Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Martha Moses Mlata

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara hizi mbili. Kwanza niwapongeze Mawaziri wote Mheshimiwa Selemani Jafo pamoja na Mheshimiwa George Mkuchika, Naibu Mawaziri George Kakunda na Josephat Kandege, Makatibu Wakuu wote katika Wizara hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi nimpongeze sana Mheshimiwa Jafo na Manaibu wake kwa kazi kubwa ambayo tumeiona. Wamekuwa wakitembelea Halmashauri zetu na maeneo yetu yote kuhakikisha kwamba shughuli za maendeleo zinamfikia mnyonge kama Rais wetu ambavyo amekusudia. Nampongeza sana Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa Selemani Jafo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nami niungane na wale wote wapenda maendeleo waliompongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya. Naomba apelekewe salamu na akubali kwamba yeye kuwa mti ule uzaao matunda yaliyo bora na yaliyo masafi na yaliyo mazuri, kwa sababu mti wa namna hiyo ni lazima upigwe mawe ni lazima upigwe vijiti na ni lazima unenewe maneno yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba akubali kwamba yeye ni mti uzaao matunda yaliyo mema na ndiyo maana wale wasiopenda mema wanamrushia mawe. Naomba pia apelekewe salamu kwamba wananchi wa Mkoa wa Singida tuko pamoja na yeye, tunamuunga mkono kwa kazi kubwa na nzuri ambayo ameendelea kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyoongea upande wa miundombinu barabara za Mkoa wa Singida nyingi zinapitika hata kama ni za vumbi kwa sababu wale akinamama walioko pembezoni hata wanapotaka kupata huduma za afya kuna bajaji, kuna bodaboda, kuna Noah. Wakifika hospitali wanakuta nidhamu ya watumishi iko safi, dawa ziko nyingi, Rais ameongeza bajeti kubwa, vitendea kazi vipo, wafanyakazi wanafanya kazi nzuri ya kuwahudumia wananchi. Tunamuunga mkono aendelee tuko pamoja naye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho nasikitika sana mpelekeeni salamu Mheshimiwa Rais mwambieni atusaide tupate upinzani utakaosaidia kujenga Taifa hili, Upinzani unaojitambua, Upinzani unaojitambua, Upinzani ulio bora, Msajili wa Vyama awapeleke Wapinzani kwenye nchi zenye Upinzani wenye mfano ambao Mataifa yao yameweza kusimama imara. Nasema hivi kwa sababu hapa Tanzania bado hatujawa na Upinzani ulio imara, Upinzani utakaosaidia katika Taifa hili ili tuwasaidie wanyonge na kulijenga Taifa letu. Mpelekeeni salamu kwamba, bado hatuna Wapinzani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Rais...

T A A R I F A . . .

MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sipokei taarifa hii kwa sababu Upinzani uko wapi wa kuruhusiwa kwenda kufanya mikutano kwa wananchi, Upinzani unaoenda kuwahadaa wananchi wasifanye shughuli za maendeleo, wakae wanaandamana barabarani, Upinzani unaomkataa Rais, Upinzani usioona yale mazuri, Upinzani ni upi utakaoruhusiwa kwenda barabarani.

T A A R I F A . . .

MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, iwe Vyama vya Mageuzi, iwe ni Upinzani lakini mimi nasema Upinzani gani hata mambo mazuri wanayakataa? Rais amejitoa kwa ajili ya Taifa hili...

KUHUSU UTARATIBU . . .

MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nilikuwa kwenye utawala bora lakini sasa nataka kusema mwambieni Rais kwamba yale yote anayoyafanya wako watu watakuja kuyakumbuka kama ambavyo wanamkumbuka Jakaya sasa hivi, asonge mbele aendelee kuwa mti uzaao matunda mema, watakuja kumkumbuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shukrani hizo ambazo nampa Mheshimiwa Rais, tunamshukuru sana Mheshimiwa Selemani Jafo kwa sababu katika Mkoa wetu wa Singida ametuletea hospitali mbili, hospitali ya Mkalama pamoja na Ilongero. Naomba hospitali hizo zikajengwe mahali ambapo amezipanga. Pia naomba sana hospitali ya Ilongero itakapokwenda kujengwa pawe ni pale ambapo ndipo maeneo ya Makao Makuu ya Halmashauri ile, hivyo naomba Mkurugenzi ahamie haraka eneo lile ambalo mwaka 2006 ndiyo tulipitisha kwamba patakuwa ni Makao Makuu. Namwamini na naomba atembelee eneo lile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana nizungumzie suala la afya. Naomba kuuliza, Mheshimiwa Rais ametoa fedha nyingi sana kwa ajili ya dawa zile Delivery Kits kwa ajili ya kujifungua vile vitu ni vya bure kwa nini wanauza au ni ule mfuko ndiyo wanataka kuuza? Watoe ule mfuko waache vifaa waweke labor, wanawake wapate vifaa bure, wasiuze ile kits au set kwa ajili ya wanawake. Kumbukeni pia kujenga mama ngojea kwa ajili ya kuokoa akinamama wenye matatizo ya uzazi ili waje wasubirie pale, hilo naomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, naomba sana hebu tuangalie Kata ya Mwanga kule Mkalama, hata nguzo moja ya umeme haijawahi kupelekwa, kwa sababu tunataka kujenga uchumi wa viwanda na kule ndiko kwenye kilimo cha vitunguu, alizeti na mahindi, tunaomba wapeleke nguzo na hatimaye waweke umeme kule. (Makofi)