Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini

Hon. Deogratias Francis Ngalawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ludewa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini

MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuchangia Wizara hii muhimu ya Madini. Kwanza kabisa, nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Dada yangu Angellah na marafiki zangu, Waheshimiwa Stanslaus Nyongo na Doto Biteko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja kwenye dira ya Wizara hii ya Madini. Ukiangalia dira ya Wizara inasema ni kuwa Wizara inayoheshimika Afrika katika kuendeleza rasilimali za madini ili ziweze kuchangia kwa ufanisi katika uchumi wa Taifa, niishie hapo. Mimi natoka Ludewa, kule kuna chuma ambayo naamini ni madini na kuna makaa ya mawe ambayo naamini kuwa ni madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukijaribu kuangalia kile chuma cha Liganga naona hakuna link kati ya Wizara ya Viwanda na Wizara ya Madini. Ndiyo maana unaweza ukaona hata kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri hajagusia kabisa chuma cha Liganga. Pamoja na kuwa kwamba huu ni mradi kielelezo ambapo tuna imani kwamba katika programu yetu ya miaka mitano ipo na katika programu ya mwaka moja moja ipo, naamini hapa kuna shida ya kutokuwa na link nzuri ya kuona kwamba hiki chuma kinaweza kuisaidia nchi kwenda. Kwa sababu ya ile dira ambayo sasa tumeshaizungumza naamini kabisa tunge-link haya madini na tukapata ule mwelekeo ambao ni sahihi chuma hiki cha Liganga kingeweza kupewa kipaumbele na kuleta tija kubwa sana kwa maslahi ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunazungumzia miundombinu ya reli na majengo mbalimbali, ukijaribu kuangalia soko la ndani tu peke yake hiki chuma cha Liganga kinaweza kuleta tija kubwa. Kwa hiyo, napenda tu kuwepo na link kati ya Wizara hizi mbili badala tu ya kusema kwamba hii imeenda moja kwa moja kwenye Wizara ya Biashara. Ni kweli chuma ni biashara, ni kweli chuma ni uwekezaji lakini chuma ni madini. Kwa hiyo, at least Mheshimiwa Waziri angeweza kukiongelea tuone ni namna gani kinaweza kushughulikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho napenda kukizungumzia ni juu ya suala la makaa ya mawe. Tumeona hapa makaa ya mawe yamezungumzwa Kiwira na Ngaka. Tunayo makaa ya mawe Mchuchuma, licha ya ule Mradi wa Makaa ya Mawe Mchuchuma kwa maana ya kuzalisha umeme, bado kuna eneo kubwa la Ludewa linayo makaa ya mawe. Je, Serikali imefanya utaratibu gani kwa sababu Ketewaka tunayo makaa ya mawe mengi sana. Maeneo yale yote ya Mwambalasi kuna makaa ya mawe mengi sana, lakini sioni kama Wizara imeshajielekeza kuona licha ya ule mkaa wa mawe ambao unaweza ukazalisha umeme pale Mchuchuma kuna sehemu nyingine ambazo vilevile zingeweza kutumika na kama ambavyo Ngaka wanauza bado na maeneo mengi ya Ludewa yangeweza kuchimbwa huo mkaa na ukauzwa na ukaleta tija. Tija kwa maana ya wananchi ajira na kwa maana ya Serikali kupata kodi. Kwa hiyo, nadhani GST iendelee kufanya kazi yake nzuri na tuweze kuainisha kwa kiasi kikubwa tuna mkaa kiasi gani maeneo yale kwa ajili ya faida ya wananchi wetu na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao hawa wachimbaji wadogo. Serikali imechukua hatua, niipongeze kwa ajili ya kuwapa mikopo lakini wachimbaji wadogo wanaopata mikopo ni wachache. Kwa hiyo, naamini kwamba tungeweka utaratibu mzuri wa kuwapa elimu hawa wachimbaji wadogo ili waweze kukopa hata kwenye mabenki badala ya kusubiria ruzuku kutoka Serikalini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini tunao wachimbaji wadogo sana, Ludewa yapo machimbo sehemu za Amani kule, Kata ya Mundindi wapo wachimbaji wadogo wengi lakini hawajui nini wafanye. Wale watu hawana elimu ya kutosha, nadhani sasa Serikali ifike wakati ipeleke elimu ya kutosha kwa wale wachimbaji ili ikiwezekana sasa wajue namna gani ya kuendesha biashara, namna gani ya kutunza kumbukumbu, namna gani wanaweza wakakopeshwa na mwisho wa siku waweze kuendeleza biashara in sustainable way.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo suala la tanzanite. Tanzanite inapatikana Tanzania tu lakini ukienda kwenye soko la nje madini yaliyopo kule ni mengi zaidi na yanapelekwa na nchi ambayo siyo Tanzania. Nakumbuka mwaka jana tuliongelea hapa juu ya certificate of origin, kwamba mtu yeyote ambaye anaweza akasafirisha yale madini awe na certificate ambayo inatoka kwenye nchi husika. Sijajua Wizara mpaka sasa imeshafikia wapi katika kuhakikisha kwamba haya madini yanapokuwa yanauzwa kule ili isionekane kwamba hawa watu wametorosha au wamefanya biashara haramu, kuwepo na certificate maalum ya kuonesha kwamba madini haya yametoka Tanzania. Kwa kufanya hivyo, maana yake tutapunguza sasa ile watu kutorosha madini kupitia kwenye mipaka na maeneo mbalimbali tuweze kupata ile faida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali kwa kujenga ule ukuta. Pia nimshukuru Mheshimiwa Rais, Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Mkuu wa Mkoa wa Arusha na pia DC wa Simanjiro Bwana Chaula kwa kufanya usimamizi mzuri na kuhakikisha kwamba ule ukuta umekamilika na pia niishukuru Wizara kwa ujumla wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tuna suala hili la GST. GST imepewa majukumu makubwa sana ya kufanya tafiti za madini kwa nchi lakini ukijaribu kuangalia bajeti ambayo wanawekewa ni ndogo sana. Kwa hiyo, kila mmoja hapa na katika Wilaya na Jimbo lake wanahitaji kuona kwamba ni madini kiasi gani yapo na namna gani tunaweza tukayatumia wananchi waweze kunufaika na madini hayo, lakini bajeti wanayopewa GST hailingani na haitoshelezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine naamini kabisa tunao wataalam pale GST lakini ni wachache. Serikali ichukue sasa hatua kuelimisha wataalam wetu wawe wengi ili mwisho wa siku tuweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni juu ya gharama za tafiti. Watu wengi sana wameshika haya maeneo na wana leseni lakini gharama zile zinakuwa ni kubwa kwa maana GST iko centred sehemu moja. Kwa hiyo, kila mmoja anayetaka kuja kuitumia GST kwa ajili ya kumfanyia tafiti maana yake ni asafiri kutoka aliko aje Dodoma. Sasa wananchi wetu hawana uwezo mkubwa kiasi hicho. Naamini kwamba wangeweka utaratibu ambapo accessibility yake iwe ni jirani ili hiki chombo kiweze kutumika kwa unafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri tu-create awareness kwa wananchi wajue hizi shughuli, kwa sababu GST iko Dodoma na naamini wengi wenye machimbo haya hawaijui GST, wala hawajui GST maana yake nini. Kwa hiyo, yawepo matangazo ya kutosha, tu-create awareness ya kutosha ili wananchi wetu waweze kujua kazi ambazo zinafanywa na GST na wakati mwingine kuepukana na matapeli ambao wanawazunguka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la uwekezaji, tumekuwa na wawekezaji wengi sana wageni na inafikia mahali sasa kile kitu ambacho kinafanyiwa tafiti kule Serikali iko unaware. Kwa hiyo, ifike mahali sasa hawa wageni wanapokuja kufanya tafiti kuwepo na element ya Serikali ili kuweza kujua ni madini kiasi gani, kwa sababu unaweza ukapelekewa ripoti ambayo si sahihi, ripoti ambayo hailingani pengine na hali halisi iliyopo na hii naamini kwamba imeligharimu sana Taifa huko tulikotoka. Kwa hiyo, tukifanya utaratibu huo tutaona tija ya madini yetu na hawa wanaofanya tafiti hasa mashirika ya kigeni lazima yaweze kusimamiwa na tujue ni nini ambacho kinafanyiwa tafiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni juu ya utoaji wa leseni. Mara nyingi unakuta kwamba mtu ambaye madini yapo kwenye eneo lake hajui kama pana madini lakini unaambiwa kwamba eneo hili tayari lina mtu na tayari ana leseni, Serikali ya Kijiji na Wilaya hazijui, nadhani tuweke utaratibu sasa iliā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.