Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Prof. Norman Adamson Sigalla King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. PROF. NORMAN A.S. KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nianze kwa kuishukuru Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi kubwa na nzuri inayofanywa chini ya uongozi wa Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ya kuimarisha miundombinu na kutengeneza mazingira sahihi ya uwekezaji Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya eneo zuri sana ambalo Mheshimiwa Rais amefanya ni kuimarisha Benki ya Uwekezaji (TIB) na matawi yake ambapo sasa Mtanzania anayetaka kuwekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji kinachohitaji mitaji mikubwa, benki zetu sasa zinaweza kufanya; ukitaka kuwekeza kwenye viwanda benki zetu sasa zinaweza kufanya; na uchimbaji wa mabwawa benki zetu sasa zinaweza kufanya. Kwa hiyo, naomba sana Watanzania kwa ujumla wao wale wanaopenda kuwekeza watembelee benki zetu za TIB ili waweze kutumia fursa hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, ni salamu za wananchi wa Makete. Wanampongeza Rais hasa kwa kutenga vijiji 51 katika ya 67 vilivyoko Makete ili waweze kupata umeme ambao utafasili uanzishwaji wa viwanda na matumizi mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili naomba nisisitize jambo moja. Wilaya kama Makete ambazo tunafahamu mchango wake kwenye nchi yetu ya Tanzania na hasa upande wa maji yanayozalisha umeme ikiwemo bwawa tarajiwa na mradi mzima wa Stigler’s Gorge, Makete ndiyo hub, ndiyo catchment mama ya mito hiyo ya Ruaha Mkuu ambao baadaye unabadilika majina unaitwa Kilombero na baadaye kuitwa Rufuji. Naomba sana Serikali ipeleke maendeleo ili kuwazuia wananchi wa Makete wasije wakaingia kwenye jaribu la kuharibu vyanzo vya mito.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapelekaje maendeleo? Kwa mfano, badala ya kupeleka umeme katika vijiji 51 ilikuwa ni kumaliza vijiji vyote 67 vilivyoko Makete ili wasikate miti, wasiharibu vyanzo vya mito ambapo kama wasipoharibu tunajihakikishia kwamba miradi tunayoifikiria na kuitekeleza kama Stiegler’s Gorge, Bwawa la Mtera, Kihansi pamoja na Kidatu watapata maji kwa uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, namwomba sana hasa rafiki yangu Mheshimiwa Waziri, sera zetu za uwekezaji zisikilizane na vitendo vyetu. Mipango yetu na nyimbo zetu za uwekezaji zisipingane na vitendo vyetu. Kwa mfano, sote tunafahamu kwamba maduka ya kubadilishia fedha kwa maana ya Bureau De Change tulianza na mtaji wa shilingi milioni 20 tukapanda kwenda shilingi milioni 40, shilingi milioni 80, shilingi milioni 100, lakini sasa nafahamu mtaji wa kuanzisha duka la kubadilisha fedha ni shilingi milioni 300. Tunataka watu wawekeze kwenye maduka ya kubadilisha fedha au wafunge maduka? Kwa vyovyote vile siyo dhana sahihi hata kidogo. Unapomtaka Mtanzania wa kawaida awe na duka la kubadilisha fedha lakini mtaji wake unasema shilingi milioni 300 siyo sawa. Ushauri wangu kwenye hili, mtaji wa kuanzisha maduka haya uwe kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda Serikali ifahamu, ufa uliokuwepo kwenye maduka ya kubadilishia fedha ilikuwa ni mamlaka za Serikali kutokufuatilia kama hawa wabadilishaji wa fedha wanatoa risiti. Kwa sababu hakukuwa na risiti ambazo ziko centralized kwamba mtu
nikibadilisha dola 100,000, BoT au Hazina wanajuaje kwamba Bureau A amebadilisha fedha? Kwenye nchi nyingine ukishabadilisha, aki-punch tu, Hazina wanajua kwamba Bureau ya Norman ameshabadilisha fedha. Tujitahidi huko ili kupata kodi stahiki, siyo kubana. Tutafunga watu wengi na tukifunga maduka haya mengi, maana yake tutapoteza ajira nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo sasa, niiongeze tu hapo hili la kuhusu mitaji. Leo mtu anaulizwa umepata wapi shilingi milioni 300 za kufungua Bureau De Change? I keep on asking myself, hili swali linaisaidia Serikali kupata mapato? Sielewi!

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri, juzi tarehe 4 Mei, 2018 nilikwenda kwenye Mkutano wa Uwekezaji pale Dubai. Niliyeambatana naye alikuwa ni rafiki yangu mfanyabiashara wa nchi jirani, alikuwa na cash money dola 400,000. Alipofika Dubai alipoambiwa a-declare akasema 400,000 USD. Pale pale wakampa pass ya VIP na kumwambia Sir, do you want us to facilitate your protection while in Dubai? Unataka tukulinde ukiwa hapa? Akasema hapana, I am comfortable. Je, unapenda tujue hoteli unayofikia? Akasema ndiyo, akataja hoteli yake. Akapewa heshima tofauti na Norman Sigalla King aliyekuwa na Dola 350 za kulipa tu hoteli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii nini maana yake? Maana yake ni kwamba mwekezaji anapoleta fedha, it is immaterial kuhoji ametoa wapi? Ametumiaje ni sahihi kuuliza. Ndiyo maana kwenye mchango wangu mwingine nimesema, mtu kama anataka kuangusha Serikali yetu, huyo mfuatilieni. Dunia ya leo unaweza uka-track matumizi ya fedha bila kunihoji kabisa. I will feel comfortable kwamba this is the correct avenue ya ku-invest. Nitasema hapa ndiyo mahali pa kuwekeza, kwa nini? Siwi disturbed, sisumbuliwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana tufuatilie matumizi ya fedha wanazoingia nazo watu. Kwa vyovyote vile fedha ni jambo la msingi zikiingia kwenye nchi yetu isipokuwa matumizi yake ndiyo yanaeleza ushetani wa fedha. Sisi Wachungaji Makanisani huwa tunapokea kila sadaka bila kuuliza inakotoka kwa sababu ni matumizi ya hela ndiyo yanayoeleza uovu wa mwenye hela na siyo vinginevyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili la haraka haraka ni sekta ya kilimo. Sekta ya kilimo ndiyo uti wa mgongo kwa Watanzania. Kwenye bajeti ya rafiki yangu Mheshimiwa Dkt. Mpango anaeleza wazi kwamba asilimia 66 ya Watanzania wanategemea kilimo. Ombi langu, moja, tuanzishe kiwanda cha kutengeneza mbolea ambayo itakuwa branded kutoka kwenye uzalishaji kwamba this is not for export, ni kwa ajili ya wakulima wa Tanzania na mfuko wake ni Sh.20,000 kwa yeyote anayetaka, bila kuweka categories.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, NFRA kwa jinsi ilivyoanzishwa, bahati nzuri ni part ya andiko langu ndiyo lililoanzisha NFRA. Anayependa asome kitabu changu kinachosema ‘Maendeleo ni Vita, tufanyeje’. Tulichopendekeza ni kwamba NFRA ipewe fedha nyingi za kutosha ili i-act kama backup ya wakulima wanapokuwa wamelima mahindi, wawe na assurance ya price, wajue bei yake kwamba naenda kukopa benki kwa sababu najua kilo moja ya mahindi ni shilingi fulani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu kwa Serikali, afadhali Serikali ipoteze shilingi bilioni 30 au shilingi bilioni 40 kwa kuwagawia wakulima waliolima kiukweli kuliko vinginevyo. Naiomba sana Serikali, fedha za kununulia mazao kama ya mahindi zipelekwe kwa wingi na tulazimishe wafanyabiashara wote kununua NFRA au kama hiyo Tume ya Mazao au whatever wanunue huko, lakini kwa mkulima tu-ensure price yake kwamba the minimum price you will get is this much, kwa hiyo, tupeleke fedha kwenye eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwa haraka kwenye huduma za afya. Sasa hivi tunajikita kwenye kupeleka madawa, naomba sana Serikali ibadili sura. Sasa tupeleke elimu kwenye kula vyakula bora. Mwezi uliopita tumekwenda Korea, tulikuwa tunakohoa tukauliza kwa mtu mwenye miaka 74 kama anaweza kutuonyesha kituo cha afya kiko wapi, anasema hafahamu kituo cha afya popote. Tukamwuliza, kwa nini? Akasema sijawahi kuugua, kwa hiyo, hajui lakini siri ni aina ya vyakula anavyokula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unafahamu, leo hii tunagombania sukari, tunaongelea habari ya mafuta, nchi za wenzetu, mafuta yanayoitwa sijui mawese na mafuta yoyote ya kupikia kwao zilipendwa. Hakuna wanaotumia mafuta hayo sasa, yanarushwa kwetu nchi changa. Kwa nini? Kwa sababu wanajua kuwa ni madhara kwenye afya zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nihitimishe na jambo la pili kutoka mwisho kuhusu umuhimu wa kutekeleza Mradi wa Stiegler’s, chonde chonde, naiomba Serikali yangu ya CCM, mradi wa Mchuchuma na Liganga upewe kipaumbele.
Nilisema wakati…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. PROF. NORMAN A.S. KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema wakati fulani hapa kwamba ndiyo mradi pekee ambao Tanzania ina hakika kwamba utalipa fedha tulizowekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante.