Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Joshua Samwel Nassari

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Arumeru-Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. JOSHUA S. NASSARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Maliasili na Utalii. Kabla sijaanza, ni-declare kabisa mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, nitazungumzia mambo matatu. La kwanza, migogoro kati ya wananchi, vijiji na hifadhi za Taifa. Vilevile nitagusia sekta nzima ya utalii kama ilivyo na mwisho nitagusia kidogo habari ya Stiegler’s Gorge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na migogoro kati ya wananchi na hifadhi zetu. Waheshimiwa Wabunge ambao tunakaa ndani ya Bunge hili kama kweli tunataka kuitendea haki nchi hii, kama kweli tunataka kuwatendea haki wapiga kura waliotuchagua kuja ndani ya Bunge hili leo tunaitwa Waheshimiwa, ukizunguka kwenye nchi hii wafanyabiashara wanalia, wakulima wanalia, wafugaji wanalia na wavuvi wanalia, whom are we serving? Tunamhudumia nani? Sasa leo hifadhi zetu baraka ambayo tulipewa na Mungu badala ya kuwa baraka kwetu imegeuka kuwa laana kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, to be specific, mimi natoka Meru. Mwaka 1949,1950 mpaka 1951, Watanzania ama Watanganyika kutoka jamii ya watu wa Meru walichomewa nyumba na wakafukuzwa kwenye makazi yao na waliokuwa wakoloni kwa maana ya walowezi wakati ule na hiki ndicho kinachoitwa The Meru Land Case, kwa wale ambao wameipitia wanaifahamu vizuri. Watu walikuwa displaced, wakafukuzwa kwenye maeneo yao, wakachomewa nyumba, wakaenda kuanza maisha mapya sehemu nyingine kabisa. Mwaka 1952, watu wa Meru walichanga fedha kwenye vyungu barabarani, haikuibiwa senti hata moja, mwaka 1952 alikwenda Umoja wa Mataifa, Mtanganyika wa kwanza kwenda Umoja wa Mataifa, UNO wakati ule aliitwa Ndugu Japhet Kirilo Ngura Ayo na alikuwa Mbunge wa kwanza wa jamii yetu ndani ya Bunge hili. Amekwenda UNO mwaka 1952 kwa sababu ya ardhi ya watu wa Meru, watu wa Ngarenanyuki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii mwaka 2018, miaka mingi na uhuru umepatikana na tumesonga mbele, watu wa Meru wamekwenda kufukuzwa kwenye ardhi yao ile ile ya Ngarenanyuki. Sasa, who is better? Mkoloni ambaye alichoma tu nyumba au leo ambaye anafukuza watu, anawapiga na risasi, anapiga rasilimali zao risasi, anawapiga na mabomu, wanawaachia vidonda, who is better?

Mheshimiwa Mwenyekiti, with due respect, Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla is a good friend of mine and he knows na urafiki wetu it’s personal, lakini katika hili Mheshimiwa Waziri tunahitaji msaada wako. Where is the supremacy of this Parliament? Mwaka jana nimeongea ndani hapa, aliyekuwa Naibu Waziri wa Wizara hii akakubali kuondoka hapa kwenda Meru kusaidiana ku-solve mgogoro wa watu wa Momela na Hifadhi ya Taifa ya Arusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa masomoni Uingereza, nikamuomba Mheshimiwa Mbatia hapa anisaidie ku-handle this case nikijua uwezo wake na heshima ambayo anayo na namna gani anaweza ku-handle vizuri suala lile. Akakubaliana na Waziri hapa, wameondoka wamekwenda Arusha, Mheshimiwa Mbatia ametangulia Momela kukaa kwa niaba ya Mbunge Nassari, Waziri amechoma mafuta kafika Arumeru, amezuiwa wilayani akaambiwa mgogoro huu umekwisha, hakuna kinachoendelea, hakuna tatizo, akalazimishwa kuondoka. Mheshimiwa Mbatia akapigiwa simu akaambiwa nimepata dharura bwana ondoka, rudi zako Moshi, kisa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkuu wa Wilaya aliyeondoka kwenda kuweka vigingi yeye na askari wa TANAPA kwenye hifadhi ya Taifa ya Arusha kwenye namba 40 na 41 akiitwa Alexander Mnyeti, bila kushirikisha mwananchi hata mmoja wa Momela, hata mmoja. Vigingi vimewekwa siku ya Jumapili watu wako Kanisani, wanatoka wanakuta vigingi vinawekwa. Mnatutonesha vidonda. Yale tuliyofanyiwa na wakoloni mnakuja kutufanyia leo, mnatonesha vidonda vya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ninayokuonesha hapa, hizi ni risasi za moto na mabomu waliyopigwa wananchi wa Momela. I will table this, nitaweka kwako hapo. Siyo hivyo tu, hizi ni picha na ng’ombe waliopigwa risasi pale Momela shamba 40 na 41 ambalo wakoloni walinyang’anya watu wa Meru wameondoka wamewaachia leo hii 2018, linakuwa claimed kwamba ni sehemu ya hifadhi, hifadhi imeanza miaka 60, watu wa Meru tumeishi hapo kabla, tumenyang’anywa mwaka 51, tumerudi leo hii mnatunyang’anya, twende wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono maoni ya Kamati yaliyosomwa na Mheshimiwa Nape hapa leo, kwamba zoezi la uwekaji wa vigingi lisimame. Leo hii ukienda Rukwa, Shule ya Msingi aliyosoma Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda, shule ya msingi aliyosoma Waziri aliyeko hapa ndani leo anaitwa Mheshimiwa Kamwelwe, leo imeambiwa ni sehemu ya hifadhi lakini Waziri Mkuu alisoma hapo, are we serious? Shule aliyesoma Nsa Kaisi leo inaambiwa iko ndani ya hifadhi, are we serious? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, with due respect Mheshimiwa Waziri, tafadhali na Naibu Waziri alishakubali tuondoke hapa twende Meru. Naomba maoni ya Kamati yaheshimiwe, zoezi lisimame, ushirikishwaji ufanyike. Leo unaenda kuweka kigingi kwenye kitanda cha mtu anaishi hapo, hivi kweli, nani mwenye thamani nchi hii tembo au raia wa Tanzania? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafugaji wananyanyaswa kwenye nchi hii, ng’ombe waliochukuliwa wakaenda kuhifadhiwa na ANAPA hawa hapa wamekaa zaidi ya mwezi mmoja kule ndani, angalia walivyodhoofu. Wamekuja kuachiliwa, achilia mbali waliopigwa risasi, over 75 percent of them wamekufa kwa sababu ya kudhoofu. Wale wanyama walikuwa wanatumika kwenye kilimo wakati wa masika watu hawakulima kwa sababu wanyama wameshikiiwa, wengine walikuwa ni ng’ombe ambao wana ndama, ndama wamebaki ndani wakafa. Msitutie umaskini nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo langu la Meru kwenye kata 26, kwenye Kata ya Ngarenanyuki ambapo Momela ndiyo kata pekee ambayo Chama cha Mapinduzi mlichaguliwa mkapata Diwani mmoja, ndiko mmekwenda kuwapiga risasi, mtawaambia nini 2020? Mtawaambia nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, utalii kama sekta. Kwa mujibu wa ripoti ya Tanzania Economic Update ya World Bank Tanzania tuna uwezo wa ku-earn over 27 trillion per year kama kweli tukiweza kuwekeza vizuri kwenye sekta ya utalii. Southern Circuit peke yake ni eight billion USD. Leo tunavyozungumza, tunakwenda kujenga Stiegler’s Gorge, Selous, world heritage, dunia inatushangaa, tunatafuta megawatt 2100, hivi tuko serious? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikusomee kwa sababu ya muda niende haraka tu. Wote tunahitaji umeme na mimi nahitaji umeme sana kule kwangu lakini kwa miradi ifuatayo ambayo ni upstream bila kwenda kuhangaika na Selous na kuharibu miti milioni 2, bila kuchukua eneo ambalo ni kubwa usawa wa Dar es Salaam ndani ya hifadhi ya Selous, tuna uwezo wa kuzalisha zaidi ya megawatt 2196, leo tunatafuta megawatt 2100 Selous, uwekezaji hela hatuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sikiliza, megawatt 180 peke yake tunaweza kupata Kihansi ambayo tayari imeshafanyika, megawatt 165 Mwanga, megawatt 685 Ruhuji, megawatt 485 Mnyera, megawatt 87 Iringa, megawatt 130 Lukose na megawatt 464 Kilombero. Bomba la gesi tumetumia six percent peke yake, tuna megawatt 800 kwenye miradi ya Kinyerezi. Tukitumia asilimia 25 ya bomba la gesi ambalo leo
Watanzania tunawalipa Wachina waliotukopesha, tuna uwezo wa kupata over 3000 megawatts, are we thinking right? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu nawauliza ndugu zangu wa CCM mnapata wapi hela ya kujenga huu mradi wa Stiegler’s Gorge? Wamarekani hawawapi shilingi kwa sababu UNESCO wamekataa na mashirika yote ya dunia yamepinga. Ulaya hamtapata shilingi hata moja, mnasema mtakwenda China, China wamebaki kwenye Paris Agreement as we are speaking today, China ndiyo wame- burn meno ya tembo wanajaribu kuji-brand duniani kwamba wanapigania uhifadhi, where are you getting the money? Tunahitaji umeme lakini siyo kwa namna hii. Naomba Wabunge tuitendee haki nchi yetu. Tulitendee haki Taifa letu, tutendee haki nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sekta ya utalii nilizungumza kidogo. Wanaotangaza utalii leo nchini ni tour operators. Tour operators ndiyo wanakwenda kwenye trade fairs, ndiyo wanakwenda Indaba, WTM, ITB, Vegas, leo Waziri wa Maliasili na Utalii tangu ameingia madarakani kama Waziri hajawahi kushiriki kwenye trade fair hata moja. Tumsaidie Waziri asafiri akaitangaze nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, angalieni Wakenya wanafanya kitu gani, nyie mmeweka VAT tulikubaliana kwenye mkutano wa East African Community baada ya kukubaliana mmegeuka, Wakenya wakaondoka, sisi tumeweka. Leo hii ukichukua miaka minne mfululizo tangu mwaka wa fedha 2012 -2016 growth rate ya utalii nchi hii kwa maana ya watalii waliokuwa wanakuja…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)