Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nakushukuru sana kunipa nafasi niweze kuchangia kidogo kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, hotuba ya Serikali ambayo iko mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye vitabu vyote vya Mheshimiwa Waziri; kitabu cha hotuba hata kitabu cha hali ya uchumi wa Taifa, uchumi wa Tanzania umekua kwa asilimia 7.1 tofauti na mwaka 2017 ambapo ulikua kwa asilimia 7 mwaka 2016. Ukijaribu kuangalia hivi vitabu vinavyosema na ukienda kwenye actual ground kule chini kwenye maisha ya watu ni tofauti sana. Uchumi tunaosema kwamba umekua kwenye vitabu kule chini bado hauendani. Nami nakubaliana kabisa na hotuba ya Kamati kwamba tumeshindwa kuoanisha uchumi na hali ya wananchi kule chini, tumeshindwa kuoanisha kukua kwa uchumi kwa kufungamanisha na hali ya maisha ya Watanzania kule waliko chini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi tunavyoongea kilo ya dagaa Sh.10,000 tena wa Mwanza. Hivi tunavyoongea jana sato Sh.10,000 kilo moja hata hapa kantini tunakula haijalishi ni mdogo au mkubwa. Ukiondoa mazao ya nafaka, mazao mengine yote gharama ni juu. Kwa hiyo, kwa mwananchi wa kawaida ukimwambia uchumi umekua hakuelewi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tukienda pia kwenye vifaa vya ujenzi, cement wiki iliyopita ilikuwa Sh.14,500 leo asubuhi ni Sh.15,500. Sasa uchumi umekua umekuaje? Miezi miwili iliyopita nondo milimita 16 ilikuwa Sh.19,500 mpaka Sh.20,000 leo nenda duka la dawa vifaa vya ujenzi ni Sh.38,000 imepanda almost mara mbili. Nashindwa kuelewa, mimi siyo mchumi ni mtu wa maliasili na mazingira, Waziri atuambie uchumi ukikua unaupima wapi? Unaupima juu au kule kwa wananchi walioko kule chini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali lazima tuhakikishe kukua kwa uchumi kunaendana na hali kule chini. Hivi tunavyoongea watu wanazidi kuuza mashamba na viwanja vyao, mabenki yanatangaza kila siku kapiga minada nyumba za watu, watu wameacha kukaa kwenye nyumba zao walizokuwa wamejenga wameziuza wameenda kupanga nyumba, sasa hii kusema uchumi umepanda umepandaje? Kiukweli kusema uchumi umepanda wakati hatuuoni huko chini tunaoishi na wananchi bado kuna walakini mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni uzalishaji wa mazao. Ukienda kwenye Kitabu cha Hali ya Uchumi kwenye page 134, kuna baadhi ya mazao ambayo siku za nyuma ndiyo yalisaidia uchumi wa Taifa hili kukua ikiwemo kahawa, pareto, katani, tumbaku, mkonge, pamba, korosho na chai . Leo ukisoma kitabu kinasema mazao haya yamepungua tena kwa asilimia kubwa na sababu zilizotolewa hapa ni kwamba, kwanza mvua za kutosha zimekosekana lakini pili, wakulima wameshindwa kununua pembejeo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumzia habari ya uchumi wa viwanda, bado tunategemea mvua ambazo hazina uhakika. Hatuwezi kuzungumzia uchumi wa viwanda wakati mazao ambayo yalikuwa yanainua uchumi wa Taifa hili, ukisikia Kagera wameendelea ujue ilikuwa ni ndizi na kahawa; Kilimanjaro wameendelea ni kahawa, kule Mbeya cocoa, Tanga viwanda vilikuwa zaidi ya mia ni katani ilisaidia sasa leo yale mazao hayapo, yamekuwa ni mapori, tunazungumzia habari ya uchumi wa viwanda, vinatoka wapi hivyo viwanda? Kwa hiyo, tukitaka kwenda kwenye uchumi wa viwanda lazima tujizatiti kwenye kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikubaliana miaka mitano iliyopita kwamba tutahakikisha tuna angalau hekta 1,000 za umwagiliaji. Kwenye hotuba ya Waziri wa sekta nilisoma mpaka sasa hivi ni hekta 460,000 hata nusu kwa miaka mitano hatujafika, hatuwezi kwenda na leo tena mabadiliko ya tabianchi, global warming na mambo mengine mengi. Kwa hiyo, hatuwezi kwenda kwenye uchumi huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sababu ya pili tumeambiwa ni wakulima kushindwa kutumia pambejeo. Zao kama kahawa leo ukisema mkulima anunue pembejeo hawezi, ni very expensive. Kwa hiyo, kwenye mzao kama haya lazima Serikali itoe ruzuku kuwaachia wakulima ni vigumu. Wengine wanang’oa wanapanda maharage, migomba kwa sababu hawawezi kuendelea kumudu kununua pambejeo. Kwa hiyo, naomba tuangalie hisotoria ya nyuma, Mwalimu Nyerere alifanya kazi kubwa sana, mazao ambayo ndiyo yalikuwa kielelezo cha Taifa letu tusiyaache. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hata kwa mazao ambayo yapo sasa hivi, kwa mfano, suala la tumbaku Mkoa wa Tabora tunalima lakini bado wakulima wake wameendelea kuwa maskini. Bei za mazao yetu bado ni tatizo. Hivi navyoongea masoko ya jana na juzi bei imeshuka kutoka Sh.4,000 mpaka Sh.4,500 kwa kila sasa wanauza kilo nzima ya tumbaku kwa Sh.181, hayo ni masoko ya jana. Sasa mkulima kama huyu ambaye amenunua pembejeo kwa Sh.90,000 mfuko mmoja wa kilo 50 mpaka Sh.140,000 kwa wale waliokosa ruzuku lakini bei ya Serikali Sh.90,000, mkulima huyu akauze tumbaku Sh.181 wakati amekwensda kukopa benki, anadaiwa kwenye taasisi za fedha, ananyanyukaje huyu? Kwa hiyo, hata kwa mazao ambayo yanasaidia bado Serikali hatujaweza kusimamia bei nzuri ya mazao yetu, hili ni tatizo kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine, Mkoa wa Tabora umelima tumbaku lakini bado kiwanda kipo Morogoro. Tumepiga kelele sana hapa kwa nini Kiwanda cha Tumbaku hakijengwi Mkoa wa Tabora? Majibu tunaambiwa kwamba tunatafuta wawekezaji lakini juzi mwaka uliopita amekuja mwekezaji wa Kiwanda kingine cha Tumbaku amejenga Morogoro. Naomba Serikali na Waziri aje na majibu, tunataka Kiwanda cha Tumbaku kiende kikajengwe Mkoa wa Tabora na mtuambie namna gani mtafanya kiwanda kile kiweze kujengwa vinginevyo kiukweli vijana wale hawana ajira lakini tumbaku inalimwa kwao tena asilimia 60 ya tumbaku ya Tanzania inalimwa pale Mkoa wa Tabora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye kitabu pia cha Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 92 utaona namna gani ambapo tunaingiza sana bidhaa ndani kuliko kupeleka nje kwa hiyo, tunauza kidogo, tunaingiza sana, hili ni tatizo. Kuna vitu vingine ambavyo hatuhitaji kuingiza kutoka nje, kwa mfano, toothpick, pamba za kwenye masikio, viberiti lakini tuna-import kutoka nje, fedha tunayokusanya tunapeleka nje kutengeneza ajira kwa vijana wao, sisi tunabaki ni masoko ya bidhaa za wenzetu, hatuwezi kupiga hatua, hili ni tatizo kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Tabora tunalima mbao, tena quality mbao, mninga na mpogo safi unaupata Tabora. Serikali ilisema itahakikisha samani zote za Serikali zinatoka ndani ya nchi lakini leo tunapeleka magogo, mbao, Wachina wanakwenda kuchukua, tunakwenda kununua bidhaa za Kichina very weak, hazina ubora kwa gharama kubwa. Kwa nini Serikali inashindwa kusimamia vitu ambavyo tunaweza kutengeneza hapa ndani ya nchi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi kweli kwa ule Msitu wa Sao Hill pale Iringa, kuna haja ya kwenda kununua kiberiti nje? Hata mtoto wa darasa la saba anatengeneza kiberiti, hata mtoto wa darasa la pili anatengeneza toothpick, tunayo pamba, vitu vingine ni sisi tunajitakia. Fedha ambayo tunaipeleka nje inakwenda kujenga kule nje kumbe tunaweza tukaitumia ndani ya nchi yetu ikazunguka humu humu, tuka-invest ndani ya nchi yetu. Kitendo cha Serikali kuruhusu hata vitu vidogo vidogo vikaingizwa ndani ya nchi ni kushindwa kusimamia nchi yetu lakini pia ni kushindwa kusimamia namna gani vijana wetu wapate ajira, tuna- create ajira kwa Wachina na kwa wengine huku vijana wetu wakiwa watanga tanga bila ya kuwa na ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.