Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini

Hon. Julius Kalanga Laizer

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Monduli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Naibu Spika, nami ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii, kwa kweli niwe muungwana kwamba mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Historia ya uchumi wa madini kwenye nchi yetu kuanzia siku za nyuma na hapa tulikofika, hauwezi kabisa kuacha kutambua juhudi zinazofanywa na Serikali katika kudhibiti utoroshaji wa madini nchini kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna dhamira ya kweli katika kushughulikia jambo hili. Hata hivyo, katika dhamira hiyo hiyo ni lazima tutambue kwamba misingi ya wizi wa madini kwenye nchi yetu ulianzia wapi na hatuwezi kulinda rasimali za nchi hii kwa mtutu wa bunduki wala kwenye majukwaa ya siasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo kubwa naloliona ni sheria zetu haziko katika mazingira mazuri ya kulinda rasimali ya Taifa. Kwa hiyo, naamini katika nia njema hii ya Serikali, ni lazima tutambue sheria zetu ndiyo kinga pekee katika vizazi vyote kusaidia kusimamia rasilimali ya Taifa hili. Inawezekana Rais huyo akawa na nia njema lakini kama hatujaweka misingi imara kwa ajili ya kusimamia rasilimali zetu hizi, atakuja Rais mwingine tutarudi kule kule tulikotoka. Kwa hiyo, hatutamani ulinzi wa rasilimali zetu utokane na utashi wa mtu mmoja au kikundi cha watu wachache. Tunatamani ulinzi wa rasilimali zetu utokane na utashi na sheria za nchi ambazo zimesimamiwa vizuri na ambazo zinalazimisha viongozi kusimamia sheria hizi. Tusije tukatoka mahali ambapo tunaenda mbele tunarudi nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya utangulizi huo, naomba niseme mambo machache. Ukiangalia katika ahadi ya makenikia ya dola milioni 300, ambapo mpaka sasa hivi hatujapokea, hii ni kwa sababu ilikuwa ni utashi wa wale wenye makinikia kuahidi, lakini ingekuwa ni jambo la kisheria fedha zetu tungeshapata, hatujapata kwa sababu ilikuwa inaonekana kama ni hisani. Kwa hiyo, ndiyo maana nasema, lazima tuwe na sheria ambazo zinalinda rasilimali zetu.
(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kidogo kwenye changamoto zinazowakabili wachimbaji wadogo na ni muhimu Mawaziri wakatuelewa katika hili. Hatuchukii kabisa walioko katika maeneo yale Serikali kukusanya kodi. Kwa mfano, madini ya ruby ambayo bei yake imeshuka kwa sababu ninyi mnataka tukate kama inavyokatwa tanzanite, madini haya hayafai kukatwa na ninyi mnachukua muda mwingi sana kutoa mwelekeo kwamba ni namna gani mnataka madini yale yasimamiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, walikuja Naibu Mawaziri wawili kule Longido kwetu, wakatoa ahadi za kutosha mpaka leo hawajatekeleza. Ni muhimu sana mkashughulikia jambo hili kwa haraka, siyo mnafanya ziara tu tunakuja tunawapokea mnatupa matumaini na matumaini hayo hamyatekelezi. Wachimbaji walioko kwenye maeneo yetu wanapata changamoto nyingi sana kwa sababu madini haya yameshuka bei kule Mundarara na mpaka leo hatujajua nini msimamo wa Serikali katika hilo. Wamekuja watu wawili ni vijana wakatuahidi kwamba tutaleta hizi sheria mara moja, hakuna kitu. Naomba leo waniambie hili suala la Mundarara linamalizika lini. Tena Waziri akasema Wamasai tunajenga, tunajenga kweli, sisi hatuoi kama Wasukuma, sisi tukipata fedha tunajenga, tunanunua vitu vingine, sasa watuambie ni lini suala hili la Mundarara litafika mwisho kuhusu madini ya ruby ili wananchi wetu waweze kunufaika na madini haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili kwenye hilo, eneo la madini ya Mererani. Naomba Wizara waseme, nani anayepaswa kusimamia wachimbaji wadogo, Polisi wamegeuza wachimbaji wadogo wa Mererani kuwa chanzo chao cha kupata fedha. Wale wanaofanya biashara ya madini siyo wachimbaji, wananunua wakauze, lakini wakishatoka kununua yake madini watu wanakamatwa wanaambiwa lipa kodi. Sasa anayekusanya kodi ni TRA au Polisi? Wasaidieni wananchi hawa, wanaumizwa kabisa barabarani na bahati mbaya wale Polisi wamejua maeneo yao, akikutwa na jiwe anaambiwa lipa kodi, sasa analipaje kodi wakati hajauza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ule ni ujasiriamali tu, kuna wanaochimba lakini kuna wale wanaookota kwenda kuuza. Ni utafutaji wa riziki, watu wanateseka katika kutafuta lakini wanachajiwa kodi ambayo hauna sababu ya msingi. Lazima mtupe maelekezo ya wale wachimbaji wadogo na wale wafanyabiashara wa madini watakavyonufaika na watakavyolipa kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu, Mheshimiwa Waziri Rais aliwahi kusema kwamba suala la utoaji wa leseni lizingatie wananchi wanaokaa kwenye maeneo yale. Tuna tatizo la mchanga wa kujengea wale watu wanaenda kushika PR kwenye mashamba ya wananchi, kwenye vyanzo vya maji, wanapewa huko kwenye Kanda wakija huku hawaelewi chochote, hawasilikilizi wananchi, wanawaondoa wananchi, hatuna manufaa nayo, wanatuachia mashimo. Ni muhimu mbadilishe ile sheria ili mtu anayetaka leseni ya madini kwenye eneo fulani aanzie kule kijijini na hakutakuwa tena migogoro kwa sababu wananchi watakuwa wameshiriki kuanzia mwanzo mpaka mwisho, kuliko kuja kuingia kwenye migogoro ambayo hauna sababu ya msingi. Hii sheria naomba muipitie muone namna ambayo mnavyoweza mkafanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, tuna tatizo la ufisadi katika Wizara hii katika sehemu ya watumishi. Wako Makamishna Wasaidizi 12, miezi sita sasa wamesimamishwa kazi na Katibu Mkuu wa Wizara na wameajiriwa watu wengine katika nafasi hiyo, kwa hiyo, kuna malipo mara mbili, yaani wale walioko kazini na wale ambao hawako kazini. Kama Serikali inaona Makamishna hawa hawatoshi, wastaafisheni kwa maslahi ya umma muwalipe mafao yao, kuliko kuwalipa Makamishana Wasaidizi 24 kwa wakati mmoja, wakati uhitaji wenyewe ni 12. Wale ambao mmewarudhisha nyumbani, wapeni maslahi yao, kama hamuwapi, warudisheni kazini, kuliko kuwaweka nyumbani halafu, wengine wanalipwa. Hii ni hasara kwa Serikali kwa kulipa watumishi pasipokuwa na sababu ya kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho, ni suala hili la makinikia na ulinzi wa ukuta wa Mererani. Ukuta wa Mererani ni hatua ya kwanza ya kudhibiti rasilimali zetu na madini haya nami naiunga mkono, lakini tukiendelea na utaratibu huo hivi huo ukuta tutalinda kwa mtutu mpaka lini, tutalinda na Jeshi mpaka lini?