Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Lucy Simon Magereli

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru nami kupata fursa kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali mwaka 2018/2019. Nianze tu kwa maelezo ya awali ambayo ningetaka niyaweke katika utaratibu ambao tumeutumia wakati wote kama Wabunge wa Kambi ya Upinzani, kama Kamati za Bunge tunapokuwa tunatekeleza majukumu yetu ya kuishauri Serikali, kama wadau wa maendeleo ya nchi hii tunapotaka kutoa ushauri wetu kwa Serikali na pia kwa wananchi wetu ambao ndio picha halisi ya kazi ambayo inafanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Biblia, Kitabu cha Yeremia 33:3, neno linasema hivi:-

“Niite nami nitakuitikia na nitakuonesha mambo makuu, magumu usiyoyajua.”

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na maelezo yangu ya awali kwamba kama Wabunge, kama Kamati, kama wadau wa maendeleo tumekuwa tukiishauri Serikali hii lakini bado imeendelea kutuletea mipango ambayo ni copy and paste, yenye mambo yale yale ambayo hayatekelezeki, basi nimefikiri labda we need God’s intervation. Labda tusali sasa, kwa sababu kwa maneno tu kwa kusema kwa kuandika, kwa kuhubiri tumesema sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitamani nikuletee memo kwenye Kiti chako nikuombe labda leo Bunge hili tulibadilishe liwe nyumba ya Ibada halafu niongoze maombi, halafu na Wabunge wanijibu kwa kusema twakuomba utusikie. Kwa sababu sijaomba, basi naomba tu muwe wasikivu, mnisikilize niombe.

Mwenyezi Mungu nakuomba uwakumbushe Serikali ya CCM kwamba wananchi wanataka huduma za maji, afya, elimu bora na sio ndege ambazo hawatozipanda mpaka wanakufa. (Makofi)

Mwenyezi Mungu nakuomba uwakumbushe Serikali ya CCM waache kutuletea mipango ya maendeleo hewa. (Makofi)

Mwenyezi Mungu ninakuomba uwakubushe Serikali ya CCM kwamba wananchi wa Simanjiro walihitaji maji kwa sababu sasa hivi wanakunywa maji katika bwawa moja na ng’ombe, hawakutaka ukuta Mungu wakumbushe hilo.

Mwenyezi Mungu naomba uwasaidie kuwakumbusha Serikali ya CCM...

T A A R I F A . . .

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimemsikia Mheshimiwa Umbulla lakini mambo haya huwa ni maneno yanayosemwa tu, ni tarakimu zinazotajwa tu. Hata bajeti zimekuwa zikitajwa kwa tarakimu hivyo hivyo mwisho wa siku asilimia moja, mbili, kumi na moja, tunangoja kuona hilo la Simanjiro litachukua muda gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee na maombi yangu. (Kicheko)

Mwenyezi Mungu nakuomba uwaambie Serikali ya CCM ya kwamba uchumi wanaouhubiri unakua kwa kasi wao peke yao ndiyo wanaouona, wananchi wetu hawauoni na sisi Wabunge pia hatuuoni. (Makofi)

T A A R I F A . . .

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Naibu Spika, wakati naanza mchango wangu niliomba idhini ya Kiti, kwa hiyo, naamini na wewe unamwamini Mwenyezi Mungu na hili wala halikupi shida, naomba niendelee na mchango wangu.

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa maelekezo yako. Naomba basi niwakumbushe mimi kwa sababu tayari Mungu ameshaona dhamira niliyonayo moyoni kwangu, basi atayajibu maombi hayo kwa ileile dhamira yangu kwamba …

T A A R I F A . . .

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Kitwanga kwa taarifa yake, lakini mngewapa fursa Watanzania wakachagua nini wanataka, kati ya ndege au nini ambacho kitaleta madhara kwenye maisha yao, wangekuambieni wanataka X-Rays, CT-Scan, MRI kwa ajili ya afya zao kwa sababu mpaka sasa hivyo ni vitu ambavyo vinaonekana ni vya kupatikana Ulaya na si Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nimalizie kwanza kwenye ile hoja yangu ya sala, kwamba namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuwa amejidhihirisha yupo na anatenda miujiza katika maisha ya Mheshimiwa Tundu Antiphas Mughwai Lissu. Yule ambaye mlimtesa, mkampiga

risasi 18, mkakataa kupeleleza nani alifanya hivyo, mkashindwa kumtibu, navyozungumza …

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Magereli. . . .

HE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimshukuru Waziri wa Maji, kwa kazi nzuri aliyoifanya, baada ya malalamiko ya wananchi na wakazi…

T A A R I F A . . .

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee na mchango wangu. Naomba nimshukuru Mheshimiwa Waziri wa Maji kwa kazi nzuri aliyoifanya baada ya malalamiko ya sisi wadau na wakazi wa Kigamboni kuhusu mradi wa visima 20 vya maji vya Kimbiji na Mpera ambavyo hata juzi wakati nauliza swali kwa niaba ya Mheshimiwa Mwita Waitara nilieleza kwamba vile visima havijakamilika, kwa hiyo, Serikali inatudanganya kutuambia kwamba visima vimeshakamilika kinachofanyika ni kutafuta fedha kwa ajili ya usambazaji. Kwa taarifa rasmi zilizotolewa na Serikali juzi nimeona amevunja Bodi ya DUWASA na kuwawajibisha waliohusika wote kwa sababu ya ubadhirifu uliofanywa katika vile visima 20 na kwamba mpaka leo havijakamilika. Kwa hilo, naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo lingine ambalo na mimi nataka nilizungumzie kwa kina ambalo ni unyanyasaji na matendo yasiyo sawa kwa wafanyabiashara, watu wa sekta binafsi na wawekezaji. Ukitaka kuwekeza Tanzania, unaandamwa na ada, tozo, kodi, ushuru, leseni, na vibali visivyopungua 30. Tunasema tunakwenda kwenye Tanzania ya Viwanda, tunafikaje huko? Sisi tunaikimbia PPP, hatutaki kufanya miradi ya ushirikiano, wawekezaji wanaotaka kuwekeza nchini kwetu tunawaandama kwa milolongo ya kodi, ada na tozo zisizomithilika, tunafikaje Tanzania ya Viwanda? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukitaka kuwekeza katika kiwanda au katika sekta ya kilimo kwa ujumla, unatakiwa kulipia kibali cha BRELA, TBS, TPRI, TOSC, NEMC, Fire, Bima, OSHA, Zimamoto, TIN/VRN, Leseni ya Biashara, Vibali vya Kusafirisha Mazao, Ushuru wa Kusafirisha Mazao, Usajili wa Mbegu, Mabango, Bodi ya Usajili na Mizani na Vipimo. Ukiwa mwekezaji ukafika nchini ukapewa orodha ya kwamba haya ndiyo matakwa unayotakiwa kukamilisha ndiyo hatimaye usajiliwe na kufanya biashara Tanzania, naamini hata kama ungekuwa ni wewe ungekimbia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie swali lingine la mipango inayoendelea ya kutaka kuuwa Serikali za Mitaa.

Mipango yote tuliyonayo sasa hivi kiukweli na ukitazama hali halisi ilivyo tunamaanisha tunataka kurudi kwenye Centralization na si Decentralization ambayo ndiyo mfumo ambao tumekuwa tunautumia wakati wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naisu Spika, tumechukua vyanzo vya mapato vyote vya Serikali za Mitaa. Majukumu ambayo yalikuwa yakitekelezwa na Serikali za Mitaa mengi sasa naona yapigiwa upatu kwamba yarudishwe Serikali Kuu. Majukumu kama ya ujenzi wa barabara za vijijini tukaanzisha mamlaka inaitwa TARURA. Leo Serikali za Mitaa zinakwenda kukutana na aina ngumu kabisa ya mateso kwa sababu hata fedha za utekelezaji wa shughuli zake zitatakiwa kuombwa kutoka Serikali Kuu. Mmeshaona kwa miaka miwili hii iliyopita unaomba fedha inachukua muda mrefu sana hata kupatiwa hizo fedha kwa ajili ya matumizi mengineyo ya Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, fahamuni kwamba katika Serikali za Mitaa ndiko kwenye umma mkubwa wa Watanzania na ndiko wanakopata huduma kwa maeneo ya karibu. Sasa tunapofikiri kwamba lazima tupange mlolongo mrefu kusubiri fedha kutoka Serikali Kuu, nadhani hili ni kosa kubwa tunalolifanya na Mheshimiwa Waziri aangalie namna ya kulirekebisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala ambalo nimeliona kwenye bajeti kwamba kuna mpango wa kulinda viwanda vya ndani kwa kuongeza import duty. Mimi nadhani ambacho tunapaswa kufanya si kuongeza import duty kwa bidhaa zinazotoka nje ni kuangalia mazingira yetu yanavyoweza kuwa rafiki ili tuboreshe kilimo chetu lakini tuzalishe kwa wingi tutosheleze soko letu na tuweze kuwahudumia Watanzania bila kufikiri kuwakandamiza watu wengine ambao wanatakiwa kutuhudumiwa ambapo kwa wakati huo hatujaweza kuzalisha hizo bidhaa toshelevu kiasi tunachotaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kitabu cha Kamati na kabla sijasoma maoni hayo niliyoya-quote kisehemu kidogo, niipongeze Kamati ya Bajeti wamefanya kazi nzuri, wamechambua vizuri na wamekuwa honest, wamekuja kwenye Bunge na wamesema ukweli kuhusu wanachokiona kuhusu mwenendo wa bajeti ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ukurasa wa 30, Kamati wanasema kwamba, Kamati inajiuliza kuwa upungufu huu mkubwa wa mikopo na misaada kutoka nje unatokana na nini? Naomba nisaidie kuijibu Kamati kwamba upungufu wa misaada na mikopo kutoka nje inaletwa na ukanywagaji wa Katiba katika maeneo ya utawala wa sheria, utawala bora, uhuru wa kupata habari, uhuru wa kujieleza, uchaguzi wa Zanzibar na mauaji ya raia ambayo mpaka sasa hayachunguzwi na hatupati majibu yake.