Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini

Hon. Eng. Joel Makanyaga Mwaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chilonwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini

MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nashukuru sana kupata nafasi hii leo kuwa mmoja kati ya wachangiaji katika hotuba ya Waziri wa Madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Joseph Pombe Magufuli pamoja na Serikali yake yote, kwa namna wanavyofanya kazi kwa umakini mkubwa sana unaotuletea Taifa manufaa makubwa sana ambayo sote tunayaona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue pia nafasi hii kumpongeza sana Waziri wa Wizara hii pamoja na Naibu Mawaziri wake wote wawili kwa kazi kubwa wanayoifanya ambayo sote tunaiona. Kipekee kabisa nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa namna alivyoiwasilisha hotuba hii hapa leo asubuhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii sasa niseme kwamba toka Serikali ya Awamu ya Tano imeingia madarakani tumeona hatua kadha wa kadha zinazochukuliwa ambazo zinalenga kuboresha maslahi ya nchi hii. Tumeona hatua madhubuti zilizokwisha kuchukuliwa mpaka sasa zinazoihusu Wizara hii ya Madini, mojawapo ikiwa ni suala la makinikia, kazi kubwa imefanyika, sisi sote tuna masikio tulisikia, tuna macho tuliona, tunaona jinsi gani mambo yanavyokwenda sasa ukilinganisha na hapo awali kuhusiana na suala zima la makinikia na mapato ya Serikali kupitia jambo hili la makinikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona pia hatua ya ujenzi wa ukuta kuzunguka machimbo ya tanzanite kule Mererani. Kwa hakika mambo haya pamoja na mengine mengi yameongeza kwa kiasi kikubwa sana mapato ya Wizara hii katika uchumi na ujenzi wa Taifa hili la Tanzania. Tunawashukuru sana na kuwapongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa Dodoma kama inavyooneshwa kwenye kitabu hiki tulichogawiwa cha Wakala wa Jiolojia Tanzania kuhusiana na madini yanayopatikana Tanzania, Dodoma pia ipo kwenye orodha na ina madini mengi sana. Dodoma hakuna wilaya ambayo haina madini, kila wilaya ina madini yasiyopungua mawili, matatu ambayo yanapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile sasa Wizara zote ziko Dodoma ikiwepo na yake, naomba waangalie ni namna gani madini haya ikiwemo madini nikel, dhahabu na chrysoprase ambayo yanachimbwa kwa wingi sana katika Wilaya ya Chamwino na hasa katika Jimbo langu la Chilonwa yataweza kunufaisha wananchi wetu. Halmashauri hatuna tunachopata kwa maana ya service levy na corporate responsibilities hatuzioni katika maeneo yetu ambako madini haya yanachimbwa. Kwa hiyo, kwa wao kuwa hapa Dodoma hebu wasaidie Halmashauri zetu ziweze kuwa miongoni mwa Halmashauri zinazofaidi machimbo haya yaliyopo hapa Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuangalia hiki kitabu niseme tu sijaelewa sana ni kwa nini, kuna madini yanaitwa dhahabu nyeusi (black gold) na najua anafahamu, haya ni mawe. Mawe haya kulingana na wachimbaji kwa jinsi tulivyokaa na kuongea nao wanachimba kule Kibaha pia lakini wakilinganisha na hapa Dodoma madini hayo wanayachimba kule Itiso, madini ya hapa yana ubora wa hali juu sana, siyaoni kwenye hiki kitabu. Tulivyokwenda kutembelea kule madini haya ya black gold yanatumika kwa sehemu kubwa sana kutengeneza marumaru yenye ubora wa hali ya juu sana na zote zinauzwa nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Serikali kuhamia Dodoma kwamba sasa ujenzi mwingi unafanyika hapa Dodoma, hebu nilete rai kwa Waziri, waangalie namna gani wanavyoweza kuhakikisha marumaru zinazopatikana Itiso zinakuwa sehemu kubwa ya ujenzi ya majengo yanayojengwa hapa Dodoma kwa kipindi hiki ili angalau kama Serikali tuweze kuwa na sehemu ya kufanya mchakato wa yale mawe na kupata final product tu-generate ajira kwa ajili ya vijana wetu pia na kipato kwa ajili ya wananchi wetu. Naomba sana Mheshimiwa Waziri akiona inafaa pamoja na Naibu Mawaziri, mmojawapo baada ya bajeti hii hebu tukatembee huko mkajionee wenyewe kwa macho ni nini kinachoendelea kule na ni namna gani kwa ukaribu zaidi mnaweza mkasaidia kuhakikisha kwamba Halmashauri zetu zinaweza kunufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, niseme kwamba naunga mkono hoja. Ahsante sana.