Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Risala Said Kabongo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa dakika tano hizi ningependa kujikita kwenye makundi matatu yanayotoa huduma katika Mlima Kilimanjaro.

Mheshimiwa Spika, kuna makundi matatu yanayotoa huduma katika Mlima Kilimanjaro, kuna waongoza watalii, wapagazi na wapishi. Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro ni hifadhi maarufu duniani lakini hifadhi hii ni moja ya maajabu saba ya dunia. Ni hifadhi yenye urefu wa mita 5,895. Vilevile hifadhi hii ina wageni wengi wanaotembelea kuliko Watanzania. Nikiangalia nina takwimu hapa mwaka 2013/2014 wageni wa nje walikuwa 35,682 na wa ndani walikuwa 2,021 lakini mwaka 2016/2017 walifika wageni 45,818 na wageni wa ndani walikuwa 2,723 tunaona tofauti ilivyo kubwa.

Mheshimiwa Spika, waongoza watalii, wapishi na wapagazi wamekuwa ndiyo engine ya kupandisha wageni katika Mlima Kilimanjaro na wapagazi hawa wanapandisha Mlima kwa mwaka wakiwa na idadi ya zaidi ya 30,000 lakini kwa muda mrefu waongoza watalii hawa wamekuwa hawapati stahiki zao kama inavyopaswa. Watu hawa wamekuwa wakionekana kwamba hawana elimu wala hawana ujuzi wa kutosha, lakini ndiyo wanaofanya kazi kubwa sana, wakikosekana basi hakuna mgeni anayeweza kupanda Mlima Kilimanjaro. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivyo basi ninaiomba Serikali itambue kuwa waongoza watalii ni kazi ya kitaalamu na ya kitaaluma inayostahili kuheshimiwa, kuthaminiwa ikiwa ni pamoja na kuwawekea mazingira mazuri ya kufanya kazi, pia watambulike kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitarejea barua moja hapa ya wakati Mama Shamsa Mwangunga alipokuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, hii ni pamoja na utekelezaji wa changamoto zinazowakabili waongoza watalii, pamoja na wapishi na wapagazi. Ilikuwa ni barua tarehe 15 Desemba, 2015 na tarehe 8 Aprili, 2016. Kulikuwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja ya namna ya kuwalipa wapagazi hawa, wapishi na watembeza watalii ambayo ilikuwa ni ya GN Na. 228 ya mwaka 2008. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kikao hicho walishiriki Tanzania Association of Tour Operators, Kilimanjaro Association of Tour Operators, Kilimanjaro Guard Association, Tanzania Tour Guard Association, Tanzania Porters Organization na kwa upande wa Serikali walishiriki Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Wizara ya Kazi, Ajira na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro. Kwa masikitiko makubwa kuna zaidi ya makampuni 400 yanayofanya shughuli za kupandisha Mlima Kilimanjaro lakini ni Makampuni 20 yanayowalipa stahiki hawa wapanda mlima, wapagazi na wapishi. Wengi wao wanawalipa shilingi 5,000/shilingi 8,000 mpaka shilingi 10,000 inasikitisha sana. Kwa sababu wapagazi hawa na wapishi na watembeza wageni wanafanya kazi ngumu, wengine wanafia kule mlimani, wengine wana familia, wana majukumu makubwa, hawana makato yoyote yanayowafanya baada ya kumaliza muda wao wa kazi hizi waweze kufaidika na kazi hii lakini bado wanalipwa kipato cha chini sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kingine kikubwa Watumishi hawa kwa kuwa hawapati mikataba kutoka kwa waajiri wao kama Tour Operators wanapoteza mapato mengi sana ya Serikali, kwa mfano hizi withholding tax hawawezi kulipa kwa sababu hawana mikataba na waajiri wao.

Kwa hiyo, ninaomba Serikali iangalie sana suala hii kwa mfano, Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Wizara ya kazi hawawezi kukwepa kukaa pamoja kuweza kushughulikia tatizo hili. Wamekuwa na kilio cha muda mrefu na hakuna msemaji wameunda vikundi vyao vya kuwasemea, lakini wanapofika kwa mwajiri wanakuwa hawana mtetezi kwenye Wizara ya Kazi, wakati mwingine kwenye mikoa kunakuwa na mwakilishi mmoja tu wa Wizara ya Kazi ambaye anakuwa na mambo mengi hawezi kuwasemea watu hao. Lakini vilevile wamekuwa wakipata mafunzo katika Chuo cha Taifa cha Mweka, kumekuwa na mafunzo ambayo yanatolewa ya muda mfupi wiki tatu wanalipa shilingi 800,000 ili waweze kupata certificate. Lakini nilikuwa naiomba Serikali…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.