Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Albert Ntabaliba Obama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buhigwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia bajeti iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa nimshukuru Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na timu yake yote, kwa kweli wanatupa ushirikiano mkubwa sana kwenye Kamati yetu ya Bajeti. Vilevile niendelee kumpongeza Mwenyekiti wetu wa Kamati na Makamu wake kwa kutuendesha vizuri ndani ya Kamati kwani tumeendelea kutoa maoni yetu kwenye sekta mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niipongeze Serikali kwa miradi inayotekelezwa na waliyoipanga kwenye bajeti hii sisi tumeibariki, tunaona kwamba haina matatizo, ni miradi muhimu. Miradi ya ndege, meli kwenye maziwa na bahari huko na miradi mingine ambayo inaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze bajeti kwani lengo linaonesha kwamba mnataka kulinda viwanda vya ndani na kuhamasisha uzalishaji. Kwa hiyo, hilo nalo tunawapongeza na tunampongeza Rais kwa dhamira njema ya kuleta bajeti nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo machache tu kwenye ushauri ambayo napenda niyaseme. Kwanza ni namna ambavyo tumeanza kuua halmashauri zetu. Nilikuwa nafikiri mpaka muda huu tungekuwa tumeshaleta sheria ya kufuta local government kwa sababu sasa hivi meno yote yameondoka. Ukiangalia vyanzo vingi vimechukuliwa, miradi mingi ya maji imekwenda Wizara ya Maji, kilimo ndiyo hivyo na mambo mengine. Kwa hiyo, ifike hatua mlete sheria ya kuua huu ugatuaji ambao tuliupigania kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana tulikuwa na Waziri wa Fedha tumeongea naye juu ya namna ya kuanzisha akaunti ya pamoja ndani ya Wizara ya Fedha, hii ambayo inaonesha kwamba halmashauri zetu zitakufa. Kwa hiyo, nashauri kwamba tulete sheria tuweze kufuta halmashauri zetu mara moja ili tuweze kuendelea na centralization ambayo tunaitaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuhusu wakulima wa zabibu wa Mkoa wa Dodoma. Kodi zilizopo kwenye zabibu na mvinyo unaotengeneza pombe kali kama valour zinazotokana na zabibu iko juu, tunaomba iangaliwe. Wakulima wa zabibu Mkoa wa Dodoma wanalia kwelikweli, tunaomba kwa kweli iweze kuiangaliwa ili kwenye Finance Bill muweze kuleta amendment kama Serikali ili tuweze kuwaokoa. Walikuwa wamezoea kodi ya Sh.450 sasa mmepeleka karibu Sh.3,315. Kwa hiyo, tunaomba hilo eneo waweze kuliangalia vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine ni kuhusu ETS. Kwenye ETS Mheshimiwa Waziri tumekaa naye kwa muda mrefu, mmetufundisha kama Kamati ya Bajeti lakini kuna maeneo ambayo bado tunaona kwamba kwenye bidhaa, bia, sigara hamkuongeza lakini mmeiongezea kwenye gharama ya kuweka hizo stempu ambapo wafanyabiashara itabidi waingie gharama kubwa kuliko waliyokuwa wanalipa ili kuweza kuweka hizo stempu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba hilo kwa kweli mliangalie, hizo gharama ziweze kuwa revised. Kwa kuwa production inaonekana itakuwa kubwa, kwa hiyo, tunashauri ile rate iweze kuwa ndogo. Tulifikiri teknolojia itaweza kuleta gharama ndogo zaidi kwani teknolojia haiwezi kuleta gharama kubwa. Kwa hiyo, tunaomba kwa kweli muendelee kuliangalia. Nimesikia, kuna mtu ameniambia anafikiri Mheshimiwa Rais amesema itakuwa miaka miwili lakini mmewapa miaka mitano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 2 Februari, Serikali yetu hii ili-publish regulations ambazo Kamati ya Bajeti ndiyo tumeziona leo. Hatujawahi kuona regulation ya ETS ambayo ndiyo hii hapa ilikuwa published lakini hatujawahi kuiongea kabisa. Nasi tumeisoma leo kidogo bado hatujamaliza na hatuwezi kusema mengi zaidi kwa sababu tutakutana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lazima tujiangalie sana na mifumo maana kwenye sheria humu inasema kama mtu amefungiwa huo mtambo, wakati wa kuzalisha ikitoa hitilafu anatakiwa asimamishe uzalishaji. Wanasema TRA itaweza ku-respond katika saa 48. Tukumbuke raw material za viwandani zingine zina expire baada ya saa mawili au matatu, kama yameshakorogwa yanatakiwa yazalishwe. Sasa ikisimama inakuaje, hizo gharama nani ata-incur? Mheshimiwa Waziri ana timu nzuri, naomba muendelee kuliangalia suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kodi ya ardhi. Wako watu wenye mashamba makubwa ya katani, pamba, tumbaku, mmetoa gharama ya land free kutoka 400 mpaka 1,000, watu wana mashamba makubwa, kutengeneza shamba kwa muda mwaka inamchukua gharama nyingi na gharama nyingine tena ni ya kodi. Ardhi tulipewa na Mungu bure, ingekuwa sehemu ya mtaji wa mtu aendelee. Watu wana mashamba ya chai, land rent ni bei kubwa kuliko zao lililopandwa pale juu. Kwa kweli nashauri Waziri aweze kuliangalia hili na hata Waziri wa Ardhi aweze kuliangalia, msitumie ardhi kama ndiyo mtaji wa kila kitu na huku tulipewa na Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba wakandarasi walipwe. Kwa wale wakandarisi mliowahakiki muwalipe fedha zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo linatuudhi sisi watu wa Dar es Salam tunapokuwa tuko kule na katika Mikoa mingine ya Mwanza na kadhalika ni kufunga madukasaa 12.00 asubuhi mpaka saa 4.00 ya kila Jumamosi iendayo kwa Mungu katika mikoa yote ya Tanzania. Hebu tujaribu kufanya utafiti kuona hasara tunazozipata, kodi tunazozipoteza, unaamka asubuhi unataka kutumia fedha ya mtu anasafiri hakuna kibanda cha kutuma fedha. Watu tulizoea supu za asubuhi, hatuwezi kunywa supu Jumamosi. Mheshimiwa Waziri hebu mlipitie, sheria ya usafi tunaiheshimu, ingeweza ikatokea hata kwa mwezi mara moja, haiwezi kila Jumamosi ni matatizo huwezi kupata huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naunga mkono hoja na Waziri ajue challenge kubwa ni kwamba tuna fedha kidogo lakini mipango ni mingi, lazima ifike mahali tu- compromise. Watu nao ni muhimu, kipato cha watu ni muhimu, kwa hiyo, tu-balance mambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.