Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Mendard Lutengano Kigola

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia Wizara hii muhimu sana. Kwanza kabisa nianze na pongezi kwa Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri, tumeona kazi nzuri, kila mtu anajua kazi inafanyika vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mchango wangu una mambo machache tu. Jambo la kwanza, Mheshimiwa Waziri, tungeomba kujua vizuri masuala ya ardhi. Tukiangalia kuna Maliasili, kuna Wizara ya Ardhi, kuna sehemu fulani kama tunaingiliana. Kwa mfano sasa hivi ukiangalia kuna migogoro ya ardhi ambayo inajitokeza, watu wa Maliasili wanasema maeneo yale ni yao, tena ukienda Ardhi wanaweza wakasema yale maeneo ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna mgongano kidogo pale. Ukiangalia watu wa Maliasili wenyewe wanaangalia vipimo vya miaka ya 1976. Ukiangalia population ya mwaka 1976 tulikuwa Watanzania wachache sana, tulikuwa kama milioni nane, sasa hivi Watanzania tuko milioni hamsini na nane na kila kijiji ukiangalia sehemu kubwa imechukuliwa na watu wa Maliasili. Wananchi sasa hivi hawana ardhi hata ya kufugia au kulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mimi kwenye jimbo langu, Jimbo la Mufindi Kusini, watu wa Maliasili walichukua maeneo makubwa sana na sehemu nyingine zilichukuliwa na wawekezaji, kwa mfano wakulima wa chai walichukua maeneo makubwa sana. Mfano, ukienda pale Kijiji ha Mtwango wananchi wamekaa tu kwenye barabara ni sehemu ndogo sana, hata kufanya sehemu za kilimo hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile ukienda Kijiji cha Sawala kile wananchi hata kwa kujenga makazi hakuna. Hata tukisema tukafanye upimaji wa ardhi kwa ajili ya wananchi tutashindwa. Sehemu kubwa imechukuliwa na watu wa maliasili. Naomba sasa unapotupa maelekezo masuala ya ardhi tupate ufafanuzi kwamba, Maliasili ana uwezo wa kujipimia ardhi au ardhi inapimwa na watu wa Ardhi? Hii itatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, nimesikia kuna upimaji kule wanafanya vizuri sana, Wilaya ya Kilombero, kuna program nzuri sana. Ile program nimeipenda na inaenda kwa bei nafuu sana, nadhani wanatumia simu tu kwa bei nafuu, kuna wafadhili nadhani, Waziri anaijua, ile program ingekuja Tanzania nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri kama anakuja wilaya nyingine namwomba kwenye Wilaya ya Mufindi basi aje apime. Kwa sababu sisi kule, kama nilivyoongea mara ya kwanza kwamba, wawekezaji wengi sana na sasa hivi tuna tatizo kubwa sana la ardhi. Kwa hiyo, tukija kupimiwa matumizi bora ya ardhi, halafu nasikia wanatoa hati bure, ile itatusaidia sana. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri angalau atuangalie Wilaya ya Mufindi kwa ile program na sisi ije kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine kuna upanuzi wa ilikuwa vijiji, sasa hivi imekuwa miji tayari, tunaita miji midogo. Kwa mfano pale Igoole, Nyololo, Mninga na Kasanga, ile ni miji midogo, lakini kuna upimaji ulifanyika pale. Upimaji ule nadhani watu wa halmashauri walisema wapime, ni upimaji mzuri si mbaya, lakini ukipima makusanyo yote yanaenda kwa halmashauri, hiyo ni njia nzuri na ile fedha tunajua ni Basket Fund, halmashauri inagawanya katika wilaya nzima, lakini kijiji husika ambacho kimetoa ardhi hakipewi mgawo mkubwa, kinaweza kikapewa mgawo mdogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, kijiji husika basi kipewe percent kubwa, ili waweze kufanya maendeleo makubwa kwa sababu wale ndio waliotoa ardhi pale. Hii itakuwa imesaidia sana kuondoa migogoro ya ardhi ndani ya vijiji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, tuna mgogoro pale kati ya mpaka wa Makambako na Mufindi. Kuna Kijiji kimoja pale Nyigo tunapakana na Makambako. Ukiangalia Serikali ilipatia Kijiji cha Nyigo, mipaka iko Kijiji cha Nyigo lakini wa Makambako na wenyewe wanasema ni sehemu yao, ule mgogoro ndio sasa unakuwa mkubwa. Naomba Wizara iingilie kati hilo suala la mgogoro wa ardhi ni mkubwa sana na unapanuka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mwekezaji alitaka kuwekeza pale, lakini bado wananchi pale hawaelewi. Mheshimiwa Waziri nadhani ameiandika imekaa vizuri, lakini wananchi pale hawajui, kwa hiyo wangeenda pale wakawaelimisha wananchi itakuwa imetusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine napongeza ugawaji wa viwanja, wamegawa viwanja vizuri, hata hapa Dodoma wametugawia viwanja vingi sana vya kununua. Hata hivyo mtu ukisema square metre moja Sh.6,000/= au Sh.12,000/=, bado hujawasaidia wananchi. Naishauri Serikali waweke bei nafuu, ila labda waweke masharti ya kujenga kwamba, wajenge nyumba ambayo ni reasonable, inaonekana ni nyumba, lakini viwanja wakiuza kwa bei kubwa, kwa mfano, sasa hivi watu wametoka Dar-es- Salaam, wametoka wapi, wamekuja wafanyakazi wamesema hapa ndio makao makuu wajenge nyumba, wanahangaika wanapanga huku na huku nyumba hazieleweki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tusipunguze bei ya viwanja ili watu wajenge nyumba nzuri? Tukisema square metre moja Sh.12,000/= au Sh.6,000/=, mtu kusema anunue kiwanja sasa hivi milioni kumi, milioni ishirini, milioni thelathini, anunue kiwanja kwa hali ya sasa hivi nani atanunua? Itakuwa bado. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi napendekeza. Kwa sababu, sisi ndio tunaishauri Serikali, vile viwanja kwa square metre moja hata ukifanya Sh.3,000/= kwa square metre moja, mtu akanunua kwa milioni mbili ama milioni tatu kwa kiwanja itakuwa ni reasonable; lakini ukisema milioni kumi na ngapi huko itakuwa ni ngumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hati miliki. Zile hati miliki ni nzuri sana; kwa mfano kwenye jimbo langu, walipima kwa ajili ya hati miliki, lakini bado wananchi ile hati miliki hawaelewi kama anaweza akakopea mkopo benki, bado haijakaa vizuri. Kama tumetoa hati miliki zile za kimila, mimi nazungumzia zile za kimila, naomba kama mtu ameshapewa basi itambulike benki. Akiweza kukopea maana mwananchi yule inamfaidisha ardhi yake, akafanya maendeleo makubwa, hii itakuwa imemsaidia sana mkulima na yule mwenye ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, migogoro ya ardhi kwa wakulima na wafugaji. Nadhani hili suala siku moja tuseme sasa mwisho hakuna migogoro tena na ili kulimaliza vizuri lazima elimu ipite vizuri. Mkulima akielimishwa na mfugaji akielimishwa watu hawatauana, lakini elimu bado. Kwa mfano, zamani unaweza ukaona mtu analima pia ni mfugaji lakini walikuwa hawagombani, lakini sasa hivi ardhi ya wakulima na wafugaji imekuwa ni mgogoro mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaiomba Serikali, nadhani Mheshimiwa Waziri wetu yuko vizuri, wakishauriana vizuri na labda na huyu Waziri wa Ulinzi na wengine wanaohusika katika Wizara nyingine tutakuwa tumefikia mahali pazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu ni huo.

Naunga mkono hoja, ahsante sana.