Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Julius Kalanga Laizer

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Monduli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Spika, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nitasemea maeneo machache na nianze na suala la viwanda. Hakuna mtu ambaye anapinga suala la ujenzi wa viwanda kwa sababu inatusaidia kukuza uchumi kama Taifa, lakini kuondokana na tatizo la umaskini kwa mwananchi mmoja mmoja. Hoja yetu hapa ambayo tunataka Waziri wa Fedha atuambie, hivi lengo la viwanda hivi tunavyojenga ni kwa ajili ya nani, tunajenga viwanda hivi ili tuwe na viwanda vingi katika Taifa hili au tunajenga viwanda ili tuwasaidie wananchi wetu kuondokana na umaskini katika Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siyo mara ya kwanza nchi hii kuwa na viwanda, lakini vimekufa si mara ya kwanza nchi hii kuwa na ndege lakini zimekwisha, kwa hiyo suala siyo kuwa na miradi mikubwa, suala ni kuwa na miradi mikubwa lakini endelevu (sustainable development project). (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mpaka leo miaka mitatu tunaimba sera ya viwanda lakini hakuna hand out guideline ya nchi inayoeleza muktadha mzima wa viwanda vitakavyosimamiwa nchi hii. Hivi akiondoka Rais huyu akaja Rais mwingine hili suala la viwanda si limekufa? Kama tuna millennium ya 2025 kwa nini tusingekuwa na program ya Taifa kama Taifa ambapo kila mwananchi na kila sehemu anayo inayoonesha namna suala la viwanda vitakavyoendelezwa katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, huwezi kuendeleza viwanda kama hauna kodi stahiki ambazo zinasimamiwa kwa muda fulani ambao mwekezaji atawekeza, tunabadilisha kodi kila mwaka tunafanya trial and error ile tunayosoma kwenye biology kwamba unatengeneza kaboksi halafu panya anaenda huku anakosa mlango, anaenda anakosa mlango, ndiyo maana kila mwaka wanarekebisha Sheria ya Kodi, kila mwaka wanakuja wanasamehe kodi hii, wanaanzisha kodi hii, kwa nini tusingekuwa na program ya nchi inayoonesha kwamba ni kodi gani tuache kwa sasa ili tu-invite wawekezaji halafu watu waweze kuwekeza, lakini wanafanya uwekezaji hawaja-base katika rasilimali watu.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia katika bajeti ya Mheshimiwa Waziri, hakuna mahali popote Wizara inazungumza habari ya ujenzi wa vyuo vya kati ili vijana wetu wanaomaliza form four waweze kupata ujuzi waende wakafanye kazi kwenye viwanda vyetu. Ndiyo maana watajenga viwanda lakini wataanza kuomba vibali vya kupata expert kutoka nje kuja kufanya kazi katika viwanda vya nchi yetu kwa sababu hatujawaandaa vijana kufanya kazi katika viwanda. Maana yake viwanda tutakuwa tunajenga kwa ajili ya watu wengine lakini siyo kwa ajili ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nilikuwa nasema asubuhi nchi hii inazalisha zaidi ya vijana laki tatu wa kidato cha nne kila mwaka ambao hawaendelei na kidato cha tano. Waziri wa Elimu amenijibu kisiasa kwamba wataenda kwenye Vyuo vya Ualimu ambapo wanaenda lakini hawaajiri na wao sera ya elimu wanasema kuanzia miaka ijayo wanafuta kidato cha nne kuanzia sasa shule ya msingi zinafundishwa na watu wenye Diploma, hivi mtu aliyemaliza form four anaweza kusoma Diploma kwa kuunganisha au mpaka aende Certificate? Kwa hiyo ni muhimu tuwe na viwanda ambavyo tumeandaa vyuo vya kati na vya juu vinavyoandaa vijana wetu kwenda kufanya kazi katika viwanda tunavyovijenga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu rasilimiali kwa maana ya malighafi, hakuna muunganiko kati ya viwanda, kilimo chetu na mifugo yetu. Bajeti mbili zimepita tu hapa kwa mbinde, tena baada ya kwenda kukaa party caucus Bajeti ya Kilimo, na bajeti ya Mifugo na Uvuvi, lakini walitupa matumaini na Kiti cha Spika kilitupa matumaini kwamba wakati wa Bajeti Kuu Serikali ita–subsidize kule ambavyo tulikuwa tumelalamikia katika kupeleka ruzuku na katika kusaidia uwekezaji katika sekta ya kilimo na mifugo.

Mheshimiwa Spika, nimesoma kitabu hiki hakuna, hakuna amendment yoyote ya kuiongezea bajeti Wizara hizo, hivi Waziri wa Kilimo atafanyaje kazi, Waziri wa Mifugo atafanyaje kazi kama hana fedha. Kwa hiyo ni muhimu kama kweli wangekuwa wanatujali na wanataka kuunganisha Sekta ya Mifugo, Kilimo na Viwanda wangeleta bajeti ambayo itasaidia kule wakulima wetu walime kisasa. Haiwezekani ukajenga kiwanda cha kutegemea kilimo cha msimu, kwamba unasubiri mvua inyeshe halafu mwenye kiwanda afunge kiwanda kwa sababu hamna mazao kwa ajili ya kuendesha kiwanda. Ni lazima tuwe na sustainable projects ambazo mwekezaji wa kilimo akiwekeza awe na uhakika wa kupata raw material mwaka mzima bila ya kutegemea mvua ambayo hatujui kama inanyesha au hainyeshi, miradi hiyo iko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hu ni mwaka wa tatu Serikali iliahidi kuleta miradi ya kimkakati ambapo mpaka sasa tunavyoongea siyo Liganga siyo Mchuchuma siyo Engaruka siyo General Tyre hata mmoja hauja-mature. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, agizo la Serikali tangu tunaanza Bunge hili ni kwamba tutakuwa na miradi hiyo ya kimkakati, Liganga na Mchuchuma tulikuwa tunasikia tukiwa nje ya Bunge tumekuja ndani ya Bunge, mpaka leo hawajatekeleza. Miaka mitatu hii hata Watumishi wameshindwa kuwapandishia mishahara halafu wanasema wana-control inflation hawaja-control inflation imeji-control yenyewe kwa sababu purchasing power hakuna, wananchi hawana fedha, kwa hiyo kama hawana fedha huwezi kupima inflation kwa sababu hakuna mtu anayenunua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Serikali ituambie, kwa sababu uchumi wa nchi hii hauwezi kujengwa na kila mtu kuwa mtaalam katika eneo lote. Tunataka kama tuna maono ya kuwa na viwanda, tuwape wataalam watuandalie programu ya kuwa na viwanda katika Taifa hili. Tuache hizi kauli za kisiasa za kutetea kitu ambacho hatuoni, tunatamani kama ni viwanda kila mtu aone, siyo wanatuletea vile viwanda 3,600 kwenye makaratasi, lakini mnatuambia tu, tupelekeni site hamna ujasiri huo, kwa nini? Kwa sababu wana-politicize miradi mingi badala ya kuangalia uhalisia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala siyo kuwa na viwanda vingi, suala ni kuwa na viwanda vinavyosaidia kubadilisha maisha ya wananchi. Hata kama tungekuwa na kiwanda kimoja, kinachobeba mazao yote ya wakulima wetu, hicho kiwanda ni bora, kuliko kuwa na viwanda 100 ambavyo vyote malighafi unaagiza kutoka nje. Kwa hiyo ni muhimu tuwe na lengo la Taifa kusaidia wananchi katika miradi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme jambo lingine, historia inaonesha Serikali zinapita, Serikali iliyopita ilikuwa inasema Kilimo Kwanza, imemaliza imeondoka, imekuja Serikali ya viwanda. Kilimo Kwanza hatujafanya na tungefanya Kilimo Kwanza viwanda vingejengwa automatically kwa sababu raw material zingepatikana vya kutosha na watu wangejenga. Mpaka leo hakuna mkakati wowote Serikali imewekeza katika kusaidia kilimo.

Mheshimiwa Spika, naomba nishauri mambo machache, ni muhimu Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Mpango kama anataka kusaidia Taifa hili, Serikali ilete mpango mkakati wa kusaidia sekta ya kilimo katika nchi hii ili iweze kuzalisha kwa tija. Kwa sababu mazao si mazao tu lazima mazao yawe na ubora unaostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, umefanya hii kazi kwenye industry ya utalii, ukiiangalia Arusha yote na Kaskazini ambavyo tuna utalii wa kutosha, lakini tunaaagiza nyama kutoka Kenya, tunaagiza material ya kwenye hotel, hata nyanya kutoka nje, ni kwa sababu uzalishaji wetu hauna viwango. Kwa hiyo siyo kuzalisha nyanya tu, siyo kuzalisha matunda tu ni lazima tuzalishe katika ubora unaostahili.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.