Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Nishati

Hon. Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Nishati

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika Wizara hii nyeti. Naomba nianze na TANESCO na muda ukiniruhusu nitaenda maeneo mengine. Wabunge tuliokuwa katika Bunge hili kipindi kilichopita na ripoti mbalimbali za Kamati ikiwepo kamati ya Mashirika ya Umma ambayo mimi nilikuwa mjumbe, Mwenyekiti wangu alikuwa Mheshimiwa Zitto Kabwe, tulizungumzia namna gani TANESCO inajiendesha kwa hasara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya Serikali ya Awamu ya Tano haijaingia madarakani, TANESCO ilikuwa ikipata hasara shilingi bilioni124. Baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani, TANESCO inapata hasara shilingi bilioni 346. Hasara hizi zinatokana na upungufu wa maji ya uzalishaji umeme pamoja na gharama za uendeshaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini siyo hapo tu, Mwenyekiti wa Kamati ametoka kuelezea madeni ya TANESCO ambayo yamepanda kwa asilimia 23 kabla ya Serikali ya Awamu ya Tano haijaingia madarakani kutoka shilingi bilioni 738 mpaka shilingi bilioni 958. Haya si maneno ya Ester Bulaya, ukisoma ripoti ya CAG na imesema kabisa madeni haya hayana uwiano kati ya mali za Shirika la TANESCO pamoja na madeni. Kwa namna nyingine TANESCO imefilisika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wakati haya yanatokea kulikuwa na ushauri wa Kamati yetu chini ya Mheshimiwa Zitto Kabwe ya Mashirika ya Umma na taarifa mbalimbali ya Serikali kulikuwa na mikakati mbalimbali na ambapo nchi mbalimbali pia zinafanya, kwamba, hili Shirika ni wakati muafaka sasa likagawanywa yakawa mashirika mawili. Likawepo Shirika linalo-deal na masuala ya uendeshaji na lingine masuala ya uzalishaji, dunia nzima inafanya. Leo hii tusingekuwa tunaendelea kuzungumzia umeme wa kwenye vibaba wakati tuna-plan kuwa na nchi ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Hong Kong hawasheherekei miaka 50 ya Uhuru wanasheherekea miaka 50 umeme hata siku moja haujakatika kwenye nchi yao. Ni kwa sababu wana mipango mizuri katika uzalishaji na usambazaji. Sisi hatutakuwa wageni, South Africa wanafanya, jirani zetu Kenya wanafanya na hii mikakati ipo kwa nini, Serikali ya Awamu ya Tano hamtaki kufanya? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mambo haya yanafanyika, hapo sijaenda deni la Standard chartered la Euro zaidi ya milioni 10 na gharama za kesi takribani bilioni 7.5, hilo naliacha wataongea wengine. Wakati haya yanafanyika na hali ya TANESCO ilivyo dhoofu, TANESCO pia inashindwa kukusanya madeni makubwa. TANESCO inaidai hospitali ya Tumaini dola za kimarekani milioni 9.4 sawa na bilioni 18 za Kitanzania na ni kodi ya pango. Tangu mwaka 1998 hawajawahi kulipa. Kulikuwa na kesi Mahakamani TANESCO imeshinda tangu mwaka 2016 na maamuzi ya Mahakama yanasema hivi, waondoke na kisha walipe TANESCO hizi Fedha. Mpaka hivi tunavyozungumza pamoja na maamuzi ya Mahakama TANESCO hawajachukua hatua yoyote pamoja na kuwa mfilisi wanahitaji fedha. (Makofi)

Mheshimiwa mwenyekiti, lakini kingine TANESCO kwa masikitiko makubwa imetoa zabuni kwa mzabuni asiye na vigezo kinyume na mkataba. Masharti ya mkataba yanasema hivi, mzabuni awe na uzoefu wa miaka mitano, lakini sasa huyo mzabuni mwenyewe ana leseni ya kusambaza pembejeo yaani majembe, mbolea, kazi aliyopewa ni ya kusambaza nguzo ya umeme na keshakula dola milioni moja zaidi ya bilioni 2. Mkataba unasema awe na uzoefu wa miaka mitano na hii ni kinyume cha Sheria Na. 3 ya Mwaka 1972 ya Leseni na Biashara. Serikali ya Awamu ya Tano aibu, shame, shame, sasa haya tunayasema kwa sababu tunapenda nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati haya yanatokea mikakati ya kushindwa kugawanya TANESCO, mmeshindwa kulisimamia shirika vizuri, mmeshindwa kufuata ushauri uliotolewa na mikakati ya Serikali inashindwa kutekelezwa mnaenda kwenye mambo mengine ya Stiegler’s Gorge ambayo mmeitengea bilioni 700, hizo ni fedha zetu za ndani wakati hizo fedha mngepeleka kuboresha Shirika la TANESCO, mngeligawa mara mbili na pesa nyingine zingeenda kwenye REA. Hapa Mwenyekiti wa Kamati ameeleza wazi, mbali ya kwamba TANESCO inadaiwa, bilioni 700 zimetengwa kwenye Stiegler’s Gorge ambayo hatima yake hatuijui. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye REA kwa mwaka huu wa fedha, kwenye fedha zote za maendeleo hiyo Stiegler’s Gorge imetengewa karibia asilimia 40 ya fedha za maendeleo. REA ambayo at least mbali na changamoto zake imefanya vizuri asilimia 20 na bajeti iliyopita REA wamepata asilimia 49. Waheshimiwa Wabunge wote tunajua sheria, fedha zilizowekewa uzio hazipaswi kutumika kwa matumizi mengine. Fedha zinatakiwa zitolewe zote, kufanya hivyo ni kuvunja sheria na ni mfululizo wa Serikali ya Awamu ya Tano kutokutii sheria, amesema pale Mheshimiwa Nape, mnaendelea tena kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilitakiwa hizi pesa zitolewe zote, sisi Wabunge tunaotoka mikoani tunajua umuhimu wa umeme wa REA kukamilika. Timizeni wajibu wenu, tuache hizi mbwembwe ndogo ndogo halafu hapa mnasema mnataka kuwa na Serikali ya Viwanda, kwa mtindo huu, kweli? Haiwezekani! Mimi niwaambie baada ya kufikiria miradi mipya una uwezo wa kuacha legacy kwa kukamilisha miradi uliyoikuta ya umeme wa upepo, makaa ya mawe, tukamilishe haya kwanza halafu twende huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwepo wakati pori la Selou linatangazwa kuwa urithi wa Dunia nchini Qatar na dunia ikakubali kutusaidia kutupa fedha nyingi. Leo tunaenda kukata miti milioni mbili huko kwenye huo mradi halafu nasikia mkiulizwa mnasema ooh, tumechukua eneo dogo, jamani ni kama mwili moyo ni mdogo lakini mwili mkubwa, toa moyo kama binadamu utaishi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi yetu sisi Wabunge ni kushauri na kusimamia Serikali ifanye kazi yake ipasavyo kwa ajili ya vizazi vyetu vijavyo. Tunalipenda Taifa hili, hatuhitaji deni la Taifa liongezeke kwa sababu hakuna mipango thabiti ya kuivusha nchi yetu. Ukiona mpaka wengine tunasema hivi yametuchosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi, timizeni wajibu wenu, acheni mbwembwe ndogo ndogo.