Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Neema William Mgaya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba hii ya bajeti. Kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Mpango na Mheshimiwa Dkt. Ashantu kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Wizara yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze tu kwa kusema bajeti hii ni nzuri kwa sababu imejikita katika kuhakikisha kwamba inalinda viwanda vyetu vya ndani lakini vilevile imeweka urahisi wa kuanzisha viwanda vipya. Kwa mfano, tuna zero rate katika viwanda vinavyozalisha mafuta ya kula na mafuta haya ya kula yanatumia malighafi ambayo tunalima ndani ya nchi yetu ikiwemo michikichi, alizeti na parachichi kule Mikoa ya Njombe na Iringa. Naishauri Serikali iangalie upya Sera ya Viwanda na Uwekezaji ili tuweze kuwa na viwanda vidogo, viwanda vya katina viwanda vikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naiomba Serikali iweke mkazo katika kuhakikisha kwamba tunajitosheleza kwa kuwekeza kwenye viwanda ambavyo vinazalisha malighafi ili iweze kutumika katika viwanda vikubwa. Kwa vile viwanda ambavyo vinazalisha malighafi vitumie malighafi ambayo zinatokana na mazao yetu humu nchini kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nasema hivyo? Tunaweza tukatoa mfano tukawa na viwanda vinavyochambua mbegu na pamba, kiwanda hicho kinachochambua mbegu kinaenda kutumika kama malighafi kwenye kiwanda ambacho kinatengeneza mafuta. Hali kadhalika ile pamba inaenda kutumika kama malighafi kwenye viwanda ambavyo vinatengeneza majora ya nguo na majora ya nguo yanaenda kutumika kama malighafi kwenye viwanda ambavyo vinatengeneza suruali, sketi, mashati na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie mifumo ya upatikanaji wa mapato kwa kutumia teknolojia ya IT. Mheshimiwa Waziri katika kitabu chake cha bajeti amesema kwamba tutaendelea kuendeleza mifumo ya upatikanaji wa mapato kwa kutumia teknolojia ya IT. Ni jambo jema lakini nilitaka kumwambia Mheshimiwa Waziri ili kuendana na mifumo hiyo katika suala zima la ukaguzi ni vyema Serikali ikaweka mkazo kuhakikisha wakaguzi wetu wa ndani na wa nje wanaenda sambamba na teknolojia hiyo ili kuweza kuwasaidia kipindi cha ukaguzi. Kwa sababu kama ukaguzi hautaendana na mifumo hiyo, utatokea udanganyifu mkubwa kipindi cha ukaguzi. Hivyo basi, Serikali ione umuhimu kwa Internal na External Auditors wetu waweze kupata elimu hii ya teknolojia mpya katika mifumo ya ukusanyaji wa mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nasema hivyo? Nimepitia taarifa ya ukaguzi ambayo ilifanywa na Mkaguzi wa Nje, Eng. Maganga Machi, 2018, katika Halmashauri ya Misungwi. Katika mambo ambayo amegundua Mkaguzi huyu kulikuwa na baadhi ya mashine za kukusanyia ushuru ambazo hazikuunganishwa kwenye mfumo zaidi ya miaka miwili. Kutokana na kutokuunganishwa huko kwa mashine hizo za kukusanyia ushuru kwenye mifumo kumesababisha kupotea kwa pesa nyingi ndani ya halmashauri hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tujiulize, wale Wakaguzi wa Ndani wanafanya ukaguzi katika halmashauri kila baada ya miezi mitatu kwa mwaka (quarterly) na muda wa miaka miwili mashine hizo za POS hazikuunganishwa na mfumo na wao wamekuwa wakikagua ndani ya miaka miwili ina maana wamekagua zaidi ya mara nane ndani ya miaka miwili bila kugundua kwamba kuna pesa zinaibiwa mpaka alipokuja External Auditor kutoka Mwanza na kugundua kwamba kuna tatizo hilo na kuna pesa ambazo zimeibiwa kwa sababu tu ya hizo Point of Sale Machine hazijaunganishwa na mfumo ili kuweza kusaidia ukaguzi wa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la gawio la asilimia 5 kwenye halmashauri zetu. Kwanza niipongeze Serikali kwa kuondoa riba katika gawio la asilimia tano kwa wanawake na vijana kwenye halmashauri zetu. Naiomba Serikali pesa hizo zitoke kwa wakati ili ziweze kwenda kuwasaidia wanawake pamoja na vijana kwenda kufanya maendeleo na vilevile kukuza uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye sanitary pads, niwapongeze kwa kuondoa kodi katika suala zima la uingizwaji wa sanitary pads. Hata hivyo, nilitaka nimkumbushe Mheshimiwa Waziri tuna viwanda vya ndani ambavyo vinatengeneza sanitary pad na lengo letu ni kuvikuza viwanda vyetu vya ndani viweze kufanya kazi vizuri lakini ukiangalia hii kodi iliyoondolewa kwenye hizi sanitary pads imewa-favor wale watu wanao-import hizo sanitary pads. Hivyo basi, naishauri Serikali iangalie ni jinsi gani inaweza ikapunguza kodi kwenye malighafi ambayo inatumika kutengeneza sanitary pads ndani ya nchi yetu ili hivi viwanda vya ndani viweze ku-compete na zile sanitary pads zitakazokuwa zinaingia ndani ya nchi yetu, ziweze kushindana vizuri kwenye soko nao waweze kuuza kwa bei ya chini ili ile azma yetu ya kuwasaidia watoto wetu wa kike katika suala zima la kupata sanitary pads kwa bei nafuu tuweze kulifikia. (Makofi)

Mheshimia Naibu Spika, mwisho kabisa nipongeze kwa msamaha wa penalty na interest ambayo mmetoa kwa muda wa miezi sita. Mimi nashauri muongeze muda iwe mwaka mmoja ili kuweza kuwa-motivate wafanyabiashara wetu waweze kufanya biashara vizuri na kwa kujiamini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.