Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Mohamed Omary Mchengerwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rufiji

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kukushukuru sana kwa kunipa fursa hii na kwa niaba ya Wandengereko wote duniani tunakushukuru sana na tunakuombea dua kwa kuwa Mbunge wao sasa ameweza kusimama na kuzungumza mbele ya Bunge lako hili Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuwapongeza sana Waheshimiwa Mawaziri wote ambao wamewasilisha taarifa zao, Mheshimiwa Suleiman Jafo kaka yangu pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Kwa kweli niseme tu kwamba wanafanya kazi nzuri. Hata hivyo, pamoja na kwamba wanafanya kazi nzuri Watanzania wanaendelea kuwaombea dua pamoja na kuiombea Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi iendelee kufanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Tunatambua kwamba Serikali yetu ya Awamu ya Tano sasa imeridhia kuwarejesha baadhi ya watendaji wale ambao wana vigezo maalum kuweza kurejea kazini. Hii ni pongezi kubwa sana, kwa niaba ya watendaji wote nchi nzima wanaishukuru sana Serikali yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora akumbuke kwamba miaka ya 2000 walikuwepo Watendaji wa Vijiji ambao walifanya kazi kwa kujitolea ambao kabla ya tamko la mwaka 2003 watendaji hawa mwaka 2004, Waziri wa Utumishi aliyekuwepo wakati ule, Brigedia Ngwilizi alitoa tamko la kutoa ajira kwa Watendaji wa Vijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora aweke kumbukumbu zake vizuri sana. Wakati wa tamko lile la mwaka 2004 ambalo lilipelekea kuajiriwa watendaji wengi wa vijiji hususani vijiji vyangu karibu vyote vya Wilaya ya Rufiji, watendaji wale hawakuwa na sifa ya kuwa na vyeti vya utumishi. Mwaka 2006 tamko lililofuata liliwataka watendaji waajiriwe kwa kuwa na vyeti vya utumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri tumshauri vyema Mheshimiwa Rais atambue kwamba wapo watendaji walioajiriwa mwaka 2004 bila ya kuwa na vyeti vya utumishi. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu iwapo leo hii tunasema kwamba watendaji wale waondolewe kazini kwa kuwa hawakuwa na vyeti, lakini vigezo vya ajira mwaka 2004 havikuwataka wao wawe na vyeti vya utumishi.

Mheshimiwa Waziri iwapo tutaamua kuwaondoa kazini watendaji hawa tunavunja mambo mengi ya kisheria hususan Sheria za Kazi. Pia niwashauri watendaji wote nchini wale ambao wanaangukia kwenye tatizo hili; iwapo barua zao za ajira zinaonesha kabisa kwamba hawakupaswa kuwa na vyeti vya utumishi, basi wasilalamikie katika mioyo yao, wasisite kwenda kwenye Mahakama za kazi ili waweze kupata haki zao za msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwa sababu watendaji hawa hawana makosa, kosa ni letu sisi wenyewe viongozi wa Serikali ambao tulitoa tamko la ajira kwa watumishi ambao hawakuwa na vyeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwa Ndugu yangu Mheshimiwa Suleiman Jafo, nimshukuru sana kwa kazi nzuri aliyoifanya; lakini kipekee kabisa nimshukuru kwa kiasi cha fedha alichokitoa kwa ukarabati mkubwa wa Kituo chetu cha Afya cha Ikwiriri, tulipokea shilingi milioni mia saba. Hata hivyo nimwombe na nimkumbushe, aliwaambia wananchi wa Rufiji kwamba atawapatia kiasi cha shilingi milioni mia saba nyingine kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya kule Mwaseni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, nimwombe Katibu Mkuu kama maagizo haya anayo basi kuhakikisha kwamba kiasi hiki cha fedha kimekwenda; na wananchi wa Kata ya Mwaseni tayari walishaandaa mazingira ya ujenzi wa kituo cha afya kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe kwamba Kata ya Mwaseni ndipo tutakapozalisha umeme wa Stieglers’ Gorge. Kwa hiyo utoaji wa fedha hizi milioni mia saba ni muhimu sana, kwa sababu tunategemea kwamba population ya wananchi wa Kata ya Mwaseni itakuwa kubwa sana. Kwa kuwa sasa Mbunge wao amepambana kuhakikisha kwamba Stieglers’ Gorge sasa inarejea na sisi tunamuunga mkono Mheshimiwa Rais. Tumwombe sana Mheshimiwa Waziri, kiasi hiki cha fedha sasa kiweze kufika na wananchi wetu wa Kata ya Mwaseni waweze kupata kituo cha afya kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunatambua kazi ya Waziri, Mheshimiwa Suleiman Jafo ni nzuri sana. Yeye ni mchapakazi kwa ajili ya wanyonge; wananchi wa Rufiji wanaomba nyongeza ya ambulance kwa ajili ya Kata hii ya Mwaseni pamoja na Tarafa nzima ya Mkongo, pia katika Kata ya Mbwala kuna uhitaji mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiendelea katika elimu nimwombe Mheshimiwa Waziri atambue kwamba Rufiji tumetoka katika matatizo makubwa sana mwaka 2017, matatizo ambayo yalitisha nchi nzima katika maeneo ya Rufiji, Mkuranga pamoja na Kibiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tutambue matatizo haya yalisababishwa na mambo mengi, lakini miongoni mwa mambo haya lazima tutambue kwamba wananchi wengi asilimia karibu 90 ya wananchi wa Rufiji, vijana wanaoanza darasa la kwanza hawaendelei kidato cha nne, hawaendelei kidato cha sita. Niseme zaidi ya asilimia 95 ya vijana wanaoanza darasa la kwanza hawaingii chuo kikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, yako mengi yanayosababisha vijana kushindwa kuendelea na shule, yako mambo mengi sana. Pia katikati ya mambo haya ni mazingira ya shule, umbali wa shule zenyewe tulizonazo na pia ziko baadhi ya kata ambazo hazina shule zetu za kata kwa mfano Kata ya Ngarambe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoka Ngarambe kuelekea Utete ni zaidi ya kilometa 68. Huwezi kuamini kwamba kijana anayefaulu kidato cha nne anapaswa kwenda kusoma Utete ambako anatakiwa atembee kwa kila siku kilometa 68. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri, upendeleo na dhamira ya Serikali kuona umuhimu wa kunyanyua elimu katika maeneo ambapo mwamko wa elimu ni mdogo; si dhambi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ipo hata katika Katiba ukiisoma ibara ya nane (8) ya Katiba inazungumzia umuhimu wa Serikali kunyanyua ustawi wa maisha ya wananchi wake. Tunapokwenda kunyanyua ustawi wa maisha wa wananchi tunazungumzia umuhimu wa maendeleo ya elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri atambue kwamba nchi yetu hii ipo jamii ya tabaka la wananchi wenye maisha duni na dumavu. Tabaka hili ni miongoni mwa tabaka la wananchi wa Rufiji pamoja na maeneo mengine ya Kibiti. Pia yapo maeneo ya tabaka la wananchi wenye maisha endelevu, yako maeneo hayo, ameyazungumzia katika ukurasa wa 56 wa hotuba yake katika mchakato wa kuboresha miji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri tunapokwenda kuboresha miji tuangalie maeneo yenye matatizo makubwa, maeneo ambapo kumekuwepo na migogoro ya mara kwa mara. Kwa mfano, Rufiji mwaka 2007 yalitokea machafuko makubwa kati ya wakulima na wafugaji, lakini mwaka 2017 kumetokea matatizo makubwa ya amani kila mmoja anafahamu. Nimwombe Mheshimiwa Waziri wakati amedhamiria kwenda kutatua matatizo haya na tunaipongeza Serikali kwa kazi nzuri iliyofanya, tuangalie sasa uwezekano wa Serikali kwenda kubadilisha kabisa hali ya maeneo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili liliwahi kufanywa na Mwalimu Nyerere miaka ya 70 ambapo aliongeza mwamko wa kutoa elimu na kuwasaidia wananchi wenye matatizo makubwa ya elimu na ya kiuchumi. Miongoni mwa watu walionufaika tunaye Profesa Kabudi alinufaika na mpango wa Mwalimu Nyerere wa mwaka 1973 na niiombe Serikali sasa kipekee kabisa…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na naipongeza sana Wizara na Serikali kwa ujumla. Ahsante sana.