Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019

Hon. Andrew John Chenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019

MHE. ANDREW J. CHENGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ya asubuhi hii niseme kwa kufupi. Nampogeza sana Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mheshimiwa Engineer Isack Kamwelwe na Naibu wake Mheshimwa Aweso.

Mheshimiwa Spika, vile vile nampongeza Katibu Mkuu wa Wizara hii Profesa Kitila Mkumbo, Naibu Katibu Mkuu Engineer Kalobelo, watendaji wote na Watumishi wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri ambayo wanaendelea kufanya. (Makofi)

Mheshiwa Spika, hotuba ya Mheshimiwa Waziri ni nzuri, imebeba matumaini kwa Watanzania kwenye sekta hii muhimu. Waswahili wanasema mnyonge mnyongeni, lakini haki mpeni. Naamini Wizara hii ingeweza kufanya mambo makubwa, lakini limitation ya rasilimali fedha, hiyo ndiyo tunaiona sote. Tunawapongeza kwa haya, hata kwa ile pesa kidogo ambayo wameweza kupewa, mnaona matokeo kwa kazi waliyofanya kwa mwaka huu tunaomaliza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naipongeza sana Serikali, maana ukilinganisha bajeti ya mwaka 2017/2018 ambao tunaumaliza, kwa upande wa fedha za maendeleo mwaka huu Serikali tofauti na mwaka 2017/2018 ambapo sehemu kubwa ya bajeti ya maendeleo ilikuwa ya kutoka nje, safari hii bajeti ya maendeleo ni fedha zetu za ndani. Naipongeza sana Serikali kwa hilo na tuendelee hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ila tu kwenye Fungu Na. 05 kwa upande wa umwagiliaji, bado sehemu kubwa ya fedha za kutoka nje. Nadhani kama tunataka tufikie malengo letu ambayo mpaka sasa tuko nyuma sana, maana tulikuwa tumepanga ifikapo mwaka 2015 tuwe tumekuwa na ekari milioni moja za umwagiliaji wala hatujafika huko.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, unaiona hali hii, lakini hata kwako hapo, mimi huwa napita na Waheshimiwa Wabunge wote tunapita sehemu ya Itanana pale au Kibaigwa hapo, kipindi cha masika hayo maji tungeweza kuyavuna tukafanya mambo makubwa. Siyo mbali, hapo kwenye Jimbo lako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo niseme mambo ya Bariadi. Naishukuru sana Serikali, naona mradi wa kutoka Ziwa Victoria kupeleka Mkoa wa Simiyu, mradi mkubwa wa kitaifa unatoa matumaini. Nimeaangalia kitabu cha Volume IV siuoni mradi huo, ila kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwenye schedule ukurasa 198 naona zipo shilingi bilioni 15. Sasa napenda Mheshimiwa Waziri anapokuja ku-wind-up hoja yake hili suala tulielewe sote vizuri, kwa sababu haiwezekani tukapitisha mradi huo lakini kwenye eneo la pesa za maendeleo hazionekani. Yawezekana labda zimewekwa kwenye fungu lingine, sitaki kuwasemea lakini watanisaidia kulielewa hili.

Mheshimiwa Spika, tuwape wananchi wa Simiyu matumaini ya kupata maji salama ya uhakika. Sisi tuna shida sana ya maji, lakini kwa mradi huu naona tunaenda vizuri. Wananchi wa Busega, wananchi wa Bariadi, wananchi wa Itilima, wananchi wa Meatu na wananchi wa Maswa, mradi huu utatuleta manufaa makubwa sana kwa maendeleo yetu. Tuombe tu kwamba utekelezwe kwa haraka, usanifu huu ukamilike mwezi huu na kweli tuanze kazi ya kuandaa zabuni ya kufanya kazi hiyo.

Mheshimiwa Spika, la pili, Mfuko wa Taifa wa Maendeleo ya Maji tulianzisha zaidi ya miaka saba iliyopita, lakini napenda sasa Serikali iende na wakati. Tulianza na Wajumbe wanne; Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mjumbe mmoja anatoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Wizara ya Fedha na Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Jamani tunataka Mfuko huu uwe ndiyo engine ya maendeleo katika kusukuma miradi ya maji. Naomba basi tupanue sura ya uwakilishi kwenye bodi hiyo, isiendelee kukaa kama kitengo cha Wizara. Tunataka isimame iwe na CO wake, Sekretarieti yake, Meneja wa Mfuko, wasimamie shughuli hii. Naomba sana Serikali walione hilo kwa haraka.

Mheshimiwa Spika, lingine ni la skimu za umwagiliaji. Mwaka 2016 Serikali ilitaja kwenye bajeti yake, kulikuwa na mabwawa kama kumi na bwawa moja lilikuwa katika Jimbo langu la Bariadi, Bwawa la Kasoli. Sasa hapa katikati silioni tena. Mheshimiwa Waziri silioni Bwawa la Kasori, nimeangalia humu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeona Skimu ya Umwagiliaji ya Mwasibuya inaenda vizuri. Naishukuru Serikali kwa mipango hiyo na pesa ambayo nimeiona humo. Napenda kama siyo mwaka kesho tuweke Bwawa la Kasoli lakini pia na eneo la Ikungulyambesha, mbona Wajapani walikuja wakaangalia eneo hilo, lakini kwa sababu ya tatizo la usanifu haikuwa imekaa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho, Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (BARUWASA) Bariadi. Sijui tumekosea nini, hii ni class. Daraja la Tatu, Mamlaka hii ya BARUWASA ni class three. Kwa mujibu wa kanuni zetu, unapokuwa kwenye ngazi hiyo wewe unastahili kupewa na Serikali kupitia Wizara, ruzuku ya kulipia umeme wa TANESCO wa kuendesha hizi pump za kuzalisha maji. Sisi hatupewi, tumekosea nini nauliza?

Mheshimiwa Spika, napenda sana Mheshimiwa Waziri hili utusaidie utupatie majibu ambayo yatawapatia wananchi wa Bariadi matumaini. Tuna shida ya maji, kama yalivyo maeneo mengi ya nchi hii. Siwezi kuwa mchoyo, lakini kile ambacho tunakipata tunataka rasilimali fedha hiyo itumike vizuri. Naelewa maeneo yetu mengi tuna tatizo la absorption capacity. Naiomba sana Serikali tuangalie watalaam wetu, tuwagawe katika njia ambao itawezesha Halmashauri zetu nyingi kunufaika na rasilimali fedha hizi ambazo zinatolewa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, nisingelipenda kupigiwa kengele ya pili; naipongeza Serikali kwa kazi nzuri wanayofanya. Tuendelee kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja hii. Ahsante sana.