Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Emmanuel Adamson Mwakasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuchangia kwenye hii Wizara muhimu na nyeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabla ya mchango wangu nianze kuipongeza hii Wizara kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya. Wizara ya Ardhi kwa kweli kuna changamoto nyingi, lakini Mheshimiwa Lukuvi na Mheshimiwa Mabula wanafanya kazi nzuri, nawapongeza sana. Hamuiangushi Serikali ya Awamu ya Tano. Pamoja na pongezi hizo, naomba niende kwenye changamoto moja kwa moja ambazo zimekuwa zikiikabili Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya ardhi kwakweli imekuwa ni mingi. Pamoja na kwamba mingine inapungua lakini mingine imekuwa ni ya kawaida. Kwa mfano, tunapoongelea suala la watu kupewa ardhi, watu wawili au watatu au wateja wawili au watatu yaani (double allocation) hili jambo ni la muda mrefu, lakini wanaosababisha hivyo ni hao hao watendaji wetu wa ardhi ambao wameaminiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi wasiwasi au mashaka yangu ni zile hatua wanazochukuliwa hawa watendaji ambao wamekuwa wakisababisha hii Wizara kupata matatizo mengi sana hasa haya ya double allocation. Sioni kama ni sahihi kumuhamisha mtu baada ya kufanya matatizo sehemu fulani anapelekwa kwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona wangechukuliwa hatua ambazo zitawafanya hata wengine wasiwe na ile kwamba atafanya makosa kama hayo ya (double allocation) halafu anajua kabisa kwamba mimi hapa watakachofanya kama sio kuniteremsha cheo, watanihamishia sehemu nyingine. Hawa wachukuliwe hatua kali kwa maeneo waliyopo ili kuwapunguzia wananchi matatizo haya yanayojitokeza mara kwa mara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna suala hili la wenye uwezo. Wamekuwepo watu mbalimbali ambao wanavamia maeneo ya watu ambao hawana uwezo. Mtu anakwenda, anajenga eneo la mtu ambaye anajua hana uwezo kwa kutegemea kwamba; anasema huyu ataenda Mahakamani na akienda Mahakamani anajua yeye kwamba kwa uwezo wake aidha anaweza kukawiza kesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu kuna mahali inafika mtu anamdhulumu mzee ardhi halafu anaanza kumhesabia miaka. Mathalani, mtu ana miaka kama 60, mtu anasema muache tu aende Mahakamani, akienda Mahakamani huyu hata kabla kesi haijakwisha huyu atakuwa ameondoka. Sasa vitu vya namna hii vinafanyika, naomba Wizara waweze kuviangalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nije kwenye wangu wa Tabora na hasa Tabora Manispaa. Katika eneo hili, Mheshimiwa Lukuvi na Mheshimiwa MAbula, wamekuja Tabora mara nyingi, nawapongeza kwa hilo. Migogoro mingi ya ardhi iliyopo Tabora wanaifahamu, lakini ile migogoro mingi pia imesababishwa na watendaji wa ardhi pale Tabora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo naomba lifanyiwe uchunguzi, waporaji wengine wa ardhi ni miongoni mwetu, kwamba ni viongozi tena wengine ni viongozi wa chama ambao nadhani Mheshimiwa Lukuvi anakumbuka alipokuja Tabora hata Mheshimiwa Mabula walikumbana na kitu cha namna hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa nini basi isifike mahali Serikali ikaanza kufanya uhakiki kama kunavyofanyika uhakiki mwingine. Uhakiki wa wamiliki halali wa viwanja vile. Inawezekana na sioni ugumu kwa sababu kuwatambua watu ambao wamefoji viwanja vile ni kufanya uhakiki. Ningependekeza hicho kwamba ufanyike uhakiki wa maeneo yenye migogoro ili ionekane ni nani hasa wamiliki wa vile viwanja kwa sababu hili tatizo lipo nchi nzima. katika maeneo mbalimbali viongozi wanajitwalia ardhi kwa kutumia vyeo vyao lakini wanaandika majina tofauti tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati viwanja kwa mfano vinagaiwa tuseme kwenye halmashauri au manispaa viongozi wanajitwalia viwanja vingi tu. Mtu mmoja anaweza akachukua viwanja hata 30 kwa majina tofauti halafu baadaye anaanza kuviuza kidogo kidogo kwa bei kubwa ya kuwaumiza wananchi. Sasa kwa nini lisifanyike zoezi la uhakiki kuwabaini hawa ili vile viwanja vingine wanapobainika pamoja na hatua za kisheria kuchukuliwa kwa wao kufoji majina mbalimbali lakini pia kuwapa wale ambao hawana uwezo wa kumiliki hivyo viwanja?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kwa pale sisi Tabora Manispaa tuna bahati mbaya, kwa upande mwingine bahati nzuri kwamba tunazungukwa na majeshi lakini pia tunazungukwa na hifadhi. Kumekuwa na migogoro ya muda mrefu ya ardhi kati ya wananchi pamoja na wanajeshi, kwa maana ya mipaka ile ambayo kwa muda mrefu haijaoanishwa sawasawa, ni nani hasa ambaye anastahili kuwa na eneo lile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, wananchi wamekuwa wakilima muda mrefu, wale ambao wanapakana na maeneo ya majeshi, lakini hivi karibuni imetokea suala la jeshi kudai kwamba yale maeneo ni yao, ambayo wananchi wamekuwa wakilima zaidi ya miaka 40 pale. Sasa naiomba Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na Wizara ya Ulinzi, waweze kufanya haraka zoezi la kupata ramani zile ili kujua ni nani hasa ni mmiliki wa maeneo gani na kwa mipaka gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba hili suala la hifadhi, hifadhi wote tunazihitahiji, wote tunahitaji utalii, tunahitaji kutunza misitu, lakini kuna sehemu kubwa ambayo wananchi wanafanyiwa uonevu. Wako wananchi miaka na miaka kabla hata ya hayo maeneo ya hifadhi hayajatamkwa bayana. Leo hii wanaondolewa maeneo ambayo hawajua sasa watakwenda wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba pia Wizara hii kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii waweze kuona ni wapi wananchi wale sasa haki yao ipo. Nadhani baada ya haya machache ambayo yanajitokeza kwenye suala hili, kama yakifanyiwa kazi nadhani tutaweza kuwa tume-solve hili suala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya machache, naunga mkono hoja.