Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019

Hon. Azza Hilal Hamad

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019

MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyenijalia pumzi na uzima na hatimaye kuweza kuchangia hotuba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, niipongeze Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi kubwa ambayo inaifanya hususani katika usambazaji wa maji ingawa kuna kasoro ndogo ndogo ambazo zipo katika usambazaji wa maji. Naamini Waziri,

Naibu Waziri na watendaji kwa sababu wako hapa watajipanga kuona wanatatuaje changamoto hizo zilizopo hususani katika Mkoa wa Shinyanga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nianze na mradi mkubwa wa maji ya Ziwa Victoria ambao ulianza Mkoa wa Shinyanga kwa mwaka 2014. Kulikuwa na utaratibu wa vijiji vilivyopo ndani ya kilometa 12 kupatiwa maji, hiyo ni toka mwaka 2014, lakini mpaka hivi tunavyoongea imekuja awamu nyingine ya usambazaji wa maji ya Ziwa Victoria kuna vijiji ambavyo havijapata maji. Naomba nitaje baadhi ya vijiji hivyo, vijiji vya Ntobo, Nyamigege, Kula, Buchambaga, Busangi na vingine vingi ambako bomba la Ziwa Victoria limepita kwa mara ya kwanza. Niiombe Wizara ya Maji waangalie wanakwendaje kumaliza vijiji hivi vilivyopo ndani ya kilometa 12 kwa mradi wa awamu ya kwanza ya Ziwa Victoria ambavyo mpaka leo hii hawajapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiwa katika Mkoa wangu wa Shinyanga, naomba niizungumzie Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu. Mkoa wa Shinyanga mradi mkubwa wa maji ya Ziwa Victoria ndiyo unakwenda kupeleka maji Mkoa wa Tabora. Nasikitika kusema kwamba Halmashauri ya Ushetu haina kijiji hata kimoja ambacho kinapata maji ya mradi wa Ziwa Victoria. Ukiangalia Kahama Mji na Ushetu ni jirani sana na Ushetu imetokana na Kahama Mji inanipa taabu ni kwa nini Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu hamjaiweka kwenye mpango wa mradi wa maji ya Ziwa Victoria na ukiangalia Ushetu imezaliwa kutoka Kahama. Niiombe Wizara mjipange muangalie Halmashauri ya Ushetu wanawezaje kupata maji ya Mradi wa Ziwa Victoria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niingie katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu. Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu ina mradi mkubwa wa maji wa Ziwa Victoria ambao mpaka sasa hivi unatekelezwa na baadhi ya maeneo yanapata maji. Vijiji vinavyopata maji ni Kolandoto, Maganzo, Mwadui na Munze ambapo ni Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nimesema katika utekelezaji wa mradi huu, kuna matatizo ambayo yanajitokeza. Ukiangalia pia katika Halmashauri Wilaya ya Kishapu sehemu ambapo bomba kuu linapita kuna vijiji ambavyo viko ndani ya kilometa tatu mpaka tano yaani wanatizama bomba lakini hawana maji, haipendezi. Anawezaje mwananchi wa kawaida kuangalia yeye anahangaikia ndoo moja ya maji lakini bomba analitizima linapita kilometa tatu kutoka hapo yeye alipo? (Makofi)

Wizara ya Maji kaeni mjipange, haipendezi na kutakuwa na uharibifu tusipokuwa makini, mtu hawezi kupata shida ya maji wakati bomba analiona linapita kwenye eneo lake. Vijiji hivyo vilivyopo katika Halmashauri ya Kishapu ni Kijiji cha Songwa, Seseko, Nyenze, Kakola, Igaga, Lubaga, Uchunga na Mwadui Luhombo. Naomba Wizara ya Maji mjipange muone vijiji hivyo vinakwendaje kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sasa niingie katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ambayo mimi ndiyo naihudumu na ninakoishi. Nianze moja kwa moja na sehemu ninayotoka, msahau kwao ni mtumwa.

Mheshimiwa Spika, mwaka jana wakati wa bajeti nilisimama ndani ya ukumbi huu nikaipongeza Serikali na nikaishukuru Wizara ya maji kwa mradi mkubwa wa maji ambao kwa kitabu cha bajeti cha mwaka jana, ninacho hapa, ukiangalia ukurasa wa 70 kitabu cha mwaka jana mradi mkubwa wa Ziwa Victoria ulikuwa unasomeka kwa ajina la Solwa, Tinde, Nzega, Igunga, Uyui na Tabora. Nilisimama hapa na kuishukuru Serikali, lakini naomna kusema sijui Wizara wameepitiwa, Mheshimiwa Waziri na Naibu wako na watendaji wenu mpo hapa. Mimi naomba mnijibu, kitabu chenu cha mwaka huu cha bajeti jina la mradi limebadilika, mradi huu umeenda kuondoa jina la Tinde, Mheshimiwa Waziri naomba nipate majibu. Ni kwa nini jina la mradi limebadilika? Katika hotuba yako ya mwaka huu ukurasa wa 46 mradi unasomeka Solwa, Nzega, Uyui, Igunga na Tabora; Tinde tena haimo, kama mmepitiwa naomba muangalie.

Mheshimiwa Spika, ukizingatia Mheshimiwa Rais alisimama Tinde na akasema, mradi mkubwa wa maji unatoka Solwa, Tinde, Nzega na kwenda mpaka Tabora. Lakini nashangaa hotuba ya mwaka huu labda bajeti ya mwaka huu mmekwenda mradi wa maji wa Tinde. Ninaomba nipate majibu, Mheshimiwa Waziri tumeshasema sana na wewe, nimekufata mara nyingi, lakini kunyamaza si majibu, watendaji wako hapa naomba nipate majibu, wananchi wa Tinde wapate majibu, mradi wa maji wa Ziwa Victoria ni kwa nini mwaka huu wa fedha haupo katika mradi wenu ambao unasomeka? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiwa hapo hapo Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga naomba nisemee mradi wa maji tena mwingine wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ambao ni mradi wa Ziwa Victoria wa Kijiji cha Masengwa.

Mheshimiwa Spika, kuna fedha ambazo mradi huu ilikuwa imesha pata, lakini mradi huu unatoka Manipsaa ya Shinyanga na mradi huu ukifika katika kijiji cha Masengwa unaweza ukahudumia Kata zingine ambazo hazina maji. Ikiwemo Kata ya Samuye, Kata ya Usanda pamoja na Kata ya Mwamala. Kata hizi zinaweza kupata maji kupitia kijiji cha Masengwa.

Mheshimiwa Spika, na niseme mradi huu halmashauri yangu imesha andika barua nyingi Wizara ya Maji, kuanzia mwezi wa tatu mpaka hivi ninavyoongea Wizara ya Maji haijajibu. Kuna matatizo matatu ambayo yanaonekana yapo, Halmashauri imeomba Kibali cha kutumia maji ya SHUWASA kutokana na kwamba, Masengwa ipo nje na Manispaa ya Shinyanga, hivyo hawarushusiwi kutumia maji kwa sababu wao wapo vijijini. Halmashauri imeomba kibali Wizara ya Maji lakini mpaka hivi leo ninavyoongea kibali hakijapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kikwazo kingine cha pili, wizara haijatoa maelekezo ya namna ya usimamizi kutoka Wizara ya Maji kwenye Halmashauri husika, Halmashauri imeandika barua wameshapiga simu wamekuja wenyewe mpaka ofisini kwenu lakini majibu hayajapatikana mpaka sasa hivi.

Mheshimiwa Spika, kikwazo cha tatu katika mradi huu, vetting kutoka katika Mwanasheria Mkuu wa Serikali haijapata majibu Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga. Kwahiyo naiomba Wizara mtuambie, mradi huu wa Masengwa mna mpango nao gani? Kwa sababu mna utaratibu wenu wa matumizi ya fedha hizi za maji mna siku 21 sijui siku 35 siku hizi zikiisha manakwenda kuwanyang’anya Halmashauri fedha. Naomba majibu kwa nini wizara haitekelezi wala haijibu maandiko yanayoletwa na Halmashauri.

Nakushukuru naunga mkono hoja.