Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Kiza Hussein Mayeye

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia jioni ya leo, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya na kuweza kusimama hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kabisa na kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha Dkt, Philip Mpango pamoja na Naibu Waziri nimeipitia bajeti, niwapongeze sana kwa kuweza kupunguza kodi katika hizi taulo za kike. Naamini kwamba wamemfikiria binti wa Kitanzania ambaye yupo kijijini ambaye alishindwa kujiifadhi na wapo wengine mpaka kutumia majani kwa sababu ya kushindwa kupata hizi pads. Kwa hiyo, niwapongeze sana kwa kumfikiria binti huyu wa Kitanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu suala zima la kilimo, wote tunafahamu kwamba kilimo ni uti wa mgongo. Wote tumefika hapa tulipo, wazazi wetu wamekuwa ni wakulima wamelima na leo Mheshimiwa Waziri wa Fedha umefika hapo naamini hata kule Buhigwe babu yangu alikuwa akilima na akamsomesha na amefika hapo. Ningeomba sana Mheshimiwa Waziri katika bajeti hii tuzingatie sana suala la kilimo, kwa sababu naamni kilimo ni uti wa mgongo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia katika bajeti ya Mheshimiwa Waziri bado kuna mazao ambayo sijaona wakiyapa kipaumbele kwa mfano zao la mawese ndani ya Mkoa wangu wa Kigoma. Zao hili la michikichi, mbali na kwamba linatoa mafuta, pia linatoa bidhaa nyingi, tunaweza kutengeneza sabuni kwa kutumia michikichi, bado tunaweza kupata mafuta ambayo yanaweza yakalainisha ngozi na muonekano mzuri kwa akinamama, ningeomba sana tuweze kujali suala hili la michikichi na tutenge bajeti kwa wananchi wa Kigoma na maeneo mengine, tulifanye zao hili kwamba ni la biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika michikichi, leo michikichi iliyopo katika Mkoa wa Kigoma tayari imeanza kuzeeka, lakini wananchi wa Kigoma wako tayari kulifanya zao hili la biashara, naomba sana Mheshimiwa Waziri kuna mbegu bora ambazo sasa zinapatikana za michikichi waweze kuwagawia wananchi wazipate bure, mashamba yapo, maeneo yapo, waweze kulima na wapate mbegu hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mche mmoja leo unauzwa kwa Sh.5,700, katika maisha ya kawaida mtu hawezi kulima heka moja na akaweza kupata michikichi hii. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri aliangalie zao la michikichi Kigoma, Serikali iwagawie wananchi michikichi na tuko tayari kuweza kulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie tena zao la alizeti. Alizeti inalimwa katika maeneo ya Singida na maeneo mbalimbali. Ningeomba sana Serikali tulifanye hili kama zao la biashara, mikoa yote tuweze kulima alizeti tuweze kupata mafuta na tuweze kuondokana na uhaba wa mafuta katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie tena katika suala zima la afya, maeneo mengi ndani ya nchi yetu ya Tanzania bado kuna changamoto ya Wauguzi, hospitali nyingi hazina Wauguzi na hata nikitoa mfano katika Mkoa wangu wa Kigoma nimekuwa nikilisemea sana na kuuliza, kwamba hatuna Madaktari katika hospitali ya Mkoa, hata baadhi ya vituo havina Wauguzi. Unakuta kituo cha hospitali au zahanati kina Muuguzi mmoja katika hali ya kawaida bado tutaendelea kuwa na vifo vya mama na mtoto kwa sababu hatuna Wauguzi wa kutosha wa kutoa huduma kwa haraka na wakati unaostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba sana Mheshimiwa Waziri katika bajeti hii wanapokwenda kutenga fedha wahakikishe kwamba ajira hizi 8,000 wanazozitoa basi waweze kutusaidia ndani ya Mkoa wa Kigoma tupate Wauguzi wa kutosha na maeneo yote yenye changamoto hizi yaweze kupata Wauguzi. Wauguzi watakapokwenda katika maeneo husika basi waweze kulipwa pesa zao kwa haraka na kwa muda ambao unaostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie katika suala zima la ajira. Ajira imekuwa ni changamoto kubwa sana katika nchi yetu ya Tanzania hasa kwetu vijana. Vijana wengi wamekuwa wakimaliza vyuo; lakini wanakaa mtaani. Wao wanasema kwamba tujiajiri, kijana huyu wa Kitanzania anaweza kujiajiri vipi kama hata mtaji hana? Kwa hiyo, ningeomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha katika kuhakikisha kwamba wanaleta ajira kwa vijana hata kama wao wanajiajiri basi waweke mikakati ya kumwezesha kijana kujiajiri na biashara mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inaonesha kwamba sasa Afrika tunakabiliwa na tatizo la ajira, vijana wengi wamekuwa wakikimbilia nchi za ughaibuni kutafuta ajira, lakini katika bajeti hii sijaona Mheshimiwa Waziri ameelezea suala la ajira kwa vijana kwamba kama Waziri, kama Serikali wana mkakati gani wa kuhakikisha kwamba wanawasaidia vijana wa Kitanzania na je, tupo katika hatari gani kama vijana wa Kitanzania kukimbilia katika nchi zingine kutafuta ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukisikia watu wakiangukia katika bahari wanatokea Ethiopia, lakini hata Tanzania kuna vijana ambao wanakimbilia South Africa, wanaishi maisha magumu South Africa, wanateseka wanauawa, yote hiyo ni kwa sababu hakuna ajira, wanaona bora wakimbie nchi zingine kutafuta ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha baba yangu Dkt. Mpango waweke mikakati ya kumsaidia kijana wa Kitanzania kuondokana na changamoto ya ajira. Hii itasaidia vijana kujiepusha na vitendo vya wizi, lakini itawasaidia vijana hasa kina dada kuepukana na tabia hii ya kujiuza ili waweze kupata kipato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie tena katika suala la TRA. Tunasema kwamba ‘Hapa Ni Kazi Tu’ na kweli wananchi wanajituma kufanya kazi. Imekuwa inasikitisha hata Mama Lishe ambaye anajitahidi kuchuuza ili aweze kumsomesha mtoto na kuondokana na umaskini bado TRA wanamsumbua. Hata kijana huyu wa Kitanzania ambaye ametoka shule anasema ngoja nijiajiri nifungue kibanda changu niweze kupata riziki, bado TRA wanakimbizana nae. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiukweli hii inakatisha tamaa na kwa stahili hii tutaendelea kuwa na vibaka na wezi ndani ya Taifa letu. Kwa hiyo, ningeomba sana TRA Mheshimiwa Waziri ukae nao uongee nao, imekuwa ni changamoto kubwa, imekuwa ni kero kubwa watu wanafunga maduka, imefikia hatua sasa mtu anaona nina milioni tatu siwezi kufanya biashara, kwa sababu milioni tatu hata dada akisema afungue kisaruni chake kidogo bado hataweza kufanikiwa kwa sababu TRA nao wako nyuma yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri suala zima la TRA kiukweli wakae nao chini waangalie ni jinsi gani wanaweza kutusaidia wananchi, isifike mahali sasa mtu unaogopa hata kufungua biashara yoyote kwa sababu unaamini TRA wanakwenda kunisumbua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie tena katika suala la nishati. Nipongeze sana Wizara ya Nishati kiukweli wanafanya kazi nzuri katika miradi hii ya REA maeneo mengi yamepata umeme na naamini hata yale ambayo hayajapata umeme yanakwenda kupata umeme katika REA III. Pia nipongeze mradi huu wa Mto Rufiji, binafsi naona ni mradi mzuri na naupongeza sana, lakini naomba kutia msisitizo kwamba tuhakikishe fedha zinakwenda kwa wakati, pia nimwombe sana Mheshimiwa Waziri kwamba tutenge bajeti ya kutosha katika suala zima la nishati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mradi huu pamoja na kwamba tunaenda kupata megawati nyingi za umeme lakini kwa sababu tunakwenda katika nchi ya viwanda bado naamini kwamba yawezekana ule umeme usitoshe na tukahitaji umeme mwingine, tuweze kuwa encourage hawa private sector investors waweze kuja kuwekeza na wenyewe katika nishati hii ya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, nishauri jambo moja, kwamba ingekuwa ni vizuri…..

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nimalizie kwamba ingekua ni vizuri ikatengwa bajeti kwa sababu ya watu wa TANESCO wakafanya feasibility study and then ikaelezea kwamba hapa tunazalisha megawati kadhaa, tumetumia kiasi kadhaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga hoja.