Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Maulid Said Abdallah Mtulia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunijalia mimi pamoja na Wabunge wenzangu kukutana mahali hapa leo na kupata fursa ya kuchangia Wizara hii ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Sambamba na hilo nitumie fursa hii kuwatakia watu wa Jimbo langu la Kinondoni, Ramadhan Mubarak na Watanzania kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli, niseme wazi naipongeza sana Wizara hii ya Ardhi kwa kazi kubwa wanayofanya. Nimtaje kwa jina mzee wangu Mheshimiwa Lukuvi na Naibu wake, wanafanya kazi kubwa. Kwetu sisi Kinondoni hakuna asiyefahamu kwamba tulikuwa na migogoro mingi sana ya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Naibu Waziri alikuja pale tukaenda mpaka katika maktaba yetu ile ya ardhi tukaangalia pamoja, tukaona namna gani baadhi ya watendaji wetu wanavyokiuka utaratibu katika kutafuta namna ya kuwadhulumu wanyonge wenye ardhi yao na badala yake kuwapa umiliki huo matajiri. Kwa kweli, wamefanya kazi kubwa sana, tunawashukuru sana mwendelee kuchapa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi leo najikita kwenye jambo moja tu. Jambo langu, kama mnavyojua, Jimbo langu la Kinondoni ni Jimbo ambalo lina kata 10 na kati ya kata hizo 10, kata tisa zote zimepitiwa na mabonde na wananchi wangu katika hizo kata tisa wote wanaishi katika maeneo yasiyokuwa rasmi. Kwa hiyo, unapozungumzia suala la urasimishaji, suala la uendelezaji wa miji, suala la upangaji miji na wakati mwingine hata suala la kuleta bomoabomoa kwa ajili ya kutengeneza mji mimi ni mhanga na wananchi wangu ni wahanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nitajikita sana hapa na kuiomba Serikali iangalie namna gani inaweza ikatusaidia sisi watu wa Kinondoni na Dar es Salaam kwa ujumla ambao mji wetu maeneo mengi watu walienda kama ni mashamba, lakini leo ni mji na yamepangwa katika mpango usiokuwa bora, tunafanyaje kuboresha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia katika kitabu cha Mheshimiwa Waziri na nimevutiwa na maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia ukurasa wa 38 Mheshimiwa Waziri anazungumzia Mpango Kabambe wa Utekelezaji wa Miji na katika mpango huo kabambe amelitaja Jiji letu la Dar-es-Salaam. Kwa hiyo, tuna mategemeo makubwa sana watu wa Dar-es-Salaam tutanufaika katika mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda katika ukurasa wa 41 ameanzia ukurasa wa 40 ameendeleza urasimishaji wa makazi holela Jijini Dar-es-Salaam. Kama mnavyoelewa, kama nilivyotangulia kusema katika Jimbo langu la Kinondoni hayo makazi holela yapo. Kwa hiyo, kwa kweli, nina mategemeo makubwa sana kutoka kwa Mheshimiwa Waziri kuhusiana na jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda tena ukurasa wa 47, Mheshimiwa Waziri ameelezea maendeleo ya sekta ya nyumba na hapa napenda kunukuu; Mheshimiwa Waziri anasema:-

“Wizara yangu ina jukumu la kuratibu uendelezaji wa sekta ya nyumba nchini, sekta hii huchangia kukuza uchumi, kuongeza fursa za ajira na kupunguza umaskini. Kwa kuzingatia hayo Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi, ili kuvutia uwekezaji katika sekta hii na kuwezesha wananchi kumudu gharama za nyumba zilizo bora.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimevutiwa hapa katika Serikali kuwezesha wawekezaji kuja nchini. Sisi watu wa Dar es Salaam, tena hili niseme kwamba naungana na Mheshimiwa Waziri kabisa, tunashirikiana katika Mto wetu Msimbazi. Tunaathirika vile vile katika Mto Msimbazi, lakini vile vile tumeathirika katika Mto Ng’ombe, Mto Kibangu, mito mingi. Jambo hili limesababisha wananchi wangu kuishi katika maeneo ya mito na hata kuvunjiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipokuwa kwenye kampeni tulizungumzia Dar es Salaam mpya. Namwomba Mheshimiwa Waziri aje na mkakati sasa kwa sababu, tukisema kila anayekaa bondeni tumvunjie, katika jimbo langu tutavunja asilimia 60 ya nyumba zote zilizokuwa katika Jimbo la Kinondoni. Kama nilivyotangulia kueleza kata tisa zote zina mabonde, tukiamua kwenda kuvunja nyumba maana yake zaidi ya asilimia 60 ya nyumba zote tutakuwa tunavunja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Mheshimiwa Waziri anazungumzia kutengeneza mazingira mazuri ya wawekezaji kuingia; Mheshimiwa Waziri ana mpango gani wa kuhakikisha tunarasimisha makazi haya ya Jimbo la Kinondoni, ili Kinondoni ile ya kisasa tuliyokuwa tumeihubiri katika kampeni ipatikane?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wananchi nimezungumza nao, wako tayari kutoa maeneo yao kama atapatikana mwekezaji kwa ajili ya kushirikiana. Wao wanatoa maeneo mwekezaji anajenga nyumba za kisasa, ili tuondoe kabisa squatter katika Jimbo langu la Kinondoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na vile vile tumeambiwa katika Mto Msimbazi kama kuna mtu, kuna mtu kajitokeza anataka kuwalipa fidia wale watu wanaokaa mabondeni, ili yeye alitumie jengo lile kwa ajili ya maendeleo. Sasa Waziri anatuambia nini kuhusu kuwapa fursa hawa wawekezaji? Kwa sababu, sisi kama Serikali tukiamua tufanye sisi, maana yake itabidi tukakope hela benki, lakini mwekezaji ameamua aje kuwekeza kwa gharama zake mwenyewe; Serikali ina mpango gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itambue kwamba, Jiji la Dar-es-Salaam lina zaidi ya watu milioni sita, lakini watu hawa wanataabika kwa mifereji ya Mto Msimbazi ambayo Serikali inapaswa kujenga miundombinu wezeshi, miundombinu ambayo itafanya Dar-es-Salaam iwe ya kisasa. Angalia juzi pale imenyesha mvua Jangwani, jiji lote limesimama; hivi kweli, tunasimamisha jiji kwa mradi ule Mto Msimbazi? Hivi kweli Mto Msimbazi hautibiki? Inafika mahali Dar-es-Salaam inasimama kwa Mto Msimbazi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri aje na maelezo ya kutosha namna gani Dar-es-Salaam yetu mpya tunaijenga na hasa wananchi wako tayari kutoa maeneo yao kushiriki…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mto Msimbazi kama kuna watu wanajitokeza kuwekeza na Serikali ikajiweka mbali wakalipwa fidia wananchi wetu hili jambo litakuwa lina manufaa kwa wananchi na lina manufaa Serikali.

Nakushukuru na naunga mkono hoja.