Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Masoud Abdalla Salim

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtambile

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru, kama Serikali inataka kuambiwa ukweli ili ijirekebishe bajeti ya 2018/2019 ni bajeti ya kuwadanganya Watanzania, ya kufikirika, ya kusadikika na isiyo tekelezeka. Ni bajeti ambayo kwa kweli imewahadaa Watanzania na hasa wakulima. Ikiwa leo wakulima wametengewa asilimia 0.4 ya fedha za maendeleo ndani ya fedha za bajeti ya maendeleo ya shilingi trilioni 12 ukiachia shilingi trilioni 2.1 fedha za nje, hivi Tanzania ya viwanda kuelekea uchumi wa kati ni kweli inawezekana? Mnawadharau wakulima tangu bajeti iliyopita mwaka 2017/2018 walitengewa shilingi bilioni 150.2 mkapeleka shilingi bilioni 16.5 hadi mwezi Machi sawa na asilimia 11, Tanzania ya viwanda iko wapi? Mmewatelekeza wavuvi, leo wavuvi bajeti ya maendeleo kwa mwaka huu mmetenga 0.06 ndani ya shilingi trilioni hizo ambazo nimezitaja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli Serikali kama inataka kuambiwa ukweli ni kwamba wavuvi wametelekezwa, wakulima wametelekezwa na mifugo imetelekezwa. Sasa nauliza mkakati wenu wa Serikali wa kuboresha uvuvi uko wapi, hauonekani. Wananchi wa Mtwara, Lindi, Dar es Salaam mpaka Tanga mkakati wa kuboresha maisha yao uko wapi? Kwenye maziwa nako vilevile, Mikoa ambayo iko katika Ziwa Viktoria, Ziwa Tanganyika na maziwa mengine, yote hakuna mkakati, bajeti yao ni 0.06 ya fedha za maendeleo, ina maana Serikali haina mkakati. Mkakati mkubwa unaojulikana ni kuchoma nyavu moto na kupeleka wapimaji wa samaki kantini, tutafika kweli? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nashangaa kweli kweli, ukiangalia Vote 99, Ministry of Livestock Development and Fisheries Livestock, Subvote 1001, item 22010 Travel-In-Country, hii ndiyo Waziri mwenyewe, wametoka kwenye Sh.108,960,000 hadi shilingi milioni 300 safari za ndani kumbe ni za kuchoma nyavu moto na kupima kantini samaki wa Bunge. Hili halikubaliki lazima tubadilike tuendane na wakati ulivyo kwamba wavuvi mmewaacha kuendelea kuwa maskini, nchi nyingine duniani wanaandaa mazingira mazuri kuwawezesha wavuvi wadogo wadogo kutafuta vyombo mbalimbali baadaye wanakwenda kuvua bahari kuu na Serikali inapata mapato, lakini nyie mkiambiwa mnasema sisi siyo wazalendo, hatuwezi kufika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nigusie jambo lingine, nimesema bajeti hii ni kiini macho, ni kizungumkuti kwa sababu kwenye ukurasa 78 hakuna uhalisia wa ukweli wa matumizi ya lazima yanayoendana na mapato. Deni la Taifa ni shilingi trilioni 10 kwa hivyo kwa kila mwezi zinatakiwa zipatikane shilingi bilioni 833, ukienda kwenye mishahara shilingi trilioni 7.4 kwa kila mwezi lazima zipatakine shiling bilioni 617, matumizi mengineyo ni shilingi bilioni 3, kila mwezi ipatikane shilingi bilioni 254, shilingi trilioni 1.7 mtaipata wapi na hamna makusanyo? Tukisema vyanzo chukueni vyanzo hamtaki, hamueleweki. Amesema Mheshimiwa mmoja pale Mheshimiwa Mgimwa, kwamba Waziri usiwe mgumu ukubali ushauri wa Waheshimiwa Wabunge. Ikiwa makusanyo ya mwisho ni shilingi trilioni 1.2 mpaka 3, leo mnataka ipatikane shilingi trilioni 1.7 ya lazima, hamna kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tena basi angalia ukurasa wa 74 wa kitabu chao kuna shilingi trilioni 12 hizi ni fedha za maendeleo ukiachia shilingi trilioni 2.1 ya fedha za nje. Bado haijakuja hapo, nazo zikusanywe shughuli iende. Ukiangalia kitabu cha Mheshimiwa Mpango na mwenzake Naibu Waziri picha ya juu hapa wanasema, uzinduzi wa mfumo wa ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielekitroniki, uzinduzi lakini hawawezi kumuonesha Rais, tena Rais yupo hapa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, muonesheni Rais vyanzo vipya vya mapato mbona hamumuoneshi? Kuna picha hapa, nawashangaa kweli kweli, andaeni mazingira, njia mpya ya mapato iko wapi, uzinduzi wa vyanzo vipya vya mapato iko wapi? Ni vilevile vya siku zote hivyo ni kuwaumiza wananchi, hamsomeki hamueleweke shauri yenu. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo linanikera Serikali hii hakuna ongezeko la mshahara, bajeti hii haijagusa kabisa wafanyakazi, hakuna nyongeza yao. Hata lile takwa la kisheria la nyongeza ya kila mwezi nalo haliko, annual increment hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo baya zaidi ni kwamba ukiangalia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali mbali na kwamba mishahara haikupandishwa, hakuna ile annual increment ile ya mfanyakazi ambayo ni ya kisheria haipo lakini hata pale wanapostaafu hawa wafanyakazi wanapunjwa, wanadhulumiwa na kunyonywa nakupa ushahidi. Ripoti ya Mdhibiti ninayo hapa, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha unaoishia 30 Juni, 2017, ukurasa wa 71 sikiliza uovu na ubaya walionao hawa jamaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa wa 71, majalada yanayokaguliwa wastaafu 406 asilimia 11 ya majalada, majalada hayo 176 yamepunjwa yakiwa pungufu kwa Sh.516,078,816. Hiyo ndiyo ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, mishahara haipandishi, hakuna ongezeko la mwaka la kisheria na wale wanaostaafu nao wanapunjwa mnataka nini kwa Mungu, mkaseme nini? Nawashangaa jamani mwogopeni Mwenyezi Mungu, nyie tumewapa kazi ya kusimamia kwamba hata wastaafu nao kumbe maslahi yao wanayopata mafao yao siyo, mwaka mbaya kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaambie Waheshimiwa wenzangu hapa kwamba jukumu mlilopewa ni kubwa sana na kama jukumu mlilopewa ni kubwa sana muandae mazingira kwamba mtende haki. Siyo hiyo tu, huu wizi na ubadhirifu katika nidhamu ya matumizi ya fedha umekuwa mkubwa sana na inaelekea kwamba Mawaziri wameshindwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kitabu hiki hapa kuna wizi na ubadhirifu unaonekana. La kwanza, naomba nianze na kwenye ukurasa wa 291 wa ripoti na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Katika ukurasa huu inaonekana kwamba hata Hazina yenyewe chombo ambacho wanakisimamia, Idara ya Hazina Fungu 21 kuna ubadhirifu mkubwa wa fedha umeonekana na wao ndiyo wasimamizi. Ukurasa wa 291 Naibu Waziri fungua uangalie lakini ukusara wa 290 pia mmepata hati isiyo na shaka, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kumbe ukiona kilemba kimeloa uchafu sijui shuka inakuwaje? Mtihani, tumewapa dhamana lakini hakuna kitu. Maisha yamekuwa magumu, mzunguko wa pesa hakuna. Mwaka 2017 baya zaidi, hii hapa hotuba ya Mheshimiwa Dkt. Mpango alituambia kwamba lengo lake ni kuwatoa wale wanaokula mlo mmoja kutoka asilimia 9.7 mpaka asilimia 5, nendeni Majimbo Wabunge wote hapa tuandae vikundi twende Mikoa yote Tanzania Bara tukachunguze wanaokula mlo mmoja wameongezeka au wamepungua?

Hali mbaya kupita kiasi. Sasa yale maelezo ambayo mnatupa siye tunayasoma na tunayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri akubali kwamba bado hali ya maisha ya Tanzania ni mbaya sana na Watanzania wana matumaini makubwa sana lakini hakuna kinachoeleweka, mpaka sasa hakuna kinachokwenda. Ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri, akae na wataalam wa kweli ambao wataweza kusadia hii Wizara angalau maisha ya Watanzania yabadilike lakini kwa hali tunayokwenda nayo Watanzania tumepigika. Bajeti hii ni mbaya, mbovu, ya kusadikika, funika kombe.