Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini

Hon. Hamoud Abuu Jumaa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibaha Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini

MHE. HAMOUD A. JUMAA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, napenda kumshukuru Mungu mwingi wa rehema kwa kuniwezesha kufika mahali hapa nami kushiriki katika kikao hiki cha bajeti ya Wizara ya Madini ya mwaka 2018/2019. Naipongeza Wizara kwa kuandaa bajeti nzuri itakayokwenda kuboresha sekta hii yenye changamoto mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuipongeza Serikali kwa kuimarisha usimamizi katika sekta ya madini ili kuwezesha sekta hiyo kuchangia kikamilifu katika uchumi wa nchi, kuongeza mapato ya Serikali na kuzalisha ajira. Hatua zilizochukuliwa na Serikali ni pamoja na kukusanya taarifa za uzalishaji wa madini, kuimarisha ukaguzi wa uzalishaji na mauzo kwenye migodi mikubwa na midogo na kufuatilia ukusanyaji wa maduhuli.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha naipongeza kwa zoezi la ukaguzi lililowezesha kukamatwa kwa madini yaliyokuwa yakitoroshwa yenye thamani ya Dola za Marekani takribani 898,523 na shilingi milioni 557. Kwa taarifa za Serikali, ni kwamba katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Februari, 2018 maduhuli ya Serikali yaliyokusanywa kutoka sekta ya madini yalifikia shilingi bilioni 180.4. Pamoja na mambo mengine, mafanikio hayo yametokana na usimamizi makini katika sekta ya madini na uamuzi wa Serikali kufungua soko la tanzanite nchini. Hatua hizi ni nzuri na ziwe endelevu kwa manufaa ya Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali imeimarisha soko la madini nchini kwa kuhakikisha kuwa madini yanauzwa kwa ushindani ili kuyaongeza thamani na kulipatia Taifa fedha kwa kupitia kodi. Hata hivyo, itakumbukwa kwamba tarehe 20 Septemba, 2017, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alielekeza ujengwe ukuta katika eneo linalozunguka Mgodi wa Tanzanite uliopo Mererani ili kuimarisha ulinzi na kudhibiti utoroshaji wa madini hayo, ujenzi wa ukuta huo wenye mzunguko wa kilomita 24.5 umekamilika. Nitumie fursa hii pia kuwapongeza viongozi na watendaji wote walioshiriki katika ujenzi huo, kwani umesaidia sasa madini yetu ambayo ni ya pekee kwa kuwa yanapatikana Tanzania tu kuwa salama ukilinganisha na hapo awali.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza pia Serikali kwa kuja na mkakati katika mwaka 2018/2019, kuwa Serikali itaendelea kuwajengea uwezo wazawa ili washiriki kikamilifu katika sekta ya madini, kwani uwezeshaji huo utakwenda sambamba na utoaji mafunzo kwa wachimbaji wadogo kuhusu teknolojia mbadala ya uchenjuaji dhahabu kwa lengo la kupunguza athari za mazingira na maafa katika maeneo ya migodi. Hatua hizi zote hapo juu ni za kujipongeza kwani ni hatua muhimu kwa kuhakikisha sekta hii muhimu inaliingizia pato Taifa na kukuza uchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kila kwenye mafanikio hapakosi changamoto na changamoto hizo huzichukua kama fursa ili kuboresha maeneo husika. Bado tuna changamoto kubwa hasa kwa wachimbaji wadogo kutopata elimu ya kutosha na kufanya uchimbaji wenye tija na usioleta athari za kimazingira. Wachimbaji hawa wanapaswa kupewa elimu ili uchimbaji wao ulete tija na Serikali iweze kukusanya kodi zake. Naishauri Serikali kuwapa elimu wachimbaji wadogo kama nilivyosema hapo awali katika kuwapa elimu ya teknolojia mbadala ya uchenjuaji dhahabu na pia iwape elimu ya uchimbaji wenye tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Serikali inapaswa sasa kuwaangalia hawa wachimbaji wadogo pindi wanapoagiza vifaa kazi namna ya kuwapunguzia kodi. Kufanya hivyo kutawasaidia kufanya kazi kisasa na kuongeza uzalishaji na kupelekea Serikali kupata kodi yake ipasavyo bila shaka yoyote. Aidha, naishauri Serikali kuendelea kusimamia ipasavyo rasilimali zetu zote katika sekta hii kwani tumeshuhudia mambo mengi ya hovyo yakifanywa na baadhi ya watendaji wetu wasiokuwa waaminifu wakishirikiana na baadhi ya wawekezaji ambao nao sio waaminifu kutudidimiza na kujipatia faida kubwa huku Taifa likiambulia patupu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kumekuwepo na changamoto ya wachimbaji wadogo kuondolewa katika maeneo yao na kutokupewa maeneo mbadala. Ni wajibu wa Serikali kuwalinda wachimbaji wadogo kwani sekta hiyo imetoa ajira kwa watu wetu katika maeneo husika ya machimbo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna changamoto ya migogoro baina ya wawekezaji na wachimbaji wadogo, ni vema ikaangaliwa na kutatuliwa kwa wakati ili pande zote mbili husika wakaendelea na majukumu yao ipasavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.