Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini

Hon. Allan Joseph Kiula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini

MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nishukuru kwa kuweza kupata nafasi ya kuchangia katika Wizara hii muhimu. Pia nishukuru kwa kupata fursa hii adimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nawashukuru Viongozi wa Wizara tukianzia na Waziri, Naibu Mawaziri wake wawili na timu nzima ya Wizara kwa kazi kubwa wanayofanya ya kufikia maeneo yetu ya madini. Sote tumeona jinsi kazi inavyofanyika, jinsi wanavyowajibika, tutakuwa wanyimi wa fadhila kama hatutawashukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, asubuhi yupo Mbunge mwezangu wakati anachangia alisemea suala la Tumuli, wachimbaji wa dhahabu walikuwa na mgogoro pale kuhusu mambo ya fidia lakini Naibu Waziri alifika Mheshimiwa Stanslaus Nyongo akaongea nao na aliongea kwa ujasiri mkubwa sana na alikuwa focused na aliweka msimamo wa Serikali na ndivyo nilivyotarajia. Kwa hiyo, alipoondoka pale nilikuwa niko vizuri sana kwa sababu hawa wawekezaji tusipokwenda nao vizuri wakati mwingine wanadharau vyombo vya Serikali, maadam tunasimamia haki kwa hiyo Waziri alifanya kazi kubwa sana na nampongeza kwa hilo pia natambua kwamba alikuwa anafanya kazi kwa niaba ya Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kuna eneo la Dominiki wamegundua madini ya gypsum yanachimbwa huko lakini kulikuwa na mgogoro. Nachotaka kusema hapa ni kwamba Maafisa Madini walioko kwenye Kanda na Mkoa wakitoa leseni wao wenyewe waweze kufika katika maeneo husika ili kutoa taarifa hizo kwamba tumetoa leseni kwa mtu huyu na utaratibu ufanyike wa kulipa fidia na yule mwekezaji au mchimbaji aweze kufanya kazi yake bila migogoro yoyote lakini mwekezaji anapoibuka kunakuwa na mgogoro mkubwa usio na lazima na unaosumbua watu wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, eneo la Dominiki ni eneo ambalo linazalisha sana vitunguu, mwekezaji alivyofika akaanza kubomoa mashamba ya vitunguu, watu wakawa wanalinganisha gypsum na vitunguu maana vitunguu ndiyo maisha yao ya kila siku, kwa hiyo ni jambo ambalo ilitakiwa liangaliwe kwa undani ili tuweze kuona kwamba suala hilo litafanyika vipi kwa uzuri wake. Jambo hilo lilikuwa linaendelea na sasa hivi mambo yanakwenda yanatulia lakini tunachosema ni kwamba hawa Maafisa Madini wasilete migogoro isiyokuwa na sababu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala zima la reserve ya madini iliyopo nchini. Tunatambua kwamba kuna madini nchini na tunatambua kwamba kuna GST ni muhimu GST ikapewa pesa za kufanyia utafiti kujua reserve iliyopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema hivi kwa sababu tumeona katika baadhi ya maeneo tunategemea takwimu za wawekezaji kujua available resource iliyoko hapo, sisi hatuwezi kufanya projection, mgodi huu utafanya kazi kwa muda gani na tunatarajia kupata kiasi gani. Tunapopata hizo takwimu lazima ziwe proved na GST, kwa hiyo GST akipewa pesa za kufanya utafiti itakuwa ni jambo jema. Pia apewe na vifaa vya kisasa vya kufanyia ili waweze kwenda na teknolojia. Kwa kufanya hivyo, nchi itanufaika na ile sera ya Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ya kutaka rasilimali zetu ziweze kulindwa na Sheria mpya ya Madini itakuwa na manufaa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri utafiti wa maeneo gani yenye madini ufanyike Tanzania nzima na hasa katika maeneo ambako Serikali ina ubia kupitia STAMICO. Hilo ni jambo muhimu sana ambalo inabidi tuliangalie, yapo maeneo kama Mwadui, TANGOLD, Buzwagi, maeneo kama hayo yakifanyiwa utafiti tukajua rasilimali iliyopo hapo itakuwa ni jambo jema sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hilo hilo tunao Maafisa Madini ambao wanafanya kazi kwa niaba ya Serikali. Ni wakati muafaka sasa kupitia Wizara lakini Tume ya Madini chini ya Prof. Mruma na mwenzake tuweze kuangalia suala la integrity, watu wanaopelekwa kule integrity yao iko vipi. Kwa sababu ukipeleka mtu ambaye anaweza ku- compromise ina maana rasilimali zetu zitakuwa zinapotea pasipo sababu yoyote. Tunatambua kwamba madini thamani yake ni kubwa, mtu aki-compromise pale anaweza kuwa anapata kitu kidogo lakini kwake yeye ni kikubwa kulingana na thamani lakini anakuwa analiumiza Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni ajira za wazalendo. Ni lazima tuangalie mgawanyo wa ajira kama zimekaa sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni Board Members. Je, Board Members walioko huko wana uwezo wa kutafsiri, wanajua wanachokifanya au tunawapeleka tu bila kuangalia uwezo wao? Kwa sababu kuna maeneo mengine professionalism inawapiga kando, unakuta wanakwenda kwenye bodi wakikaa wanakunywa chai wakitoka hapo wanapitisha wanakwenda. Kwa hiyo, suala zima la usimamizi linatakiwa liangaliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kuhusu STAMICO, kwa heshima kabisa na taadhima STAMICO wamekuwa wanatuangusha sana. Ni wakati muafaka Mheshimiwa Waziri na Wizara waangalie kwamba kuna nini huko STAMICO ili waweze kufanya kazi ambayo ilikusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kuchangia ni suala zima la wachimbaji wadogowadogo, mikopo ya vifaa imekuwa ikitolewa, lakini bado manung’uniko yapo. Ukiona kuna manung’uniko maana yake utaratibu hauko wazi au hauko vizuri, unaweza ukakuta misaada hiyo inakwenda kwenye baadhi ya maeneo tu. Kwa hiyo, ni vizuri ikafanyika sensa wachimbaji wadogowadogo wakajulikana na mahitaji yao yakajulikana na kinachopatikana kikawekwa kwenye mgawanyo mzuri sasa kwamba tunapeleka huku na huku na huku. Hili ni jambo la fairness pia ni la ku-promote hao wachimbaji wadogo wadogo kwa sababu baadaye nao wanakuwa wakubwa pia wana mchango mkubwa katika Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Maafisa Madini tunaomba wapatikane kwa urahisi katika maeneo yetu. Ziko Wizara zingine ambao Maafisa wao wanapatikana kwa urahisi lakini bado Maafisa Madini hawapatikani kwa urahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kabisa, yuko mchangiaji amezungumza suala la magari makubwa kuja kuchukua madini. Kwa mfano, gypsum Dominiki malori yamekuwa yanakuja semi trailers yanabeba hayo madini, lakini tunapata ushuru mdogo sana kama Halmashauri madaraja yamevunjika na barabara zimeharibika anayezikarabati ni nani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo muhimu sana tukaangalie ile compensation ambapo wananchi wa maeneo hayo waliothirika wanaweza wakapata kukawa na balance, kwamba madini yakachimbwa lakini barabara na madaraja yakatunzwa. Kwa sababu hatuwezi kushabikia uchimbaji wa madini wakati kuna uharibifu mwingine ambao unatokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na hayo ya kusema, naunga mkono hoja lakini nampongeza Waziri na Naibu Mawaziri, tunaomba muendelee kuchapa kazi. Watu wanasema mbele kwa mbele hakuna kurudi nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.