Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Ruth Hiyob Mollel

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mweyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hoja ambazo ziko hapo mezani. Kwanza nichukue nafasi kuwapongeza Mawaziri wote wawili na Naibu Mawaziri wao na watendaji wote walioifanya hii kazi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na tamko ambalo lilitolewa na Mheshimiwa Waziri wa Ofisi ya Rais, Utumishi kuhusu kurudishwa kwa wale watumishi waliomaliza darasa la saba ambao walikuwa wamefukuzwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitoe masikitiko yangu kwamba tangu awali hawa watumishi hawakutakiwa kufukuzwa kazi, kwasababu waliajiriwa kwa kigezo cha darasa la saba na mikataba yao ilikuwa ya darasa la saba. Kwa hiyo, hawakustahili kufukuzwa kazi na kwa kweli hiyo haikuwa sahihi na Serikali haikuwa sahihi. Sasa wamerudishwa kazini, tukumbuke wamekuwa nje ya utumishi wa umma karibu mwaka mzima, imesababisha familia hizi kupata matatizo ya kifedha, manyanyaso na kutokuwa na income. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujua, pamoja na kwamba Serikali imesema walipe mishahara yao yote, lakini je, katika ule usumbufu ambao wameupata kwa muda mrefu karibu mwaka mzima, Serikali inasema nini kuhusu hilo la kuwafidia kwa sababu ya kupata shida kwa kukosa kazi wakati walistahili kuwepo kazini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala linalofuata ninalotaka kuchangia, ndiyo wote ambao walikuwa na vyeti vya darasa la saba wamerudishwa, lakini kuna wale madereva kwa mfano ambao walikuwa darasa la saba na hawakutolewa kazini, lakini kuna madereva ambao walikuwepo kabla ya Mei, 2004 lakini kwa sababu ya shinikizo la kupata vyeti, baadaye walikwenda wakapata vile vyeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa tamko la Mheshimiwa Waziri ni kwamba wale wote ambao waliajiriwa kabla ya hiyo Mei, 2004 kile kigezo cha form four hakiwahusu. Kwa hiyo, wanatakiwa wote warudishwe. Napenda kujua, sasa hawa madereva kwa mfano, ambao walikuwepo kabla ya Mei, 2004 lakini baadae ikabidi watafute vyeti, kwa sababu wengine wakwenda kujaribu form four, wameshindwa, wakaenda kutafuta vyeti. Je, wanarudi pia? Naomba Mheshimiwa Waziri alitolee tamko kwa sababu sijaiona kama ameizungumzia katika tamko lake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo nataka kuzungumzia ni kuhusu hawa walioanza kazi baada ya Mei, 2004, ni kweli wameingia kwa vigezo ambavyo siyo sahihi, wamegushi vyeti ambayo kisheria siyo sawasawa, nasi hatuungi mkono, lakini pia ukitazama kwa upande mwingine, wamekuwa wanachangia kodi, NSSF, wengine ni PSPF, wengine ni Local Government Provided Fund (LGPF); je, Serikali inatoa kauli gani kuona kwamba hawa watumishi kweli pamoja na kwamba wame-forge vyeti ambayo sio sahihi, lakini pia wamekuwa wanakatwa kodi, wamekuwa wanachangia hifadhi ya jamii? Je, Serikali haioni ni sahihi basi kwa hawa watumishi angalau walipwe basi makato yao ya hifadhi ya jamii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alipokuwa akijibu swali langu la nyongeza, alieleza kwamba kulikuwa na majadiliano kati ya Serikali na Vyama wa Wafanyakazi kuhusu jinsi gani ya kufanya ubinadamu kwa ajili ya ku-compensate hawa ambao wamefukuzwa kazi kwa makosa ya kughushi vyeti. Napenda kujua hayo majadiliano yamefikia wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo pia watumishi ambao wametumia majina ya watu wengine kusoma, wengine wamepata udaktari, wengine wamemaliza u-nurse, wengine wamefanya ualimu; wamesoma hizo courses na wamehitimu, lakini kwa majina ya watu wengine. Napenda kusikia tamko la Mheshimiwa Waziri anasema nini juu ya watu hao? Kwa sababu tunao watu ambao wamesoma kwa maina ya watu wengine na ni watu wakubwa na wako kazini, kusiwepo na double standard. Lazima Serikali ionekane inatenda haki kwa watu wote bila ubaguzi wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja sasa kwenye suala la watumishi wa umma kutofungamana na itikadi za kisiasa. Hili jambo nilishalizungumzia siyo mara moja, wala mara mbili na ninaendelea kulizungumza. Labda ni-declare interest kwa sababu mimi mwenyewe nilikuwa mtumishi wa umma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwa na watumishi ambao wanafungamana na itikadi, kuwa na watumishi ambao wakiwa katika utumishi wa umma wanajihusisha na mambo ya siasa kunadidimiza impartiality ya utumishi wa umma, inaua professionalism. Tunataka utumishi wa umma wafanye kazi zao kwa kuzingataia professions zao kwa ajili ya kuendeleza Taifa hili na kuleta maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, athari za watumishi wa umma kujiingiza katika siasa ni kukosa continuity katika utumishi wa umma. Kwa sababu utumishi wa umma ndiyo institutional memory ya nchi. Ikiwa tunakuwa na watumishi katika ngazi za juu ambao wanaletwa wakiwa kwenye Vyama vya Siasa inaharibu kabisa integrity ya utumishi wa umma. Tunaona mahali kama Japan, kila mara Mawaziri Wakuu wanaondoka, wanakuja, lakini utumishi wa umma unakuwa intact kwa sababu hauhusiani na chama chochote. Utumishi wa umma unatakiwa utekeleze sera za chama kilichoko madarakani with impartiality. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mtindo wa sasa hivi wa Awamu ya Tano ya kuingiza watu wenye mambo ya siasa kwenye utumishi wa umma, tunaua hiyo integrity na tuta-suffer kama nchi na itabidi kuja kufanya marekebisho makubwa sana. Kwa hiyo, ni maoni yetu kwamba Serikali sasa iangalie upya na turudi tulikotoka. Enzi zetu watumishi wa umma walikuwa hawaruhusiwi kujihusisha na siasa kabisa wanapokuwa watumishi wa umma. Wakitaka kujihusisha na siasa, watoke katika utumishi wa umma waende wakahangaike na siasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la nyongeza za mishahara na kupandishwa vyeo. Watumishi wa umma ndio engine of growth ya nchi hii. Awamu hii ya Tano sioni kabisa kama Serikali iko serious na kuangalia rasilimali watu. Naona haiko serious kwa sababu tangu wameingia madarakani watumishi wa umma hawapati nyongeza zao za mshahara ambayo ni haki yao; hawapandishwi ngazi zao za mishahara, malimbikizo yao bado hayalipwi yakamalizika, kila siku ni hivyo hivyo na maneno mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila ya kuwa na Utumishi wa Umma wenye raha unaojiamini, kwa kweli hata hii dhana ya Tanzania ya Viwanda hatuwezi kuifikia. Kwa hiyo, naishauri Serikali, kwa kweli iweze kuangalia rasilimali watu, watumishi wapandishwe vyeo vyao, wapate increments zao ambazo wanastahili kwa sababu hizo increments za kila mwaka ndiyo zinawasaidia kupunguza makali ya inflation katika uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakuja kwenye suala la elimu. Sijaona kama kuna mnyororo mzuri. Tunazungumzia viwanda, ni jambo zuri; tunazungumzia standard gauge; tunazungumzia Stigler’s Gorge; lakini hatuzungumzii rasilimali watu ambayo itakuja kufanya hizo shughuli. Nikiangalia kwenye mnyororo wa elimu na nimesikia kwamba Serikali ina-train walimu wengi wa sayansi na teknolojia, ni jambo zuri. Kama Serikali ina-train walimu wa sayansi na teknolojia, ni mkakati gani basi unawekwa kuhakikisha kwamba maabara katika shule za sekondari zinakuwepo kusudi hawa Walimu wanapotoka kufundishwa sayansi na teknolojia, waende hata kwa vitendo kwenye laboratories katika vyuo vyetu. Kwa sababu malengo yote ya sayansi na teknolojia ndiyo ambayo inakuwa complement katika hiyo Tanzania ya viwanda. Huu mnyororo uendelee mpaka chuo kikuu.