Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Maftaha Abdallah Nachuma

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtwara Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumshukuru Mungu kwa kunijalia afya njema. Napenda kuchangia kwa maandishi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusu hospitali za wilaya 67; naomba kama hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI ilivyosema juu ya ujenzi wa hospitali za wilaya nchini. Napenda kupongeza mpango huo na sisi Wilaya/Manispaa ya Mtwara mjini hatuna hospitali ya wilaya kabisa. Naomba Mtwara Mjini tupewe hospitali hivyo kwa kuwa tuna shida sana ya hospitali na hasa ukizingatia hata hospitali ya kanda hatuna Mtwara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ubovu wa barabara Mtwara Mjini; kuna barabara ambazo hazipitiki kabisa wakati wa masika (kifuku). Barabara hizo ni Mbae –Mbawala chini, Mtawanya- Namayanga na Mikindani – Dimbuzi kupitia Lwelu. Naiomba sana Wizara barabara hizi za mjini Mtwara zijengwe kwa lami ili kuondoa usumbufu wa kukarabati kila mwaka kwa kuwa maji huharibu wakati wa mvua na wananchi wanakosa mawasiliano kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, stendi za kisasa Magomeni na Mikindani Mtwara; kumekuwa na ahadi za muda mrefu sana juu ya ujenzi wa stendi Mtwara Mjini eneo la Magomeni, Mkanaledi na Mikindani Mtonya. Naomba pesa ziletwe mwaka huu wa fedha kwa ajili ya ujenzi huo kwani wananchi wengi wamehamishwa kupisha ujenzi huo eneo la Magomeni lakini Mikindani Mtonya wananchi wanaishi kwa wasiwasi juu ya kupewa fidia majumba yao ili kupisha ujenzi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu TARURA Mtwara Mjini; watu wa TARURA ni viburi sana na hasa Mtwara Mjini. Wakati mwingine wanakaa na fedha kwa mfano Mtwara Mjini walikuwa na Milioni 20 za halmashauri lakini hawachongi barabara na miundombinu ya mjini inaharibika sana wakati wa mvua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili; TARURA wanakataa kutoa taarifa kwa wananchi pamoja na mimi Mbunge kuwaandikia barua kuja kutoa ufafanuzi juu ya ujenzi wa miundombinu ya barabara kwenye mikutano ya hadhara lakini TARURA pekee walikataa kuwapa taarifa wananchi juu ya mpango kazi wao wakati wanafanya kazi na wapo kwa ajili ya wananchi wa Mtwara Mjini. Watendaji wa aina hii hawatufai Mtwara kwani wananchi lazima wapewe taarifa za maendeleo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo ubadhirifu mkubwa wa fedha za halmashauri nchini. Kwa mfano Mtwara Mjini Mwekahazina na syndicate yake walitafuna milioni 800 na ushee. Cha ajabu Mwekahazina kahamishwa lakini hajachukuliwa hatua za kupelekwa kwenye Mahakama ya Mafisadi, pia wenzake waliohusika bado wapo Mtwara Manispaa na wanafanya hujuma juu ya Mkurugenzi kwa kusimamia vema halmashauri ya Mtwara Manispaa. Naomba wahusika wote wachukuliwe hatua stahiki na kuhamishwa mara moja Halmashauri ya Mtwara Mikindani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu dawa; upatikanaji wa dawa bado siyo mzuri sana Mtwara Mjini, wananchi wengi wanaambiwa hamna dawa kwenye zahanati zetu na hospitali ya Mkoa wa Mtwara. Naomba dawa ziongezwe na Mbunge nipewe taarifa juu ya kiwango cha dawa.