale Hazina kuna bwana anaitwa nadhani Kasekwa, yule huyu ni mtu mmoja ambaye namwamini sana, kwa hiyo yale mafao ambayo yakitengenezwa na bila shaka hapa atakuwa yupo. Huyu aungane na wale na wenzake, ashauriane na wenzake ili hayo mambo yaende vizuri, ni mtu mmoja mzuri sana nadhani anakuwa ni Katibu Mtendaji si ndio ana cheo fulani pale, nina imani kubwa kwamba hili jambo wataweze kulifanya vile ambavyo inavyohitajika.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo linawaumiza sana ni suala zima la shilingi milioni 50 kwa kila kijiji. Volume four ukurasa wa 24, Poverty Eradication Department, subvote 81,000, item 6508 hapa wameweka. Wanaweka nini humu na hawatekelezi, huku ni kudanganyana bure. Najua ikifika wakati wanakuja kifungu hicho kimeafikiwa na ni cha mwisho kifungu hicho kimeafikiwa ohh, waoo, hamna kitu, hawatoi fedha wanadanganya, wananchi wanasubiri kwa muda mrefu na hawajatoa hizi fedha, wanaandika kwenye vitabu, lakini hakuna kitu, tatizo nini, bora muwaambie tu kwamba, ni kweli hizi fedha hazipatikani sababu ni moja, mbili, tatu.

Mheshimiwa Spika, ni ahadi kweli ya Mheshimiwa Rais, akishasema jambo, jambo hilo ni lazima litekelezwe, Mheshimiwa Waziri tatizo lake nini, kama hana vyanzo hata juzi Kamati ya Gesi imesema kuna mabilioni mengine hayo chukua fanyieni kazi, mbali ukiachia leo uvuvi wa bahari Kuu, nawashangaa.

Mheshimiwa Spika, nawauliza Serikali kuna nini huko mwaka huu, hayo ndiyo maisha, mbaya mzunguko wa fedha hakuna, kila tunaposema tuna vyanzo fulani wachukue vyanzo fulani wavifanyie kazi hawataki, sasa wanataka ushauri kutoka wapi na sisi ndio Wabunge wao, tena Wabunge, Wabunge kweli, shauri yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, randama hii hapa, wameeleza katika hii randama, ukurasa wa 119 mpaka 120, wameweka hii maelezo yao waliweka hapa, naombeni sana sisi ni Wabunge waelewa sana, wasitufanye hivi, Wabunge wote ni waelewa sana humu, waandae mazingira basi hizi fedha milioni 50 kwa kila kijiji wametenga bilioni 60, hizi kila mwaka wanatenga, lakini fedha hizi wananchi wanalalamika Wabunge wanasema labda jambo hili limewashinda Waheshimiwa Wabunge, tunawaambia lakini Serikali sio wasikivu, Serikali haitaki kusikia.

Mheshimiwa Spika, naomba kwa hili tena leo Ramadhani kumi la maghfira hili, anajua Mheshimiwa Ashatu nazungumza hivi taratibu sana, kama ingekuwa miezi mingine ningesema maneno mengine, wajitahidi sana waandae mazingira hizi fedha zitolewe, hali ni ngumu sana .

Mheshimiwa Spika, nimalizie jambo moja dogo, kwani kuna tatizo gani katika hali ya maisha wanayoiona Watanzania na mzunguko wa pesa na maelezo ya Mheshimiwa Waziri kuwa deni bado himilivu, tuendelee kukopa, sawa na utaalam wake mimi siko huko, lakini kwa nini kwenye hotuba yake ya mwaka jana alituambia hapa kwamba nia yake ni kuandaa mazingira, wale wanaokula mlo mmoja kutoka asilimia 9.7 sasa waende mpaka asilimia 5.5, hotuba yake ya mwaka jana hiyo, ni maelezo yake, lakini mbona wanaokula mlo mmoja wameongezeka, umaskini umeongezeka.

Mheshimiwa Spika, sasa alichokisema mwaka jana hajakisimamia Mheshimiwa Waziri, sisemi kama yeye ni mwongo lakini hakusema kweli, simwambii kwamba mwongo hapana, siwezi na Ramadhani hii, lakini hakusema kweli kwa sababu haya ni maandishi yake kwamba tutahakikisha katika bajeti zinazofuata wanaokula mlo mmoja wataondoka katika asilimia 9.7 mpaka asilimia tano, leo maskini wameongezeka, hiyo asilimia aliyosema haipo, wanaokula mlo mmoja wengi, wengine hakuna mlo, maisha magumu, hali mbaya kupita kiasi, tukisema kuna vyanzo chukueni… (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa wananchi, nenda Kongwa, nenda Mpwapwa, nenda Dar es Salaam , nenda Mbeya, nenda Iringa kusanya watu upate hiyo, tunaangalia takwimu yake ambayo ametupa awamu iliyopita, sisemi kwamba ni muongo lakini jambo limemshinda fedha ziko wapi, tatizo nini? Hamueleweki! Nawashangaa mwaka huu! Kama kweli Serikali sikivu andaeni mazingira basi msikie.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya fedha ni tegemeo kubwa sana kupita kiasi, Watanzania wote wako na sikio kuangalia Wizara ya Fedha itafanya nini kuboresha maisha ya Watanzania. Leo maisha ya Watanzania yamekuwa ni ombaomba walio wengi, kila siku umaskini unaongezeka, uchumi unakua umaskini unaongezeka nchi gani duniani hakuna uwiano baada ya uchumi kuongezeka…

Umaskini umeongezeka na uchumi unaongezeka…

Mwaka huu, haya tutawaona!