Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii. Kabla ya yote, nataka nimpongeze Mwenyekiti wetu na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani pamoja na viongozi wa CHADEMA ambao kwa sasa wako katika kadhia ya kuripoti Polisi kila Ijumaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nataka nizungumzie suala la Zimamoto. Zimamoto mwaka 2016/2017, Bunge lilitenga pesa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kununua magari mawili ya Zimamoto, lakini pesa hizo hazikuweza kutoka sawasawa na Bunge lilivyopitisha. Tender Board ilikaa wakazungumza na Wizara ya Fedha pesa ziweze kutoka, zilitoka shilingi milioni 117 peke yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapozungumzia viwanda, viwanda na moto ni vitu vinaenda pamoja. Kama hutaweza kutenga pesa kwa ajili ya magari ya Zimamoto unakuwa hujafanya sawasawa katika utekelezaji wa kuleta maendeleo. Mwaka 2017/2018 Serikali ilitenga shilingi bilioni 3.5, haikutoka hata senti tano kwa ajili ya watu wa Zimamoto. Jeshi hili ninavyoliona ni kama Jeshi ambalo limesahaulika sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unafahamu kabisa kwamba Jeshi hili hata ukiangalia mavazi yao, ni chakavu kuliko majeshi mengine. Sasa sijajua tunawaweka katika ma-grade kwa sababu gani? Kwa hiyo, naomba Serikali na namwomba Mheshimiwa Waziri anapokuja kujibu hoja, tunataka kujua hizi pesa tunazopitisha kama Bunge, halafu hazitumiki na wala hazitoki, Wizara ya Fedha haitoi pesa. Kama Bunge limepitisha, kwa nini Wizara haitoi? Namwomba Mheshimiwa Waziri aje atoe majibu anapokuja kuhitimisha hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia jengo la Mchicha. Unajua Zimamoto mpaka sasa hivi wanapanga na kuna jengo tayari Serikali imeshaweka pesa pale, jengo halijakwisha, limechakaa na safari hii hakuna hata senti tano iliyotengwa kwa ajili ya jengo lile. Sijajua tunawaza nini na tunafikiria nini kwa ile pesa tuliyoizamisha pale Mchicha, mpaka leo hiyo pesa hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la Jeshi la Polisi. Jeshi la Polisi kuna wakati niliwahi kuongea na IGP nikamwambia kwamba Jeshi linafanya kwa professionalism. Unapokuwa na jeshi lazima na intelijensia inafanya kazi yake kwa makini kwa kufuata weledi wa kile walichosomea. Leo hii Jeshi la Polisi linafanya kazi na mitandao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, binti mdogo anaitwa Mange Kimambi anaanzisha maandamano mtandaoni, leo wanalitoa Jeshi sehemu za siri kulileta barabarani. Sidhani kama wako sahihi. Wakitokea Mange Kimambi 10, wanataka kuniambia watashinda wakifanya mazoezi barabarani? Sidhani kama wako sahihi. Mheshimiwa IGP, nafikiri inabidi kujitafakari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Waziri Mwigulu alipokuwa Singida sikumbuki ilikuwa hafla gani, alizungumzia kuhusu waandamanaji na akasema waandamanaji watakapoandamana inaweza ikatokea kupigwa risasi. Sasa sijajua kwamba anaota au sijajua kama yeye ni Mfalme Njozi, sijafahamu. Ninachojua, Polisi kazi yake ni kulinda raia. Maandamano mimi naona wanazungumzia kama ni dhambi au kitu kibaya. Jeshi la Polisi kazi yake kufanya intelijensia. Elimu waliyosomea ipo kwa ajili ya kuzuia mabaya, wala haipo kwa ajili ya kutetea kwa kutumia vitu vya kufikirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwa Waziri, Mheshimiwa Mwigulu, yeye ni kiongozi wa wote. Hisia zake za kichama ajitahidi kuzidhibiti zisiweze kumtoa kwenye reli. Naomba afanye kwa weledi, ataacha alama katika jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapolalamika, Polisi wanaposema wamefanya utafiti na kugundua kuwa kutatokea hali mbaya, sijaelewa huwa inaangalia upande mmoja, au ni pande zote. Kiongozi wa Chama cha Upinzani, kiongozi wa Jimbo kwa maana ya Mbunge, anaandika barua ya kufanya Mkutano ambao huo wameuruhusu, lakini Polisi inatoa majibu ndani ya masaa mawili kabla ya Mkutano kusema kwamba tumegundua amani haitakuwapo. Kwa kweli nashindwa kuelewa. Mikutano hii akifanya Polepole intelijensia haioni ubaya, lakini akifanya mtu wa CHADEMA Mheshimiwa Heche, intelijensia inaona ubaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu, nataka kuwaambia, siku zote ubaya wa kidogo kidogo huwa unajenga chuki ndani ya watu. Mheshimiwa Bwege mchana wa leo amezungumza na mkamshutumu kwamba anaongea kwa hisia, lakini kumbukeni mabaya huwa hayatokei isipokuwa yamefanywa kidogo kidogo mwisho wa siku yakawa makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa hili ni la wote na wala siyo favour sisi kuwepo hapa. Ni haki yetu na wajibu wetu na kwa sababu walikubali vyama vingi, wakubali kumeza vidonge vya vyama vingi. Polisi watuachie CCM tukae nayo pembeni sisi wenyewe tufanye nao siasa, wao wakae pembeni. Kwetu sisi CCM ni wepesi kama karatasi wakikaa pembeni; lakini wakitulazimisha na sisi ni binadamu, tutatafuta njia mbadala ili kuhakikisha tunafikia wapi tufike kwenye malengo tunayoyataka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia Uhamiaji, dada yangu kiongozi wa Uhamiaji anafanya kazi vizuri, lakini bado kuna maeneo madogo madogo hasa kwenye biashara ya kujenga nyumba za Uhamiaji, asimamie vizuri pesa za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye Jeshi la Magereza, wako vizuri, wanafanya vizuri. Tatizo lao Magereza pia ni kama la Zimamoto kutokuwa na vifaa vya kutosha ikiwemo nyumba za kuishi, lakini uniform ni kilio kikubwa sana kwa wafanyakazi hao. Magari kwa Magereza ni shida. Ukienda mikoani, wanahitaji kupeleka wafungwa kwenye kesi, hawana magari. Sasa sijajua tunategemea nini? Kesi zitaendaje? Watafanyaje kama hatutaliwezesha jeshi hili kufanya kazi zao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kwamba uhalifu umeongezeka kama wanavyosema, lakini Magereza mengi yana vyumba vidogo. Magereza mengi hayana vyumba vya mahabusu vya wanawake. Wanawake kwa mfano ukienda Gereza la Kyela, hakuna sehemu ya kuweka wanawake, wanaenda kulala Tukuyu. Ni mwendo mrefu sana na wakati huo huo hawana gari la kuchukua hao watuhumiwa na kuweza kuwapeleka Tukuyu na Kyela. Naomba Mheshimiwa Waziri anapokuja atuambie amejipanga vipi kuondoa changamoto hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado nafikiria sisi kama Bunge hatujajipanga sawasawa kuisimamia Serikali. Ni mara nyingi tumepitisha bajeti lakini bajeti hizi hazitoki. Bajeti hizi, pesa hazitoki, ni hadithi. Watu wetu wanakuja hapa Dodoma, tunakaa nao, tunawasikiliza kwenye Kamati, tunakubaliana. Ikifika kwenye utekelezaji, hiyo imekuwa ni shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Bunge lako Tukufu linapopitisha bajeti, tunataka tukija kwenye mwaka mwingine wa fedha hizo pesa zifanye kazi na ziwasaidie watu wetu kufanya kazi zao na waweze kufanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naomba kuunga mkono Kambi Rasmi ya Upinzani, najua hatujaleta maoni yetu, lakini bado tunaamini kwamba maoni yetu yangali yanaishi hata yale ya mwaka 2017 yanaweza kuendelea kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, nashukuru. Ahsanteni.