Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Dr. Pudenciana Wilfred Kikwembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kavuu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ili nami niweze kuchangia katika hoja hii iliyoko hapa mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, napenda nianze na dhima ya Wizara. Dhima ya Wizara ni pamoja na kuendeleza utalii kwa manufaa ya Taifa. Naomba nianzie hapa hapa kwenye kuendeleza utalii kwa manufaa ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi wa kuendeleza utalii Kanda ya Kusini ambao unajumuisha Udzungwa, Ruaha, Mikumi, Selou na uligunduliwa pale Iringa. Naomba Serikali na Wizara inijibu, Katavi ipo wapi? Kwa nini haiko kwenye mradi huu? Katavi tuna kiwanja cha ndege suala ni kuongeza, zimebaki kilomita mbili pia na kuweka taa ili tuweze kukuza uchumi wa kule. Katavi National Park iko wapi? Nataka kujua ina mradi gani ili na sisi tuweze kufaidika na hii hela ya REGROW ambapo imetolewa karibu dola milioni 150 kwa ajili ya kuendeleza utalii Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia niungane na maoni ya Kamati hasa kwenye sera ya ujirani mwema kuhusu huduma za kijamii. Nakumbuka niliwahi kuuliza swali hapa kuhusiana na vijiji vyangu vinavyopakana na mbuga ya National Park pamoja reserve ya Rukwa Rekwati. Vijiji hivi vimepakana na mto ambao wanautumia lakini watendaji wengine ambao si waaminifu wamekuwa wakitumia advantage ya kuwaumiza wananchi kutokana na mto huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nikaomba katika Kata yangu ama Kijiji changu cha Luchima kilichopo Kata ya Majimoto ambako kuna Vitongoji vya Luchima, Masangano, Ilunda, King’anda, Kawanga na Kiwanjani vyenye wananchi wapatao 7,571 wapatiwe visima vya maji kama ambavyo Kamati imeshauri ili tuweze kuondoa hiyo migogoro. Baada ya kufanya hivyo tuone ni askari wa TANAPA ama hawa TAWA ndio wenye matatizo na wananchi ama wananchi ndiyo wenye matatizo wanaoingia ndani ya reserve.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Kijiji cha Ikulwe ambako kuna Kitongoji cha Ikulwe A, Ikulwe B, Madulu, Isimba na Mgoroka na kuna wananchi wapatao 5,562. Kwa hiyo, niombe sana tufanye kama Kamati ilivyoshauri ili tuweze kuondoa migogoro ambayo imekuwa ikijitokeza ambapo wananchi wamekuwa wakipigwa na kuumizwa bila sababu wakati mnakuja kuwapa kifuta jasho ambacho hakifanani wala hakilingani na kiungo chake cha mwili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba niongelee kuhusu suala hilo hilo la watendaji ambapo wamekuwa wakiwaumiza wananchi. Nina mwananchi wangu nimewaambia kesi wapeleke polisi na mahakamani, ameuawa au amepotea maana haonekani katika Reserve ya Rukwa Rukwati. Kati ya tarehe 15-16 Aprili, alipotea na nguo zake zikapatikana kisa ng’ombe zilikwenda kunywa maji pale na hawa watu wa TAWA nafikiri wanalifahamu hili suala vizuri sana. Mwingine alipigwa risasi kwenye paja. Huyu mtu ambaye amepotea anaitwa Seme Mahila. Kwa hiyo, tunaomba kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani tujue ukweli uko wapi kuhusiana na tatizo hili ambalo limejitokeza katika Kata ya Mwamapuli, Kijiji cha Ukingwaminzi. Kwa hiyo, naomba sana huyu mtu tupate taarifa zake na Serikali iingilie kati ili tuweze kujua watu gani wenye makosa, ni watendaji ama ni wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala lingine ambalo limekuwa likilikumba Jimbo langu la Kavuu. Katika Jimbo langu la Kavuu sehemu tunayoweza kuchimba kifusi ni ndani ya National Park. Kwa hiyo, niwaombe sana kwa maendeleo ya wananchi wangu na jimbo langu ambalo ni jipya, hawa watu wa TANAPA na Wizara hii ya Maliasili washirikiane na halmashauri ili tuweze kupata vifusi kwa ajili ya kuweza kutengeneza barabara zetu. Tumekuwa na tatizo la kupata kifusi na sehemu tunayoweza kupata ni ndani ya National Park eneo la Kibaoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwaombe sana mnaweza kushirikiana na halmashauri kwa karibu ili tuweze kutengeneza barabara zetu angalau ziwe za kwiango cha changarawe tuweze kupita ama udongo kwa sababu barabara zangu hazipitiki. Najua ni sheria, huruhusiwi kuingia ndani ya National Park au kwenye reserve area lakini naomba kwa kutumia vigezo hivyo hivyo kwamba Serikali ni moja basi tushirikiane tuone tunatatua vipi matatizo ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nije katika sekta ya wanyamapori. Katika sekta hii ukisoma hotuba na hata ripoti ya Kamati wanazungumzia kuwalinda wanyama ambao wako hatarini kupotea kama faru na tembo. Naomba nitoe mfano wa tembo, tunasema wako hatarini kupotea lakini kila siku tunalalamika tembo wanavamia mashamba. Kwangu hivi vijiji vyote nilivyovitaja saa hizi sina mahindi, tembo wamevamia na wako wengi, mimi nasema wako wengi ndiyo maana wanakwenda kule. Je, kwa nini tusifanye uratatibu wa kuwavuna na hiyo nyama ikaliwa na wananchi ili tuwapunguze badala ya kusema tuweke pilipili, hivi nani ataweka mwanzo wa Jimbo mpaka mwisho? Hiyo pilipili unaiagiza kutoka wapi? Tunaanza kuilima lini ili huyo tembo akimbie? Je, wananchi wote sasa tuache kulima tufuge nyuki pembeni ya reserve areas? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuna mbadala ambao hata zamani wazee wetu walikuwa wakiutumia badala ya haya mambo ya vitalu mnayobadilisha sheria kila siku na matamko, tulisema hapa vitalu viondolewe ndiyo chanzo cha ujangili lakini tena mmerudisha. Wananchi zamani walikuwa wanapewa leseni wanawinda na wakawa na mapenzi mema na mbuga zao. Sasa leo mnawapa watu wachache ambao hao hao kwa kushirikiana na watendaji ambao si waaminifu ndiyo wanaopiga wananchi wetu na wanavuta wale ng’ombe kwa makubaliano wanaziingiza katika mbuga zao na kuanza kuzipiga risasi na kuwadai wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi naomba tutafute njia mbadala, hatuwezi miaka yote tukawaweka tembo, tutashindana nao, tutaishi nao vipi? Hatuwezi kuishi nao kwenye vijiji ambavyo tunapakana navyo. Kwa hiyo, niwaombeni sana taratibu zilikuwepo na wanyama walikuwepo na tulikuwa tunaishi nao, sasa kwa nini tunaanza kuja na vitu ambavyo vinaanza kutuletea shida. Wananchi wanaweza kabisa wakavuna tembo kwa utaratibu ambao mmejiwekea wenyewe kama Serikali. Nyama ile ikaliwa na wale tembo wakapungua wasilete tabu kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, mimi napenda kuishukuru Serikali yangu kwa kuendelea kuagiza ndege, naamini zitatumika katika kutangaza utalii wetu. Kwa hiyo, naomba sasa hizo ndege zinazoagizwa na Katavi zifike ili ziweze kuufungua mkoa ule pamoja na Mikoa
ya Kigoma, Iringa na huko Ruvuma, itaweza kutuunganisha vizuri sana. Kwa hiyo, mimi niwaombe Kiwanja cha Ndege cha Mpanda kitatusaidia sana kama mtakifungua ili kuweza kukuza utalii katika Mbuga yetu ya Katavi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilishawaambia kwamba ile mbuga ni very unique, ina wanyama unique kama watu wake wenyewe walivyo unique. Kwa hiyo, niwaombe sana muitangaze mbuga hii. Tuna twiga zeruzeru tunamwita Wamweru, nyie mlishaona twiga zeruzeru? Hakuna, hayupo mbuga yote tembea utamkuta Katavi na ukimuona una bahati sana. Kwa hiyo, naomba Kiwanja kile cha Ndege cha Mpanda kianze kutumika, kimetumia pesa nyingi sana kutengenezwa, kinapokaa bure haitusaidii tunapoteza mapato, tunapoteza pesa nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwaombe sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kupitia Wizara hii pamoja na Wizara ya Ujenzi muangalie namna gani kile kiwanja sasa kitaanza kufanya kazi na kuleta watalii katika mbuga yetu ili na sisi tuweze kunufaika na angalau na sisi tuwashangae hata Wazungu maana hatujawahi kuwaona. Tangu Mjerumani na Mrusi walivyoondoka hatujawaona tena. Kwa hiyo, wakianza kuja kule na sisi tutawashangaa kidogo inaweza kutusaidia na sisi tukaji-socialize na tukabadilika. Kwa hiyo, niwaombe sana sana, lazima tuangalie namna ya kukitumia kiwanja hicho na hizi ndege zinazoletwa ili tuweze kuongeza pato la Taifa maana mnasema mbuga za Kusini lakini sijaiona Katavi National Park. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naishukuru Serikali yangu kwa namna ambavyo inavyofanya kazi kuhakikisha inatatua matatizo ya wananchi. Pamoja na kwamba bajeti hii ni ndogo lakini naamini Wizara mnaweza mkafanya yale ambayo mmejipangia. Nawaombeni sana, sana vijiji vyangu nilivyovitaja vipatiwe visima vya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.