Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia bajeti yetu ya Serikali. Kwanza, naomba nimtangulize Mwenyezi Mungu katika mchango wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kuchangia naomba nimpongeze Mheshimiwa Spika na niwapongeze Chama cha Wabunge Wanawake walioko hapa Bungeni kwa hafla hii ya leo ya kuhakikisha kwamba wanahamasisha wananchi kuchangia tukio hilo la kujenga vyoo vya watoto wa kike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze mchango wangu sasa kwa kumpongeza sana Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mpango; Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Kijaji na Watendaji wote wa Wizara. Pia naipongeza Kamati ya Bajeti ambayo kwa kweli imekuwa ikifanya kazi nzuri sana kuhakikisha bajeti zetu zinakuwa rahisi hata kuzijadili hapa Bungeni. Vile vile bajeti hii ni nzuri sana. Bajeti ambayo ilisomwa tarehe 14 Juni, 2018 ni nzuri sana kwa sababu hata Mwenyekiti wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Mbowe aliipongeza bajeti hii. Kwa hiyo, inaonesha jinsi gani ambavyo bajeti hii imekuwa nzuri. Hata Mbunge wetu wa Iringa alipongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii inatakiwa sasa Watendaji wajipange kuhakikisha yale mambo ambayo yako katika bajeti wanayafanya vizuri ili kusiwepo na malalamiko. Maana Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia, hasa kwenye bajeti ya Serikali kwa Wizara ya Fedha kulikuwa kuna malalamiko mengi sana hasa kwa upande wa kodi. Kwa hiyo, naomba kabisa Mheshimiwa Dkt. Mpango ahakikishe anasimamia bajeti ili wananchi wetu waweze kutendewa haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naungana na Waheshimiwa Wabunge wote waliopongeza Serikali kwa kuondoa ushuru katika taulo za kike. Tatizo hili kwa kweli limekuwa likisumbua sana watoto wetu wa kike na nafikiri lilizungumziwa sana na Wabunge wengi wanawake na huu ulikuwa mshikamano halisi kwamba wanawake wote ni lazima tuhakikishe kwamba tunaipigania hii kodi. Serikali yetu kwa sababu ni sikivu, naona wameiondoa kodi. Kwa hiyo, nina imani kabisa bei zitapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile niendelee kuipongeza Serikali kwa kuondoa kodi katika mikopo inayotolewa katika Halmashauri zetu, ile 5% ya wanawake na asilimia tano ya vijana. Najua kuondoa kodi kutasaidia sana kuwajengea uwezo hasa wa kifedha akinamama na vijana katika Halmashauri zetu kuhakikisha kwamba kile kilio kwamba wanakosa mitaji sasa angalau kwa kuondoa ile kodi watakuwa na mitaji ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba labda Serikali ingeweka wazi kuhusiana na watu wenye ulemavu, kwa sababu hii 5% ya wanawake na vijana bado haijatamka wazi kuhusiana na watu wenye ulemavu katika Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Manispaa yetu ya Iringa, tayari imetenga 2% kwa kuwakopesha watu wenye ulemavu na vikundi vinne vimepata mikopo ya shilingi milioni tisa. Kwa hiyo, ni jambo zuri. Pengine nchi nzima kungekuwa kuna tengeo la 2% kwa watu wenye ulemavu. Kwa sababu watu wenye ulemavu wamekuwa wakifanya biashara nzuri tu ambapo kwa kweli hawataki kuomba. Ni watu ambao wanaweza kufanya biashara nzuri kuliko hata watu ambao hawana ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nielezee kuhusiana na kilimo. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Kilimo, Maji na Mifugo. Uchumi wa Viwanda ambao ndio mwelekeo wa Serikali yetu hii ya Awamu ya Tano unategemea sana sana kilimo. Naipongeza Serikali sana kwa kuweka kilimo kama kipaumbele katika bajeti yetu. Pia Azimio la Maputo linasema asilimia 10 ya mapato ya bajeti ya Serikali ni kwa ajili ya kilimo, lakini karibu miaka mitatu sasa hivi, tunaona kilimo bado hakijapewa kipaumbele. Tunaona hata asilimia moja haitengwi kwa ajili ya kilimo. Kwa hiyo, naiomba Serikali yetu, ili sera yetu ya viwanda iweze kwenda vizuri, ni muhimu sana kutoa kipaumbele katika kilimo nchini kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile Serikali ihamasishe sana wakulima wakubwa waweze kuwekeza katika kilimo. Watakapowekeza katika kilimo maana yake hata ajira pia kwa vijana itapatikana kuhusiana na kilimo kwa wakulima wakubwa kama zilivyo nchi nyingine. Vile vile tuwajengee uwezo wakulima wadogo wadogo na kuwawezesha ili kilimo kiweze kuwasaidia, kwa sababu asilimia kubwa sana ya Watanzania ni wakulima wakiwepo watu wa Mkoa wangu wa Iringa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuishauri Serikali yetu ijitahidi sana kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji, kwa sababu programu zake nyingi sana za umwagiliaji hazijaweza kufanyika vizuri sana katika maeneo mengi. Unaona maeneo mengi yametengwa, lakini bado kilimo cha umwagiliaji hakifanyi vizuri sana. Ninao mfano halisi kabisa hata katika Mkoa wangu wa Iringa, miradi mingi ya umwagiliaji haijaweza kufanya vizuri kuwasaidia wananchi wanaofanya kilimo. Kwa hiyo, naiomba Serikali yetu ihakikishe kwamba programu za umwagiliaji zinapewa kipaumbe kwa sababu zenyewe hata bila mvua bado tutaendelea kupata mazao mazuri ambayo yatasaidia hata katika viwanda vyetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu Benki ya Kilimo. Nilitegemea Benki ya Kilimo ndiyo ingekuwa mkombozi kwa wakulima, lakini badala yake inafanya biashara ya kukopesha benki. Maneno haya hata siku ile Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli aliyazungumza wakati wa uzinduzi wa ASDP II. Sasa niombe Serikali isimamie kuhakikisha Benki ya Kilimo inawafikia wakulima na inawakopesha na wakulima waweze kukopesheka vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulifanya ziara kwenye Mkoa wa Iringa kwenye miradi hii ya SAGCOT. Tumeona miradi ya SAGCOT ni mizuri sana, lakini kuna changamoto nyingi sana katika baadhi ya viwanda tulivyovitembelea. Kwa mfano, kuna suala la vifungashio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikwenda pale Tanzanice Station pale Njombe, vifungashio ni tatizo kubwa sana. Vifungashio vinanunuliwa kutoka Kenya, halafu sasa kuna walanguzi wanakuja hapa nchini wanachukua mazao, wanapeleka Kenya kwenda kufungasha. Inaonekana kama mazao ni ya Wakenya wakati ni ya Watanzania. Kwa hiyo, ni muhimu sana kuwasaidia watu watakaofungua viwanda vya vifungashio ili kuondoa hii changamoto ambayo iko kwa wajasiriamali wetu na wafanyabiashara wengi waliopo nchini ili kusaidia kuongeza kipato kikubwa katika bajeti yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulienda katika kiwanda cha Asasi, tuliona kwamba kimeanza kuwekeza katika vifungashio. Sasa labda kiwezeshwe ili kisaidie kuondoa hii changamoto kubwa ambayo ipo. Kwa sababu pia kuna changamoto tuliona katika Kiwanda cha Silverland na hata Asasi kwamba kuna tozo nyingi sana zinatozwa katika viwanda vyetu, karibu tozo 12 na kusababisha sasa hata wenye viwanda wanakata tamaa. Kwa sababu naona kuna tozo nyingine zinafanana. Kwa hiyo, naiomba Serikali ijaribu kujumuisha hizi tozo iwe moja ili kusaidia watu wengi sana waweze kuwekeza katika viwanda, itatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu miradi ya maji, bado mingi haijakamilika na miundombinu yake bado haifanyi kazi, hata iliyokamilika bado haifanyi vizuri. Sasa ile Sh.50/= naona kama Serikali ingeifanyia kazi. Tunategemea kama tutapitisha hiyo Sh.50/=, naona Waheshimiwa Wabunge wengi sana wamechangia, ingeweza kusaidia sana katika kuhakikisha kwamba mwanamke tunamtua ndoo ya maji kichwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia kuhusu kuhusu miradi ya PPP. Hii miradi ni muhimu sana. Tukichukulia tu mfano wa Daraja la Kigamboni; daraja hili sasa hivi tumeweza kujenga kwa kutumia...

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali twende na mpango huu wa PPP. Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nizungumzie kuhusu ni Electronic Tax Stamp.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono hoja. Naomba Watendaji wote waitendee haki bajeti yetu kwa sababu ni bajeti nzuri sana ambayo tunategemea kwamba itatendea haki hata Chama chetu cha Mapinduzi.