Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. ZITTO Z. R. KABWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti ya Mafungu takribani sita ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Kwanza nianze kurejea kwenye Katiba, Ibara ya 15 ambayo inasema kwamba kila mtu anayo haki ya kuwa huru na kuishi kama mtu huru. Ibara ya 15(2) inasema:

“Kwa madhumuni ya kuhifadhi haki ya mtu kuwa huru na kuishi kwa uhuru itakuwa ni marufuku kwa mtu yeyote kukamatwa, Kufungwa, kufungiwa, kuwekwa kizuizini, kuhamishwa kwa nguvu au kunyang’anywa uhuru wake vinginevyo.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ndiyo Katiba yetu ambayo inatuongoza na sote hapa tumeiapa kuilinda na kuitetea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niwakumbushe na hasa niwakumbushe wana CCM. Kwenye hotuba ya Mwalimu Nyerere alipokuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mwaka 1987 kwenye Mkutano Mkuu alisema “Panapokuwa hapana haki wala imani na matumaini ya kupata haki, hapawezi kuwa na amani, utulivu wa kisiasa na hatima yake panazuka fujo, utengano na mapambano” haya ndiyo maneno ya Baba wa Taifa, amani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunazungumza kwa mara ya kwanza tokea Mbunge mwenzetu ashambuliwe kwa risasi. Tumekaa humu ndani kwa mara ya kwanza kwa maana ya bajeti, tunakwenda kupitisha zaidi ya shilingi bilioni 596, asilimia 63 ya bajeti yote ya Wizara ya Mambo ya Ndani inakwenda Jeshi la Polisi mpaka leo Jeshi la Polisi halijaweza kufanya uchunguzi na kujua ni nini ambacho kilitokea Mbunge mwenzetu akapigwa risasi hapa Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunakutana hapa tunataka tuwatengee fedha Jeshi la Polisi lakini tuna watu ambao wana miaka inakaribi miwili wamepotea hawajulikani wako wapi akina Ben Saanane. Mwandishi wa Habari, Azori Gwanda juzi mkewe amapata mtoto, mtoto hamuoni Baba yake na Jeshi la Polisi halina maelezo yoyote ambayo limeyatoa mpaka sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa hotuba ya TAMISEMI na Utawala Bora nilizungumza kuhusu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, Ndugu Kanguye ambae ni Diwani wa Chama cha Mapinduzi, wiki iliyopita Mama mzazi wa Ndugu Kanguye amefariki dunia, amefariki dunia akiwa hajui mwanawe yuko wapi. Waziri wa Utawala Bora alituambia kwamba siyo kazi ya Usalama wa Taifa kukamata tukasema sawa, hii Serikali moja, Wizara ya Mambo ya Ndani itakuja, Wizara ya Mambo ya Ndani imekuja haya watueleze! Kama siyo kazi ya Usalama wa Taifa ni kazi ya Polisi, Polisi watueleze kwamba Ndugu Kanguye yuko wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, yote haya ni mlolongo wa mambo mengi ambayo yanaweza yakatuletea shida kubwa sana katika nchi. Mbunge wa Kilwa, Ndugu Bungara amezungumza kwa hisia na wakati mwingine muache watu wazungumze kwa hisia kwa sababu watu wanapozungumza kwa hisia ndiyo wanaongea yale mambo ambayo yanawahusu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 12 Juni, 2017, mama mmoja anaitwa Ziada Salum wa Kitongoji cha Maparani, Kibiti alichukuliwa na jeshi la Polisi saa 6.00 mchana na leo ni miezi 11 mama huyu hajaonekana yuko wapi. Siku hiyo hiyo kuna mtu anaitwa Rukia Muhoni na Tatu Muhoni ni ndugu hawa, walichukuliwa na Jeshi la Polisi mpaka leo hii tunavyozungumza miezi 11 hawajaonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina orodha hapa, nina watu 348 wa Wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji na hapa hatujajumlisha watu ambao wanatoka Kilwa. Kuna mtu jana hapa alizungumza kuna zaidi ya watu 1000 wamepotea, inawezekana orodha niliyonayo hapa na nitampatia Waziri, watu 348 na katika hao watu 68 wamethibitika wamekufa. Tunaomba Serikali itueleze nini kinaendelea Wilaya za Kusini ya Tanzania.