Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Naghenjwa Livingstone Kaboyoka

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, naomba kutoa shukrani zangu kwa Serikali kwa kusaidia kukarabati miundombinu ya maji katika Jimbo la Same Mashariki, Kata ya Maore ambapo wanyama pori waliharibu miundombinu ya maji. TANAPA walitoa fedha kwa hiyo tatizo hili limetatuliwa.

Pili, pia nitoe shukrani zangu kwa TANAPA kwa ushirikiano mzuri walio nao kwa wakazi wanaopakana na Hifadhi ya Mkomazi. Baada ya kusema hayo naomba nitoe changamoto zinazowakabili wananchi waishio karibu na hifadhi hii ya Mkomazi, nazo ni hizi:-

(i) Kutokana na kwamba Hifadhi ya Mkomazi haina maji ya kutosheleza kwa ajili ya hawa wanyamapori, wanyama hawa bado wanatoka kwenye hifadhi na kwenda kufuata maji kwa wanavijiji. Kwa maana hiyo miundombinu hiyo iliyokarabatiwa hivi karibuni iko hatarini kuharibiwa tena.

Mheshimiwa Spika, kwamba TANAPA watenge fedha ili wachukue maji ya mtiririko (gravity water) kutoka chanzo cha Mto Hingilili ambao una maji mengi na hayajawahi kukauka tangu kuumbwa kwa dunia hii, chanzo hiki cha Mto Hingilili alisha kwenda kukiona Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA Mr. Kijazi na kuahidi kutenga fedha kwa ajili ya mradi huu.

Mheshimiwa Spika, ni wazi kwamba Serikali inapoteza fedha nyingi kuchimba mabwawa ambayo baada ya muda mfupi maji yake hukauka na hivyo kusababisha wanyama pori kuvamia makazi ya watu. Wakati wanyamapori hawa wakienda kutafuta maji, huleta madhara makubwa kwa kula mazao ya wakulima pamoja na kujeruhi watu.

Mheshimiwa Spika, kutokana na kwamba mpaka wa Hifadhi hii ya Mkomazi umesogezwa karibu sana na makazi ya watu hasa wafugaji, kumetokea migogoro mikubwa kati ya TANAPA na wakulima na wafugaji. Tatizo ni kwamba wananchi hawakushirikishwa wakati wa kuweka mipaka. Matokeo yake ni kwamba wananchi wameachwa na ardhi kidogo wakati TANAPA wamechukua ardhi kubwa zaidi. Wananchi wanaona Serikali yao inathamini wanyama pori zaidi kuliko inavyothamini binadamu. Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Same Mashariki wanaoishi karibu na Hifadhi ya Mkomazi, tunaomba mipaka iangaliwe upya ili wananchi watengewe eneo kubwa la malisho pamoja na eneo la kulima.

Mheshimiwa Spika, ni wazi kwamba barabara ya Same - Kisiwani - Mkomazi ambayo inapita kando kando ya Hifadhi ya Mkomazi, ni mbaya sana kiasi kwamba hata watalii hawawezi kuvutiwa kwenda kuona wanyama kwenye hifadhi hii. Itakumbukwa kwamba faru mweusi kutoka Czech alipelekwa kwenye Hifadhi hii ya Mkomazi. Hivyo basi TANAPA wana kila sababu kutafuta namna ya kuongea na Wizara ya Ujenzi ili barabara hii itengenezwe kwa kiwango cha lami ili kuweka mazingira mazuri ya kuvutia watalii kutembelea hifadhi hii. Ni wazi kwamba utalii ni sekta ambayo inaweza kuongeza pato la Taifa kwa kiwango kikubwa sana. Nchi zinazowekeza kwenye utalii uchumi wake ni mkubwa sana.

Hivyo sekta hii ni muhimu sana kwa ukuaji wa uchumi wa Tanzania ili tufikie azma ya kufikia uchumi wa kati, kati ya miaka ya 2025 – 2030. Hifadhi ya Mkomazi ina wanyama wa kila aina wakiwepo tembo, nyati, twiga na kadhalika. Hivyo naamini Wizara hii ya Maliasili na Utalii itaiangalia Hifadhi ya Mkomazi kwa jicho la tatu.

Mheshimiwa Spika, ahsante.