Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Khatib Said Haji

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Konde

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante nakushukuru, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kusimama hapa kutoa mchango wangu katika Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, lakini nataka nianze kwa salamu moja ya pongezi kwa dhati kabisa kwa Mheshimiwa Waziri na Wizara yake kwa jambo moja kubwa la udugu walilolifanya, kwa sababu tunaelewa kama Serikali Tanzania tunazo Serikali mbili na zote Serikali mbili ni za Chama cha Mapinduzi. Kwa hiyo, udugu wa Serikali hizi mbili umedhihirika mara hii kwa udhati pale walipoweza kulitamka gawio halisi la Zanzibar la shilingi bilioni 200 kwa kweli tunawashukuru. Huu ni udugu na hii imeonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nilifuatilia Baraza la Wawakilishi, wawakilishi wakihoji hela zile zimefikia wapi na Waziri alikosa jibu, Waziri wa Zanzibar alikosa jibu. Kwa hivyo namuomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kutueleza hapa atuambie pesa hizi zimekwenda wapi au zimekwama wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili, kidogo nitakuwa tofauti kabisa na wenzangu leo na ninaomba mnisamehe sana kwa sababu katika mwezi ambao huu tunapaswa kusema ukweli ni huu. Kwa hiyo leo nataka niwe tofauti kidogo na wenzangu wa upinzani, katika jambo la kuikosoa Serikali kupita kiasi hasa kwenye masuala haya ya hela. Nasikia na nawaona wenzangu mnavyosimama sana kuhoja shilingi trilioni 1.5, mimi sikuihoji mimi nimetaka zile bilioni 200 Zanzibar ziende. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na nasema hivi kwa sababu mbora wa mkosoaji ni yule anayeanza kujikosoa mwenyewe. Na kuna mwana mashairi mmoja alisema; “mtu akitaka sema kwanza hutazama lake, akajigeuza nyuma kutizama aibu zake, ni aibu kusimama kuyasema ya mwenzake.” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema haya kwa nini? Mheshimiwa imetolewa ripoti wote tumeng’anga’nia kwenye shilingi trilioni 1.5. Lakini kwenye ripoti hiyo hiyo kuna maelezo yaliyotolewa kuhusu utumiaji mbaya wa fedha za rukuzu zinazotolewa na Serikali. Jambo hilo naomba tusikilizane, leo sihitaji makofi nahitaji mnisikilize.

Mheshimiwa Spika, Chama cha Mapinduzi kimeguswa kwamba kuna maeneo hayako sawa, CHADEMA kimeguswa, ACT kimeguswa chama changu mwenyewe kimeguswa. Sasa mimi nitaacha vyote vilivyoguswa. Na wengine wameguswa wamepeleka hesabu lakini, zina makando kando. Bahati mbaya sana chama changu ambacho nimesimama hata taarifa hakikupeleka. Hata taarifa kwa Mkaguzi hazikupelekwa, hivi mimi napata wapi ujasiri wa kukosoa shilingi trilioni 1.5 wakati chama changu kinachopokea 120 million per month kimeshindwa kupeleka hesabu kwa Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali, inanipa shida sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nayasema haya nikijua kwamba Katibu Mkuu cha Chama ndiye Accounting Officer na ndiye Masuhuli wa kujibu mambo yote yanayohusiana na pesa za chama. Naelewa na ninajua na nitaka nikufahamishe kama ni mtu ninaye mheshimu sana Katibu Mkuu wangu Maalim Seif Sharrif Hamad, lakini katika hili naomba nieleze ukweli, kwamba kwa kweli hajakitendea haki chama hiki kuacha kupeleka hesabu zinazotakiwa kwa Msimamizi Mkuu wa Hesabu za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, whatever tuna vyombo vinavyopaswa kufanya kazi ya kulinda fedha za chama. Naomba mnisikilize vizuri, sitamtaja yeyote kuhusiana na kutokushindwa kupeleka hesabu, nitamtaja Katibu Mkuu wa chama changu. Sasa kama kuna mengine yanayojificha naomba sasa TAKUKURU, Waziri wa Mambo ya Ndani, ahojiwe Katibu Mkuu aeleze ni kwa nini hakupeleka hesabu kwa Msimamizi wa Hesabu za Serikali. Tuanze hapo ndio nasema Mbora wa mkosoaji huangalia aibu zake kabla ya kusema za wenzake. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, haya mambo yanataka ujasiri sana. Itakapokuja tokea kwa bahati mbaya yakaja yakatoa ya kutokea naomba Kanuni ile inayomlinda Mbunge kwa anayozungumza humu itumike kikamilifu. Yasije yakaenda ya mwendo wa kasi kama yaliyowakumba wenzangu. Nakuomba sana. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naamini niliowataja wanaohusika na vyombo vya upelelezi watalifanya hili kwa sababu Mheshimiwa Spika ameliunga mkono kwa hiyo sitaki longo longo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nizungumzie suala la pili, kwa muda mrefu tumekuwa na kilio. Zanzibar hapa tunapozungumza siku zote mafuta ya petroli yanakuwa na tofauti kati ya 200 au 300 zaidi juu kulinganisha na Tanzania Bara. Sababu ni nini? Sababu ni moja tu, Mheshimiwa Waziri mafuta yanayokwenda Zanzibar yanakuwa-charged dola 10 per tone, ikiacha mbali tofauti na dola tatu/nne isiyozidi tano kwa nchi nyingine tunazopakana nazo. Kwa nini jambo hili linatokea kwa Zanzibar?

Mheshimiwa Spika, sisi kama ni kuhurumiana, huruma kwanza inaanza kwa ndugu na jirani. Hivi sadaka gani inayoanza Zambia, Malawi na Kongo ikaacha Zanzibar ambao sisi ni ndugu? Ni jambo la kusikitisha sana, kwa nini mpaka leo suala hili tumekuwa tukiliuliza Mheshimiwa Waziri bado mmelitafutia kona ya kuliweka ni kero ya Muungano. Tusiishi kwa mazoea ya kero, kero hupatiwa utatuzi suala hata hili la mafuta Zanzibar kutozwa dola 10 kwa tani ikiacha nchi nyingine wakienda na dola tatu/nne na isiyozidi tano, ni suala ambalo naomba mliondoe kwenye kero za Muungano na mlifanye ni suala maalum na mlipatie ufumbuzi wa haraka ili angalau Wazanzibar waweze kununua mafuta kwa bei inayofanana na wenzao wa Tanzania Bara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumekwenda mbali zaidi sasa hata ng’ombe wakipelekwa Zanzibar baada wanavyolipa mnadani wale Wazanzibari au wafanyabiashara wanaopeleka ng’ombe Zanzibar wakifika bandarini wanakuwa-charged tena kama wanaoenda Comoro. Hasa inachukuliwaji Zanzibar? Ni foreigner’s au ni nchi ya Tanzania? Haliko sawa hata kidogo.

Mheshimiwa Spika, naomba mliangalie sana, nawaomba sana, hata ng’ombe kwa hivyo hayo masuala mengine tusirundike tu kero za Muungano. Mambo ambayo yanaweza kutatuliwa kwa uharaka yatatuliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuje na suala la usajili wa vyombo vya moto, mwaka wa 20 leo ukitoa gari Zanzibar ukija hapa bado limewekwa kwenye kero za Muungano. Yanasemwa maneno tunalifuatilia, hadi lini? Vitu vingine vinasababisha manung’uniko yasiyo na msingi. Basi kama inashindikana, wenzetu wanaingiaje? Kongo wanapofika pale border wana-surrender document wanapewa permit ya kuishi na gari yao hapa ndani ya nchi yetu miezi mitatu. Akimaliza anarudi tena anaweza kukaa nayo hivyo. Basi kama Zanzibar inawezekana ikiingia gari pale bandari zizuiwe kadi Mzanzibari au yeyote anaingia na gari yake ikiwa document zimezuiwa pale, tutumie utaratibu huo. Naelewa huo hauwezekani kwa sababu sisi ni nchi moja, hilo linakuwa shida maana yake mkianzisha hilo tufungue ubalozi Zanzibar wa Tanzania. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, maana yake sasa tuna-treat kama nchi nyingine wakati sisi ni ndugu na ni nchi moja. Kwa hiyo, hebu na hili Mheshimiwa Waziri lifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine nataka kuzungumzia hapa ni suala la ushuru bambikizi, ushuru mkubwa. Jana alisema Mheshimiwa Mbunge mmoja hapa akasema kwamba tatizo moja kubwa ambalo tunalo ni kuweka kodi kubwa kwa kutegemea tutapata pesa nyingi. Matokeo yake watu wanatafuta mbinu za kukwepa tunakosa hata hicho kidogo. Nakushuru.