Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Amb. Adadi Mohamed Rajabu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Spika, nami nashukuru sana kwa kupata nafasi hii ya kuchangia hoja hii ambayo ni muhimu sana ya Hali ya Uchumi na Mpango wa Maendeleo pamoja na Bajeti ya mwaka 2018/2019. Kwanza nampongeza sana Waziri wa Fedha, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu, Wakurugenzi wote na Watendaji wote wa Wizara ya Fedha. Najua kazi kubwa wanayo, lakini kutuletea bajeti hii ni kitu kimoja ambacho wamefanya usiku na mchana na kwa kweli bajeti imeonekana na ni nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Rais hasa kwa kipindi hiki kifupi cha miaka miwili na nusu kuweza kuja na miradi mikubwa, ya kisasa na ya kileo ambapo kwa kweli miradi hii itakapomalizika, naamini kabisa kwamba uchumi wa nchi yetu utakuwa mkubwa sana. Miradi hii imeorodheshwa vizuri kabisa. Miradi kumi ambayo ameiorodhesha Mheshimiwa Waziri kwenye kitabu chake cha mpango ambayo ukianzia na reli, mambo ya ndege, mambo ya bomba la mafuta, umeme, Mkulazi na kadhalika, ni mizuri sana na imechukua matrilioni ya hela, lakini hii itakuwa ni historia ambayo Awamu ya Tano itaiweka katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bajeti hii ni ya tatu ya Awamu ya Tano. Kwa kweli ukiiangalia bajeti hii ni nzuri sana na imelenga hasa kulinda viwanda vya ndani. Mheshimiwa Waziri ameeleza kwenye hotuba yake hapa, ameongeza kodi nyingi sana kwa bidhaa ambazo zinatoka nje kwa ajili ya kuingia ndani. Kwa kweli tunampongeza sana kwa sababu kutoka page 48 - 52 ameorodhesha bidhaa zote hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Waziri na hii ni hatua nzuri ambayo inaonekana kutoa mwanya sasa kwa wawekezaji kuweza kuweka viwanda hapa nchini, kuongeza ajira na kufanya mambo mengi ili ku-discourage importation kutoka nje. Suala hili la ku-discourage importation kutoka nje lilifanyika na nchi nyingi tu; India wanafanya sana, hawataki bidhaa kutoka nje au vitu kutoka nje na wanatumia vitu vyao vya ndani, South Afrika na nchi nyingine nyingi. Kwa hiyo, hii ni hatua na mwenendo mzuri sana ambao naamini kabisa utatupa faida sana kwenye hii nchi.

Mheshimiwa Spika, napenda sasa nianze kuchangia pia kwenye mambo ya mfumo mpya wa kodi za Electronic (Eletronic Tax Stamp - ETS). Mpango huu ni mzuri sana na ni mpango ambao unatutoa kwenye manual system na unatupeleka kwenye electronic. Ni mpango ambao utaweza kujua ni bidhaa gani zinazalishwa na kupata takwimu sahihi ambazo zinatoka kwenye viwanda.

Mheshimiwa Spika, mpango huu pia wameuchukua kwenye nchi nyingi ambazo wamewahi kufanya. Wameuchukua kutoka Kenya, Morocco, Uturuki, Malaysia na Switzerland. Nchi zote hizo ambazo zimechukua mpango huu, wamekwenda kwenye mambo ya sprits; bia, vinywaji vikali na sigara. Sasa sisi mpango huu tumejumuisha vinywaji vikali, bia, sigara, maji na soft drinks. Kitu ambacho nina wasiwasi na Kamati ina wasiwasi ni kwamba huenda tukaweka burden kubwa sana kwa mnunuaji, mtumiaji wa vitu hivi.

Mheshimiwa Spika, naona kwamba mpango huu ni mzuri na unatakiwa uanze mara moja, lakini ni vizuri Wizara ikajitathmini kwamba itakapochukua vitu vyote hivi in totality hasa maji na soft drinks, huenda mzigo mkubwa ukaenda kwa mtumiaji. Ni vizuri iangalie kwa makini kwa sababu siyo ajabu kwa mpango huu vitu hivyo vikaongezeka bei, ingawa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri amesema kwamba bei hazitaongezeka kwenye bidhaa hizo, lakini nina uhakika kwamba wataongeza bei hapa. Kwa hiyo, naomba aangalie vizuri sana.

Mheshimiwa Spika, la pili, mpango huu, hiyo Kampuni ya SCIPA ambayo imepewa imeonekana kwamba itakuwa self financing, lakini sidhani kama itakuwa self financing. Hakuna biashara ambayo inafanyika bila kupata faida.

Mheshimiwa Spika, ni bahati mbaya tu kwamba vitabu vya hotuba yetu havijafika, lakini kuna mchanganuo ambao umetoa na unaonekana kwamba huenda kampuni hii ikapata faida kubwa sana. Wasiwasi uliopo ni kwamba, kampuni hii tumeipa miaka mitano. Kwa nini tuipe miaka mitano? Kwa nini tusipunguze? Tumeweka mkakati gani wa kuweza kuangalia kwamba tutafanya vipi kuweza ku-train watu wetu ili baada ya huo muda tuweze kuendelea wenyewe na huo mpango? Kwa hiyo, niliona tujaribu kuangalia hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine nataka tuangalie system hii ya Akaunti Jumuifu ya Hazina (Treasury Single Account). Tumekwenda vizuri sana kwenye Mifuko. Mfuko wa Maji umekwenda vizuri sana na umesaidia sana, kwa sababu ulikuwa ring fenced kwamba huruhusiwi, umezuiwa na Hazina walikuwa wamefanya vizuri sana wanapopata fedha zile moja kwa moja wamezipeleka kwenye maji na umesaidia sana kuleta maendeleo ya maji na miradi mingi ya maji. Hii ni pamoja na REA na barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hivi tumekwenda tunataka tuanzishe hii Treasury Single Account, kwamba sasa hii Mifuko yote inaweza kufa. Itakapokufa, majukumu yote yanakuwa kwa Wizara. Sasa hii ni issue ambayo ni muhimu sana Waheshimiwa Wabunge tuiangalie. Kweli Wizara imejitayarisha kupokea hela zote na kuhakikisha inazigawa hela zote kwa wakati? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hapa ni muhimu sana kuangalia; Wizara imejitayarisha namna gani? Ni vizuri kama wanajitayarisha, wajitayarishe kwa E-system ili kuweza kutoa hizo fedha kwenye maendeleo. Kwa sababu kuna miradi mingi ambayo imeshaanza, imetiwa saini, lakini hakuna uhakika wa kwamba hii system itakapoanza wakati huu, hiyo miradi itaendelea namna gani?

Mheshimiwa Spika, hapa tunaona hela za maendeleo zimechelewa sana kupelekwa kwenye mikoa. Sasa tunakuja kwenye E-system, hii miradi ambayo tumeshasaini mikoani itakuwaje? Ni vizuri Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind- up aweze kutoa ufafanuzi wa hili suala kwa sababu ni muhimu sana na nashauri kwamba tujitayarishe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ni suala la PPP. Ni muhimu sana kitengo hiki kikaimarishwa kwa sababu miradi mingi na mikubwa, ni vizuri ikafanyika kwa njia hii. Naamini kabisa ile miradi ambayo feasibility study imeshafanyika, basi itangazwe. Itakapotangazwa, nina uhakika wawekezaji watatokea. Tumefanya hivyo kwenye hivi viwanda vya madawa na watu wengi wametokea. Sasa hii miradi mingine, kwa mfano road toll, barabara ya Ubungo - Dar es Salaam – Morogoro, Mheshimiwa Spika, kwa nini tusiingie kwenye road toll? Ni kitu cha muhimu sana, naomba sana tuangalie. Au feasibility study ya reli ya Tanga, imeshamalizika, kwa nini wasiitangaze sasa wawekezaji watokee? Naamini kabisa kwamba tutakapochukua uamuzi huu, mambo haya yataweza kwenda kwa haraka sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, kuna suala moja ambalo sekta binafsi inalalamika sana kuhusu malipo yao ya fedha za VAT. Wanadai shilingi bilioni 600, haya mambo ya wawekezaji kwenye mambo ya sukari. Naamini kabisa Serikali italiangalia kwamba umechukua hizi hela 15%, basi hakikisha unazirudisha kama ambavyo umeamini.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, mengine nitaandika, nakushukuru sana kwa muda huu.