Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Selemani Said Bungara

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Kilwa Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametupa akili Watanzania lakini hatuwezi kuitumia sawa sawa. Pili, ninakushuru wewe leo kwa kutumia busara kwa kuwasamehe wale waliokuja kupima samaki kwa kutumia ruler; na ndivyo inavyotakiwa kwamba mzee kama wewe uwe na busara. Tuwasamehe watu kama hawa; hawajui walitendalo, wanasema watu wengine huko.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono Waraka wa Maaskofu na Mashekhe, ili Serikali ya CCM irudi katika mstari unaotakiwa. Nawapongeza sana Mashekhe na Maaskofu, na Serikali muwe wasikivu myafuate yale waliyoyasema. Sisi wengine si Wachumi, sisi wengine wanasiasa. Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema ili tuendelee tunahitaji vitu vinne, ardhi, watu, siasa safi na uongozi bora. Tatizo ninaloliona mimi ni siasa safi na uongozi bora; hapa ndipo penye matatizo hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siasa yetu ya mfumo wa vyama vingi, siasa ambayo ilikuwa kama tungeitumia vizuri maendeleo yangepatikana kwa haraka sana. Hata hivyo, kutokana na uongozi wa nchi hii, ambao unatumia sana ubaguzi katika siasa zake nina wasiwasi hatutafika lengo tunalotegemea la maendeleo ya nchi hii. Sisi watu wa kusini tulikuwa nyuma sana kimaendeleo na ndiyo sababu Mkoa wa Lindi tuko draw sasa hivi CCM wanne Wabunge na CUF wanne Wabunge ngoma draw; na kwa kuwa tuko wanne kwa wanne, mambo yako safi sasa hivi Mkoa wa Lindi; upo safi kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia Mkoa wetu wa Lindi mimi ndiye Mwenyekiti wa Wabunge wa Mkoa wa Lindi, mimi hapa ndiye Mwenyekiti; na tunafanya kazi vizuri na Mheshimiwa Waziri Mkuu. Waziri Mkuu kwa upande mwingine lakini katika mambo ya ubunge mimi ndiye Mwenyekiti wake. Tunakaa, tunapanga kwa pamoja na mambo mazuri kabisa yanapatikana katika Mkoa wa Lindi sasa hivi.

Mheshimiwa Spika, ndiyo nakupa taarifa hiyo ndiyo Mwenyekiti mimi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo kutokana na mchanganyiko huu wa CUF droo na CCM mambo mazuri wakulima wetu sasa hivi wanapata leo ufuta bei inauzwa Sh.2,750. Tunakaa pamoja na Waziri Mkuu mimi nikiwa Mwenyekiti hapa. Tunapanga, tunaongea, tukishamaliza; leo tumeanzisha jambo lingine jambo jipyaa. Siyo stakabadhi ghalani, ni malipo ghalani ya ufuta. Jana tumeuza Sh.2,750 kwa kilo, siyo CCM huo ni mpango wa Mkoa wa Lindi. Kwa kuwa tunakaa pamoja tunashauriana tunamkosoa; Waziri Mkuu hapo sivyo hapo siyo stakabadhi ghalani, tatizo wanunuzi hakuna. Sasa hivi tuna Wachina, tuna Wahindi basi aah mambo yanakwenda vizuri tunakaa pamoja.

Mheshimiwa Spika, kuna njama ya makusudi ya Serikali ya CCM, ya makusudi ya kuturudisha nyuma Mikoa ya Lindi na Mtwara kwa makusudi na sisi hiyo hatukubali. Leo katika gesi tulikuwa tunapata asilimia tatu wanataka kutuchukulia, service levy wanataka watuchukulie. Halmashauri zetu zilikuwa zinapata asilimia 0.3, leo Mheshimiwa Dkt. Mpango anapanga mpango hela hiyo itolewe katika gesi ije katika Serikali Kuu ili sisi turudi nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, korosho! Serikali hawawezi kuhudumia korosho; tukapanga mpango wetu wa Kusini tuingiziwe fedha kwa mujibu wa sheria, export levy asilimia 65 irudi kule kwa mujibu wa sheria wakachukua, wakaweka, waaa. Bilioni themanini na moja ya mwaka 2017/2018 wamechukua wamekula na wana mpango sasa hivi walete sheria humu kwamba jambo lenyewe kabisa lisiwepo kabisa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nakwambia sisi mpaka tarehe 30 kama hela yetu haikurudi tunakuomba Mheshimiwa Spika uje Mtwara kupokea maandamano ya wakulima wa korosho wa Mikoa ya Kusini. Kwa sababu inaonekana Serikali ya CCM sawasawa na patasi haifanyi kazi mpaka igongwe. Kwa hiyo nakuomba Mheshimiwa Spika tarehe Mosi Julai, ufike Mtwara upokee maandamano ya wakulima wa korosho wanataka fedha zao.

Mheshimiwa Spika, na utuelekeze isiwe kama mpima samaki, utuelekeze Mheshimiwa Spika, tunakupataje, kwa sababu maandamano ya vyama vya siasa yamekatazwa; maandamano ya Wabunge wa Mkoa wa Lindi na Mtwara kutaka hela zetu zirudi. Tunakwambia Mheshimiwa Dkt. Mpango. Tunamwambia Mheshimiwa Mpango fedha zetu atuletee kama hakutuletea tutafanya maandamano Wabunge wa Mkoa wa Lindi na Mtwara mpaka asubuhi na Mheshimiwa hivyo hivyo…

T A A R I F A . . .

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, taarifa yake butu. Namwambia Waziri kwanza mpaka tarehe
30 hela yetu watupe kama hawakutupa tunafanya maandamano, sasa una wasiwasi gani. Kama hakutupa tutafuata sheria zote na tunakuomba Mheshimiwa Spika uje kupokea maandamano ya Wabunge wa Mikoa ya Kusini kwa ajili ya Dkt. Mpango aidha atoe hela au ajiuzulu kama si hivyo; varangati lile la gesi linaanza tena Kusini. Varangati lile lile! Wamandharaba nafsi la yabuki (ajipigaye mwenyewe haliii). Tunakuomba Mheshimiwa Spika utupokelee maandamano yetu, tunaanza upyaaa! Hiyo moja. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, pili, Kiwanda cha Mbolea cha Kilwa kijengwe. Leo sisemi mengi, nawashawishi Wabunge wote wa Mikoa wa Kusini tuungane tupambane na Mheshimiwa Dkt. Mpango, huyu Mheshimiwa ana matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho, nasema bajeti hii iongezewe katika mifugo, kilimo, maji; waongeze fedha, kama sivyo nitasema hapana, mkiongeza katika habari hii mwaka huu kwa mara ya kwanza nitasema ndiyo. Wakiongeza bajeti katika kilimo, maji, uvuvi Wallah Mheshimiwa utaona ajabu leo ndiyoooo, lakini kama hamkuongeza katika kilimo, uvuvi, mifugo; hapana!

Mheshimiwa Spika, sisi tunapigiwa kura na wakulima. Wakulima wakisema hawakupigii kura Mheshimiwa Dkt. Magufuli hapiti; na mimi nawajua CCM wajanja kweli kweli, wanataka mwaka 2019 ndipo wakulima wawape, wafanyakazi wawape hela! Nheheheee! Tuseme wanawafanya Watanzania wajinga, waseme mwaka 2019 eeh! Sasa hivi barabara safi ooooh, tunaongeza mshahara. Nasema wakiongeza tutawapiga, wasiongeze tutawapiga, wasitufanye sisi wajinga. Wajanja, wanatuuaua mwishoni, mshahara unaongezwa leo 2019, kuwafanya watu wapate tabu kwa miaka mitano mwishoni akhlini! Wanawazunguka Watanzania. Hizi siasa za hila hila na uongo uongo hizi ziishe mwaka huu; wakiongeza mwishoni tunawachukua tunawaweka, goli. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, mimi leo sisemi mengi leo mimi sisemi mengi, mgeni rasmi ni wewe. Inaonekana Bunge wameshindwa kumdhibiti Mheshimiwa Dkt. Mpango, wanatuambia tutawaletea habari za korosho, sisi maandamano, tutaandamana kweli kweli mwaka huu… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Spika, ahsante.