Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa katika Mkutano wa Kumi na Kumi na Moja wa Bunge

Hon. Taska Restituta Mbogo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa katika Mkutano wa Kumi na Kumi na Moja wa Bunge

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Kwanza kabisa napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, ametujalia afya njema na uhai tuko hapa Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niipongeze kwanza Kamati ya Sheria Ndogo, ambayo ni Kamati yangu kwa kazi nzuri inayoifanya chini ya Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Mtemi Chenge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza sana Wajumbe wa Kamati hii kwa sababu moja Kamati ya Sheria Ndogo mtu mwingine/mwananchi au Mbunge anaweza akasema kwamba Kamati ya Sheria Ndogo ni ndogo. Lakini niwaambie wananchi wa Tanzania pamoja na Wabunge mliomo humu ndani, Kamati ya Sheria Ndogo siyo ndogo kwa namna hiyo, kwanza ilipaswa iitwe Kamati ya Sheria Kubwa kwa sababu Kamati hiyo inapitia kanuni zote za Halmashauri zote nchini ambazo zinakwenda kumuathiri mwananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maana kwamba kanuni zote zinazotungwa na Halmashauri nchini Tanzania zinapita kwenye Kamati ya Sheria Ndogo na kanuni hizo zinakwenda kumuathiri mwananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano, unaweza ukaenda miji mingine unakuta Halmashauri imetunga sheria kwamba ukitupa hata gamba la big G chini unalipa shilingi 50,000; ni nani anaathirika, si mwananchi wa kawaida? Ndiyo maana nikasema hizi kanuni zinamuathiri na zinatumika na mwananchi wa kawaida, anaishi nazo kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, napenda nichangie mawili/matatu kuhusu kanuni ambazi zinaletwa kwenye Kamati yetu. Kanuni zinaletwa kwenye Kamati yetu wakati ambapo zinakuwa zimeshakuwa gazetted kwenye Gazeti la Serikali na zinakuwa zimeshaanza kutumika na wananchi moja kwa moja wanakuwa wameshaathirika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa zinapokuja pia kurekebishwa, tunapokuja kukaa sisi pale kwenye Kamati tunazirekebisha, zinapokwenda tena kuchapwa na kwenda kutumika tena lakini utakuta damage inakuwa ni kubwa mwananchi wa kawaida anakuwa ameshakuwa damaged.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama walivyochangia wachangiaji waliopita, niombe tu utaratibu utumike kwamba inapotungwa sheria, zile kanuni zinapotungwa zije kwanza kwenye Kamati ya Sheria Ndogo tuzipitie, tuzirekebishe kabla hazijakwenda kuwa gazetted kwenye Gazeti la Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine ambao ninapenda kuutoa ambao naona kwamba kanuni na sheria ndogo zinamuathiri mwananchi wa kawaida, ni matamko ya viongozi. Kwa mfano tamko la Waziri, tamko la Mkuu wa Mkoa, tamko la Mkuu wa Wilaya, moja kwa moja linamuathiri mwananchi wa kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano, Mkuu wa Wilaya anaweza akatamka kwamba kila Jumamosi ni siku ya usafi maduka yasifunguliwe mpaka itakapofika saa nne asubuhi, anayeathirika hapa ni mwananchi wa kawaida. Kwa maana hiyo ni kwamba kwa mfano mwananchi akifungua lile duka au hoteli yake kabla ya ile saa nne asubuhi, atalipa faini labda ya shilingi 500,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi niombe tu yale matamko tunapoyatamka sisi viongozi, awe ni Waziri, Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya, tuyaangalie yasiwe na athari kwa mwananchi wa chini ambaye anakwenda kuishi na yale matamko yetu kwa maisha yake ya kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kutoa pendekezo lingine kwa Serikali, niombe hizo kanuni ziwe zimepita kwenye Kamati ya Sheria Ndogo tuzirekebishe, lakini pia niombe wale watendaji wanapotunga zile kanuni ambazo zinakwenda kutumika kwa wananchi waziangalie zile kanuni ziwe zinaendana na sheria mama. Kwa mfano kanuni haiwezi ikazidi sheria mama, zile kanuni zinatakiwa ziwe chini ya sheria mama au zifuate ile sheria mama inasemaje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapotunga kanuni ambayo inakuwa ni kinyume na ile sheria mama ina maana unakwenda nje ya ile sheria, ina maana wewe hapo unatunga sheria nyingine. Kwa hiyo, basi niombe tu wale watendaji wa Serikali wawe wanazisoma vizuri zile sheria na watunge kanuni ambazo zinaendana na ile sheria mama iliyopo ambayo imewafanya watunge kanuni hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninapenda kulitoa kama ombi, Halmashauri zetu nchini Tanzania zinapotunga zile sheria ndogo zijaribu kuzichapa na kuweka kwenye notice board ili wananchi wanapopita waangalie kwamba katika mji wetu kuna sheria fulani ambayo tunatakiwa tusiifuate. Ukitunga kanuni ukazikalia ofisini ukaweka kwenye draw hizo kanuni zinakuwa hazina faida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano tu niseme unaweza ukawa umetunga kanuni kwamba parking eneo hili hairuhusiwi, lakini hujaweka notice board na hujaweka kwenye mbao za matangazo kwamba hilo eneo halitakiwi mtu ku-park gari, mtu anapokuja ku-park unampiga faini ina maana hapo inakuwa si sahihi. Niombe Halmashauri kanuni zao ziwe zinawekwa kwenye mbao za matangazo na pia matamko ya Mawaziri yawe na limit, kwa mfano akitoa tamko liwe na duration period kama ni tamko la mwezi mmoja au mwaka mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwaombe sisi Wabunge tujaribu kununua yale magazeti yanayokuwa gazetted, zile kanuni zinapotolewa kwenye Gazeti la Serikali sisi Wabunge tunatakiwa tununue tuzisome na tukawaeleze wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja na mambo yote yaliyoandikwa kwenye Kamati ya Sheria Ndogo.