Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. COSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba pia nitumie nafasi hii ingawa Mheshimiwa Mwambe amesema tusipongeze lakini niipongeze sana Serikali yangu kwa kuendelea kutekeleza vizuri Ilani ya Uchaguzi ya CCM. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ili uvuke uende Geita lazima upite Busisi na juzi tumeona uzinduzi wa kivuko kipya ambacho kitakuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kuchukua abiria wengi na magari na ni njia hiyo pekee ambayo kwa kutokea Mwanza naweza kufika Jimboni. Kwa hiyo, naipongeza sana Serikali kwa kutimiza ahadi yake hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niiombe Serikali walikuwa wanafanya feasibility study nadhani kwa ajili ya kujenga daraja kwenye eneo lile ambalo litapunguza sana vifo visivyo vya lazima ambavyo vinatokea wakati unasubiri ferry kwenda Bugando kwa sababu ndiyo hospitali pekee ya rufaa, kama upembuzi yakinifu ule umekamilika basi nimwombe sana Waziri wa Fedha kwamba wananchi wa Kanda ya Ziwa hasa wananchi wa Geita na Mikoa mingine wanasubiri kwa hamu kuona ujenzi wa daraja lile unaanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri juzi amesema ameondoa kodi ya VAT kwenye taulo za kike, nampongeza sana kwa sababu ilikuwa ni ombi la kwetu wenyewe Wabunge. Wasiwasi wangu tu nataka aje anisaidie punguzo hili la VAT wamefanya utafiti litapunguza bei kwa kiwango gani kwa watumiaji. Nafahamu kwamba hizi exemptions mara nyingi mwisho wa siku zinawafaidisha zaidi wafanyabiashara na siyo watumiaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Kamati kwenye suala la maji, mwaka jana na mwaka juzi tulipendekeza kwamba iongezeke Sh.50 ili tutunishe Mfuko huu wa Maji na hatimaye tuongeze uwezo wa Serikali kwenye kuhudumia miradi ya maji. Kwa hiyo, nimwombe mwaka ule alikataa lakini mwaka huu na dalili ilivyo na kwa sababu tumemaliza mwaka mmoja na nusu kwenda kwenye uchaguzi nadhani sasa anafahamu kwamba bila kufanya hivyo suala hilo litakuwa gumu sana kutekeleza na kwa sababu ni Ilani yetu wenyewe ya uchaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende sasa kwenye suala lenyewe la hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Hapa karibuni baadhi ya wachangiaji wameonesha sana wasiwasi wa kwamba bajeti yetu Tanzania ni ndogo kulingana na nchi ya jirani kwa mfano Kenya ambao bajeti yao ni dola bilioni 30 na nimeona Uganda wenyewe wana kama dola bilioni 8.5 lakini imeongezeka kwa asilimia 15, Tanzania imeongezeka kwa asilimia mbili. Nadhani sababu ya Waziri kutokuongeza bajeti kama alivyokuwa anafanya miaka ya nyuma ni kutokana na tax base yetu kuwa ndogo na tax base yetu imekuwa ndogo siyo kwa bahati mbaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakubaliana nami kwamba Waziri wa Biashara anahangaika sana kuvutia wawekezaji waje, lengo lake ni kuongeza tax base ili Waziri Mpango aweze kukusanya kodi. Waziri wa Madini anahangaika kutengeneza sheria ili kuwarasimisha wachimbaji wadogo wadogo lakini kuhakikisha kwamba migodi yote inaweza sasa kulipa kodi ili kuongeza tax base.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napata tabu sana kama Serikali inakwenda kwa kufikiri pamoja. Wakati Wizara hii inahangaika sana kuboresha tax base unashangaa kuona Wizara nyingine inatumia sheria na kanuni kuhakikisha kwamba wafanyabiashara ambao wapo wanaendelea kulipa kodi wanafilisika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kutoa mfano kwenye uvuvi, nimeangalia hapa kwenye taarifa ya Kamati, uvuvi umetengewa 0.06. Hivi ninavyozungumza tumepata taarifa hapa kutoka kwa Mheshimiwa anayeshughulika na uvuvi na mifugo kwamba amekusanya takribani bilioni nane kwenye faini na kodi mbalimbali kwa wavuvi haramu, lakini anasema amekuja kugundua asilimia 98 ya wavuvi wote Tanzania ni wavuvi haramu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba ameondoa walipa kodi asilimia 98 kwenye mfumo wa kulipa kodi ambao Mheshimiwa Dkt. Mpango alikuwa anakusanya kodi wote ni wavuvi haramu, amewaondoa kwenye mfumo bila kuja na mpango wowote wa kuhakikisha kwamba hiyo tax base anairudishia. Madhara yake ni kwamba tunaotoka kwenye maeneo ya uvuvi kabla ya Watanzania wengi kuingia ziwani kuvua samaki, wavuvi pekee walikuwa ni wale wenye viwanda na wenye viwanda walipewa kazi na Serikali ya kuwawezesha Watanzania kununua nyavu hizi ambazo ziliruhusiwa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, waletaji wa nyavu wakalipa kodi, wakawakopesha Watanzania na wale Watanzania wakanunua wakaweka dhamana nyumba zao, nyavu ambazo zote ni haramu, zimekamatwa zote zimechomwa moto. Hawa wenye viwanda ambao leo hawawezi kuwakopesha tena Watanzania waliokuwa wanavua samaki na wale wote waliokuwa wanavua samaki hawana mitaji, maana yake ni kwamba hatuwezi tena kukusanya kodi lakini tumeua hiyo industry ya samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sishangai ninapomwona Waziri anaposema samaki wamekuwa wengi ziwani, ni kwa sababu anasahau there is no more industrial fishing tena kwa sababu asilimia 98 ya wavuvi waliokuwa mle ziwani ni wavuvi haramu kwa tafsiri yake, kwa nyavu alizopokea na alizoziruhusu yeye kuingia ziwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wasiwasi wangu ni mmoja, tunalalamika kwamba bajeti yetu ni ndogo lakini ukiangalia system nzima haifanyi kazi pamoja. Nilitarajia kwa kuwa kanuni hizi ni za Waziri na kanuni zinazomwongoza kufanya kazi hii amezitunga yeye, Sheria ya Uvuvi iko vizuri sana. Kwa kuwa nyavu hizi zililipiwa kodi na kwa kuwa tunahitaji industry ya uvuvi iendelee kuwepo ili tupate kodi, nimeangalia kwenye kwenye kitabu cha Mheshimiwa Dkt. Mpango makusanyo yote haya kwa miezi minne sasa ukienda Mwanza hayapo, angefanya mpango maalum wa kuhakikisha kwamba kunakuwa na transition period kabla ya kuanza kuchukua hatua ambazo zinaondoa walipa kodi, karibu asilimia 30 ya walipa kodi wa Kanda ya Ziwa ni Wavuvi wote wanaondoka kwenye mfumo na wakirudi kukopa wataanza kulipa interest na interest ina gharama kwenye kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwamba tunapotengeneza tax base, ukiangalia sasa hivi mwaka huu tumeshindwa kuongeza kwenye projection yetu ni kwa sababu tax base yetu ni ndogo. Tulikurupuka miaka fulani tukawa tunaongeza kila mwaka matokeo yake hatujawahi kukusanya kwa asilimia 100. Sasa kama tunatengeneza tax base leo kesho tunaibomoa, unaitengeneza kesho, kesho unaibomoa maana yake ni kwamba tunarudi nyuma badala ya kwenda mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona juzi kwamba Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi amegundua kwamba operesheni ili iweze kufanikiwa sasa ni lazima twende kwa walaji na walaji ni kwenye hoteli na anatumia regulations hizo ambazo ni za uvuvi. Tatizo kubwa ambalo naliona, mimi nadhani Watanzania wengi hawajui kwamba source ya samaki siyo Ziwa Victoria peke yake, regulation iliyopo inazungumzia samaki wa Ziwa Victoria, sato na sangara lakini kuna watu wanafuga samaki, ambao hawafugi kwa masharti kwamba ili awavune lazima wafikie sentimita ambazo yeye anazitaka. Cost yake ya ku-run lile bwawa huwezi kusubiri mpaka samaki akae miaka mitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, samaki wa Mtera na Nyumba ya Mungu hawafanani na sato walioko Ziwa Victoria. Kwa nini Waziri akili yake anafikiri tu kwamba lazima hawa watakuwa ni kutoka Ziwa Victoria halafu ukikutana na sato species 50, Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kukisema hapa ni kwamba unaweza ukaletewa sampuli ya sato 10 lakini wale sato 10 ni species tofauti, hawafanani na kadri wanavyotofautiana hawakui kwa kufanana. Kwa nini Waziri anakimbilia kwenda… kwa sababu kadri unavyochukua hatua una- demoralize watu wote wanaoshughulika na ile biashara una erode tax base. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.