Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini

Hon. Sixtus Raphael Mapunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye hii Wizara ya Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nichukue fursa hii kumpongeza sana, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuiangalia hii sekta ya madini. Kuchimba madini katika status yetu ya sasa siyo jambo ambalo ni too early au too late, maana yake kuna wengine wanalalamika tumeibiwa au tumefanyiwa nini, ukiangalia Tanzania ilivyo na madini ya kila aina kuanzia Mto Ruvuma kupakana na Msumbiji, mpaka North Mara, kila mkoa utakaogusa vitu vilivyoko chini havijawahi kuguswa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kukurupuka tu kwenda kuanza kwenda kuchimba leo bila kutengeneza mifumo mzuri ya kisheria na ya kiutendaji katika sekta ya madini, hatutafanikiwa. Nimshukuru Rais na naishukuru sana Wizara, nimpongeze Waziri anafanya kazi vizuri sana na Naibu Mawaziri wake wawili, kila siku unawaona wanasikiliza wachimbaji wadogowadogo, unaona wako na wachimbaji wakubwa, unaona kabisa kuna vitu wanakusudia kututoa hapa tulipo kutupelekea mbele zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema hapo mwanzo tuko kwenye mpito, kutengeneza mfumo bora wa kujinufaisha na madini yetu lakini wakati huo Serikali lazima ipate mapato kwa ajili ya kuleta shughuli za maendeleo kuendeleza watu wake. Haya mambo yote yanahitaji utulivu wa akili, ushirikiano na kupeana moyo. Huu mfumo ni mpya, hakuna mtu asiyejua biashara ya dhahabu ni ya familia kubwa duniani, wote tunajua, jinsi ya kuingilia hili lazima utumie ubongo mkubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna watu walianza hii biashara wanasema Karne ya 5 baada ya Kristo mpaka leo wameendelea kuchukua dhahabu na ndiyo wenye stock kubwa ya dhahabu duniani, Uingereza na Marekani. Kwa hiyo, unapoingia kupambana na hawa watu, lazima uwe na mfumo mzuri wa kisheria vilevile uelewa wa watu wako.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa minajili hiyo, naishauri Serikali kwamba inapoendelea na kazi yake nzuri ya kutengeneza mifumo, kwa namna yoyote ile mikataba inayotengenezwa na hao waliokuwa wakitunyonya siku zote na ndiyo tunaowategemea wanunue madini yetu, kwa haraka hawa hawawezi wakakubali kiurahisi, lazima kuna maeneo watatuhujumu. Lazima tuende na mpango ‘B’ kipindi tunategemea wawekezaji kuja, Serikali kwa dhati kwa sababu dhahabu haiozi hata ikachimbwa ikahifadhiwa hapa hapa kuna siku thamani yake itakua, niiombe Serikali ijielekeze kwa wachimbaji wadogo wadogo kwenye yale maeneo ambayo tumekwisha kuyaainisha, kwa sababu tumekwisha kuthibitisha kwamba wachimbaji wadogowadogo ndiyo wale wanaoleta tafsiri ya maendeleo, maendeleo is a social centred. Kila sehemu wachimbaji wadogo wadogo walipofanya kazi zao vizuri maeneo yale yalithibitika kuonekana yakiendelea sana watu wakijenga nyumba vizuri na kadhalika. Tukii-paralyse hii sekta ya wachimbaji wadogowadogo hatutafanikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe sana Wizara, inafanya vizuri katika kuwasaidia ruzuku lakini iwasaidie vilevile katika elimu, itoe elimu ya biashara ya madini lakini itoe elimu ya madini katika ujumla wake. Niliwahi kuongea na mtu mmoja anafanya kazi katika sekta ya madini huko China, akasema Tanzania mna bahati ya kuwa na maliasili za kutosha lakini hamjasomesha vya kutosha watu wakawa na uelewa wa madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali watu wale 20, 30 tunaowapeleka kila mwaka kusoma nje, kwa rasilimali tulizokuwa nazo ni wachache sana, tuongeze nguvu ya kutosha tuwapate wengi ili kila mkoa uwe na wataalam na tufanye assessment vizuri, hata kama mwekezaji akifika tunajua exactly anakwenda kwenye madini ya aina gani. Wakija kufanya assessment wao matokeo yake wanatupunja na kutuibia nchi yetu inaendelea kuwa shamba la bibi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa sehemu moja, nimepitia hotuba ya Waziri, kwenye sehemu ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania. Hii taasisi ni muhimu sana katika sekta ya madini. Nimeangalia hapa, maduhuli yao ni shilingi milioni 350, mwaka uliopita walikusanya shilingi milioni 294, tafsiri yake hiyo ndiyo watumie kwenda kufanya research nchi yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, wana majukumu tisa, yote ni mazito, ila niyaseme mawili tu. Jukumu la nne wanasema, kuwasaidia wachimbaji wadogowadogo hasa katika kubaini umbile na aina ya mbale, kutambua aina na ubora wa madini, pamoja na namna bora ya uchenjuaji. Hili jambo ni kubwa, shilingi milioni 350 haiwezi ikatosha hawa wakaweza kuifanya kazi hii nchi nzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, wana kazi nyingine ya kisayansi very technical, ya tano, kuratibu majanga asilia ya jiolojia kama vile matetemeko ya ardhi, milipuko ya volcano, maporomoko ya ardhi na kutoa ushauri wa namna bora kujikinga. Kwa bajeti ya shilingi milioni 350 hawawezi wakaweza ku-predict leo Oldonyolengai lini ile volcano ita- erupt. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali ijaribu kuwaangalia hawa ndiyo watakaotusaidia kujua nchi yetu tuna rasilimali kiasi gani, ziko wapi, zenye thamani gani na zichimbwe vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.