Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019

Hon. Ally Mohamed Keissy

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza kabisa namshukuru Waziri wa Maji, Mheshimiwa Engineer Kamwelwe, Naibu Waziri, Mheshimiwa Aweso kusema kweli baada ya kulalamika hapa Bungeni walifunga safari ingawa Nkasi ni mbali walifika mpaka Nkasi kuangalia jinsi miradi ya maji inavyoibiwa.

Mheshimiwa Spika, katika kuibiwa hii Wizara ndiyo inaibiwa, yaani hakuna sehemu tunaibiwa kama Wizara ya Maji. Mheshimiwa Aweso alijionea mwenyewe alivyofika Kirando, Mheshimiwa Engineer Kamwelwe alijionea mweyewe alivyofika Kabwe, wamejionea miradi ya kusadikika yaani ni miradi ya ajabu ajabu. Kabla ya wiki moja hajafika Mheshimiwa Kamwelwe pale tenki lilibomoka kidogo liue wanafunzi, yeye mwenyewe shahidi aliona. Alifika Mheshimiwa Aweso mwenyewe akasema hii miradi kusema ukweli wanapeana kijomba kijomba, kishangazi shangazi, hakuna kusema ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mradi wa Kamwanda - Kirando nitakusomea, mradi huu umeingiwa mkataba wenye gharama ya shilingi bilioni 7.7 na mkandarasi Wimbe, mkandarasi ni class five ambao uwezo wake ni shilingi milioni 750 lakini akapewa kijomba kijomba mara kumi zaidi. Maelezo ya Bodi ya Usajili wa Wakandarasi tarehe 4 Julai, 2017 yalieleza kuwa mkandarasi huyu hana sifa za kutekeleza mradi huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haikutosha, hata guarantee ya benki hakuweka, hana uwezo. Baraza la Madiwani Nkasi lilimkatalia, lakini baada ya kusimamisha mradi alikwenda kukopa mabomba Kahama akaleta mabomba Kirando, yaani ni wizi wa hali ya juu. Tukazuia shilingi milioni 800 na huyu mkandarasi nilizungumza hapa Awamu ya Nne, mkandarasi huyu ndiye alipewa shilingi milioni 210 kwa mradi wa maji Kamwanda, alikula hela hakuna chochote kilichofanyika, huyu mkandarasi. Tender yake haikutangazwa, siri, ni ujambazi wa hali ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huyu mkandarasi ni jambazi na miradi mingi ya Mkoa wa Rukwa huyu bwana kaingia haitoi maji. Nenda Matala mradi wa shilingi milioni 450 hakuna maji yaani miradi ya Nkasi utadhani ni Zaire kule Congo hawawezi kujua watu, lakini miradi yote ya Nkasi ni wizi, ni wizi, ni wizi hakuna hata mradi mmoja ambao unasema unatoa maji. (Makofi)

Mhesimiwa Spika, inasikitisha sana, Awamu ya Nne hapa imetoa shilingi bilioni 1 kwa ajili ya Bwawa la Mfili, alikwenda Naibu Waziri wa TAMISEMI, Ndugu yangu, shemeji yangu Kakunda kwenda kuangalia ule mradi thamani yake haifiki hata shilingi milioni 350 kwa ushahidi kabisa leo wanatoa shilingi milioni 300 kwenda kuweka mabomba, sijui kuweka mashine pale kwenye bwawa, bwawa lenyewe halina maji, amechimba kwa shilingi milioni 350, ni ujambazi wa hali ya juu. Hii Wizara kusema kweli inaibiwa hela zinatoka kule na zinarudi huku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, viongozi wakubwa ndiyo wenye miradi hii wanajulikana, kwa ushahidi wananitafuta mimi tuzungumze nao na mimi nawakatalia. Eti Mbunge nyamaza ili waibe zaidi, haiwezekani. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, Mradi wa Isale - Kate, mikataba hii hapa wamefutafuta, wameongeza shilingi milioni 24 haijulikani za nini. Wanaweka shilingi milioni 300 eti kuzuia maji tu pale ili kuja huku, shilingi milioni 300. Ndugu zangu kodi za wananchi tuzioneeni uchungu, hii ni kodi ya wananchi. Serikali haifyatui noti ni kodi za wananchi, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, walikwenda kujionea Mawaziri wenyewe, Engineer Kamwelwe alikwenda kuona kule Kabwe wameweka solar fake fake, betri fake fake tu alikwenda kuona mwenyewe, tenki kidogo liue wanafunzi alikwenda kuona mwenyewe. Mheshimiwa Aweso alifika mpaka Kirando, wakandarasi kawaambia. Sasa nataka kujua Mradi wa Kirando umesimama leo miezi sita na Mkurugenzi kasimamishwa kazi, natakakujua mradi wa Kamwanda utaanza lini kutoa maji? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumezuia wizi huu, ukipiga mahesabu zaidi ya shilingi bilioni tatu ilikuwa ziende mimi ndiyo nimezuia hii, nastahili sifa. Hata wakichunguza Mradi wa Isale - Kate kuna wizi. Miradi yote ya Rukwa ukichunguza ni wizi wa mabilioni ya hela. Ni kweli lazima Tume itumwe kila mradi wa maji uchunguzwe. Haiwezekani Rais anajitahidi kukusanya pesa Idara ya Maji ni kama mfereji, ndiyo maana ikaitwa Idara ya Maji, unatoa watu, unamwaga tu. Ndugu zangu tuwe na uchungu na nchi hii, hatuwezi kukubali kuibiwa namna hii. Maji ni uhai, Namanyere tunapata maji asilimia 16 leo mnasema maji vijijini sijui asilimia ngapi Namanyere maji yako wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilizungumza hapa mimi Mbunge nakaa siku tatu siogi, Namanyere kuna maji yako wapi? Asilimia 16 Namanyere maji hayatoki zaidi. Hakuna mradi umekamilika, hata kama mradi unatoa maji ukilinganisha na fedha mzee ni balaa tupu. Hata mimi sikusomea huo uinjinia, sikuoma mahesabu lakini huwezi kunidanyanya bei ya bomba inajulikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilizungumza hapa miaka iliyopita kweli nina uchungu nimemwambia na alikuja mpaka Waziri pale aliyetoka tukamwambia usilipe hizi hela, usilipe shilingi milioni 300 hizi kwa hili bwawa maana thamani yake haifiki shilingi milioni 900 lakini cha ajabu alilipa hela. Ndiyo maana Rais akipita sehemu anasema wakamateni wakandarasi, msaidieni Rais Ndugu zangu yuko peke yake, hebu muoneeni huruma. Haiwezekani mtu anachimba bwawa la shilingi milioni 300 mnamlipa shilingi milioni 900 na tulizuia! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, alikuwa Zumba na Zumba siku hizi ndiyo Naibu Katibu Mkuu hapa TAMISEMI, alikuwa kwenye bwawa na akasema huyu Mhandisi ondoka naye na hizi hela msilipe lakini walilipa. Zumba shahidi leo ni Naibu Katibu Mkuu, TAMISEMI, tusemeje sasa sisi? Mbunge anazuia, RAS anazuia, Mkurugenzi anazuia, DC anazuia lakini analipwa kijanja kijanja. Ndiyo maana tunasema huko Wizarani kuna mtiririko, kuna wizi, kuna ujambazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi sifichi, sili kwao, mimi nakula hela yangu ya halali hapa nawaambia ukweli kabisa anayechukia achukie, hizi kazi wanapeana kijamaa, kijomba kijomba. Mtu hana guarantee ya benki, hana chochote, anapata ile 15 percent ndiyo anakwenda kununua magari na mabomba. Leo mradi wa Isale umesimama, kapewa shilingi bilioni 1.1 kaenda kununua magari mawili, kaenda kununua mabomba, kaishiwa hela anataka certificate, hakuna chochote. Ndugu zangu tuangalie hii miradi ni nani anaichunguza mpaka kupandishwa thamani, mradi wa shilingi bilioni tano, shilingi bilioni nne unakuwa wa shilingi bilioni saba? Nataka Mradi wa Kamwanda kuanzia sasa Mheshimiwa Waziri kaufanyie mahesabu uanze kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wananchi hawana makosa au mimi kosa langu kusema panatokea wizi ndiyo mmesimamisha mradi? Maana yake mimi ndiyo nimesema kuna wizi, baada ya kusema kuna wizi shilingi milioni 800 hakupewa na mradi umesimama, wananchi wanateseka hawana maji, kosa lao ni nini? Ningeachia mradi tungeibiwa zaidi ya shilingi bilioni 3.5. Hata mtu fanya hesabu kidogo tu, mradi wa kutoka Kate mpaka Isale ni shilingi bilioni 5.4 na unakwenda zaidi ya kilometa 30, Mradi wa Kirando unachukua maji Ziwa Tanganyika nusu kilomita shilingi bilioni
7.7 Ndugu zangu hebu na nyie wenyewe semeni ukweli. Hata mtu mpumbavu hakusoma darasa la pili atajua hesabu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, mradi wa kutoka Kate kwenda Isale una-supply vijiji saba njiani, kilometa 35, shilingi bilioni 5.4 na hapo bado kuna wizi ndani yake.

Mheshimiwa Spika, vijiji vya Nkasi karibuni vyote havina maji, Kata ya Mkwamba yote haina maji, vijiji vyote havina maji wala kisima hakuna. Visima wamechimba wakati wa Mzee Nyerere pia havitoi maji. Tuna matenki Kirando tangu enzi ya Nyerere bado Rukwa iko chini ya Mkoa wa Mbeya. Kuna vijiji vya Itindi, Isale, Gele, Masolo, Katongoro, Kakoma, Ipanda havina maji wala kisima hata kimoja.

Wananchi wanafukua maji kwenye madwimbwi wakati wa masika kama panya, hela inakwenda wapi?

Mheshimiwa Spika, Serikali inatoa hela, lakini watendaji ndiyo wanaiba hela hizi. Kwa Nkasi mimi siilaumu Serikali hata kidogo, Serikali inatoa hela lakini zinaliwa na wajanja wajanja wanapewa hela kijomba kijomba, kishangazi shangazi. Amesema Ester Bulaya hapa ni kweli yule mkandarasi hata kule Mtwara alikula hela, wala siyo uongo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kusema kweli ni hatari, maji Ziwa Tanganyika yapo wananchi hawapati maji. Ni kitu cha ajabu kabisa, mradi wa shilingi bilioni 7.7 ulikuwa tayari kwenye pipe na anapewa hela hawa mapema kabisa, walitaka kumpa shilingi bilioni moja wakati hakuna kitu, Mradi wa Isale amepewa shilingi bilioni 1.1. Nataka TAKUKURU wakachunguze miradi yote Wilaya ya Nkasi na TAKUKURU wamekwenda kule wameshakaa mwezi mmoja na nusu. Niliwaomba TAKUKURU wakakae kule Mkoa wa Rukwa, nilimwambia Mkurugenzi wa TAKUKURU mimi kaangalie miradi ya mkoa mzima wa Rukwa, mkoa mzima ni wizi mtupu na inawezekana nchi nzima lakini kule kwetu mzee walifanya maficho. Namshukuru Mheshimiwa Aweso aliwaambia wakandarasi mbele ya uso wake kwamba nyie hapa mlitaka kula.

Mheshimiwa Spika, mwenyewe Waziri wa Maji alifika mpaka Kabwe akashuhudia tenki linawekwa maji baada ya maji kujaa limepasuka lote pwaaa! Mpaka leo Mheshimiwa Waziri hawajenga lile tenki. Tulikwenda na wewe mpaka leo hawajenga lile tenki. Yule mkandarasi akaja kukuambia ooh mimi tunajuana tunajuana kitu gani?

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.